Mandonga: Ushahidi mwingine wa mchezo wa ngumi ulivyo njia panda 'pesa vs afya'

Chanzo cha picha, DiraMakini
Na Yusuph Mazimu, BBC Swahili
Ngumi ni moja ya michezo yenye utajiri mkubwa duniani. Kwa mujibu wa ‘IBIS World’ mapromota wa ngumi waliingiza dola $361.5 million mwaka 2019.
Inakupa picha kama mapromota wameingiza hivyo, vipi kuhusu mabondia?
Kamapuni ya Money Inc ilimuorodhesha bondia wa zamani George Foreman kama mmoja wa mabondia matajiri zaidi wa muda wote.
Floyd Mayweather Jr akiongoza orodha, wengine ni Oscar De La Hoya ambaye ni promota kwa sasa mwenye utajiri wa dola $200 million na Manny Pacquiao mwenye utajiri wa dola $190 million.
Pambano la kihistoria duniani ambalo liliingiza pesa nyingi zaidi kuwahi kutokea ni lile la Floyd Mayweather vs. Conor McGregor lililopigwa August 26, 2017.
Mayweather aliyeibuka mshindi aliondoka na dola milioni 275 huku McGregor licha ya kupoteza aliweka kibindoni dola milioni 85.
Pamoja na kuingiza fedha nyingi, mchezo huo pia ni hatari kwa afya ya mabondia, na hilo linauweka njia panda zaidi mchezo huo.
Watu 4.3 million walilipia kutazama pambano hilo, na kufanya kuwa pambano lenye thamani zaidi duniani.

Chanzo cha picha, mma
Ya Mandonga ni kielelezo cha nguvu ya masumbwi na pesa
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa ukanda wa Afrika Mashariki, Bondia mwneye mbwembwe wa Tanzania, Karim Mandonga ni biashara kubwa sasa hivi katika ngumi.
Pambano la Mandonga wala Mandonga mwenyewe hawezi kuingiza fedha kama za kina Mayweather, lakini hamasa yake ina thamani kubwa kwa ukanda wa Afrika Mashariki.
Ukiwa Promota au muandaaji wa mapambano ya ngumi, Mandonga anaweza kukuingizia pesa nzuri tu.
Ana mvuto licha ya kwamba amekuwa akipoteza mapambano yake mara kwa mara. Na pengine alivyo na matambo yake inatosha kukuonyesha alivyo na thamani na na jinsi pambano lake lilivyo 'pesa'.
Leo atakuja na ngumi ya Sugunyo, mara ngumi mpya kutoka huko jangwa la sahara kwenye upepo mkali iitwayo "MBUNGA MBUNGA" , ili mradi ni mbwembwe tu. Kwakwe akipigwa kapiga na akipiga kapiga.
Thamani na mvuto wake unamfanya kupata mapambano kila leo ya ndani na nje ya nchi.
Kwa mapromota wanapata pesa, yeye na watu wake kama makocha wanapata pesa. Hapo ndipo hoja ya pesa vs afya inapoleta kizungumkuti. Je anaruhusiwa kupiga kila siku?
Je Bondia anaweza kupigana kila siku mfululizo?

Chanzo cha picha, DiraMakini
Mandonga 'mtu kazi' alishtua umma wa wapenda ngumi Afrika Mashariki ilipotangazwa wiki hii kwamba amesimamishwa kwa ajili ya suala la kitabibu.
Kamisheni ya Ngumi za kulipwa Tanzania (TPBRC), inayosimamia mchezo huo nchini huo, ilichukua uamuzi huo kutokana na kuingia na wasiwasi juu ya afya ya mandonga kufuatia kuchapwa mara mbili mfululizo katika kipindi cha wiki moja.
Alichapwa na Moses Golola aliyeshinda kwa Technical Knock Out Julai 29, 2023 jijini Mwanza na wiki moja kabla ya pambano hilo, Julai 22, 2023 Mandonga alitoka kutandikwa na Mkenya Daniel Wanyonyi.
Matokeo ya uchunguzi wa kitabibu yaliyofanyika Jumanne wiki hii, yakaonyesha kuwa Mandonga hajaathirika katika maeneo yaliyofanyiwa uchunguzi ya kichwani na atazichapa tena Agosti 27, 2023 huko visiwani Zanzibar.
Lengo la TPBRC lilikuwa jema tu kuangalia afya ya Mandonga, kwakuwa amekuwa akipigana mara kwa mara lakini zaidi amepoteza kwa TKO katika pambano lake la mwisho. Lakini je anaruhusiwa kupigana mapambano mfululizo?
'Hakuna sheria inayomzuia bondia kupigana, anaweza kupigana anavyopenda, lakini la muhimu ni kwamba saa 24 kabla ya pambano awe ametoka kwa daktari (kupimwa)", anasema Anthony Rutta, mmoja wa wadau wakubwa na viongozi wa muda mrefu wa ngumi Tanzania.
Hili ni dhahiri, hata ukirejea kwenye michezo kama ya Olympic zinazojumuisha ngumi za 'amature', unakuta bondia amepigana leo kaingia robo fainali, kesho anapigana tena, muhimu lazima apimwe kabla ya pambano.
Lakini kuna kupigwa kwa Technical Knock Out (TKO) na Knock Out (KO) kunatoa salama ya kwamba uendelee kupigana tena kesho ama la.
"Ukipigwa TKO, kwamba umepigwa mpaka refa anahesabu, umeinuka bado una nguvu za kuendelea, lakini refa kaona kwamba huyu mtu anaweza kupata madhara, au refarii kasimamisha pambano, au umepata maumivu kidogo, umechanika juu ya jicho, huyu hana kizuizi chochote, baada siku kadhaa, wiki moja mbili anaweza kupigana tena", anasema Rutta na kuongeza "Ukipigwa KO, ambayo umedondoshwa kabisa huwezi kuinuka, kiuhalisi ni miezi mitatu hatakiwi kucheza".

Chanzo cha picha, Getty Image
Kila mmoja, mfuatiliaji wa ngumi duniani anamjua, Muhammed Ali, bingwa huyu wa dunia wa zamni na anayetajwa kama bondia bora zaidi kuwahi kutokea duniani alilazimika kupigana mara 6 mwaka 1972. Ili kupata nafasi ya kuwania mkanda.
Unaweza kupigana kila wakati ili ili kukidhi masharti ya ngumi, yanayotaka upigane na wapinzani kadhaa ili kufikia vigezo vya kuwania mkanda, au upaswi kukaa bila kupigana kwa sababu ya viwango lakini kama unashikilia mkanda fulani, ni lazima upigane ndani ya siku 90 kwa mfano kutetea mkanda, au usikae bila kutete ndani ya kiezi 9.
Bondia Sonny Liston ni mfano muhimu, alitakiwa kuwapiga mabondia 6–7 solid kabla ya kupata pambano dhidi ya bingwa wa dunia wa wakati huo miaka ya 60s na 70s, Floyd Patterson.
Masumbwi na afya
Juni 5, 2022 Simiso Buthelezi, bondia wa Afrika Kusini alifariki siku mbili baada ya pambano lake na Siphesihle Mntungwa.
Kwenye pambano hilo, alionekana kama hayuko sawa, akipiga ngumi hewa hovyo upande ambao mpinzani wake hayupo. Walimuoana hatyuko sawa kichwani akakimbizwa hospitali akapoteza maisha siku mbili baadae.
Januari 7, 2022 masuwmbi ilimpoteza bondia mwingine wa Urusi, Arest Saakyan ambaye alikufa siku 10 baada ya pambano lake la raundi 8.
Wako wengi tu waliopoteza maisha ulingoni na nje ya ulingo.
Wapo waliokuja kupata viharusi, wapo waliokuja kuchanganyikiwa na madhara mengine kutokana na ngumi.
Muhammed Ali pamoja na kuingiza pesa nyingi, ni miongoni mwa mabondia waliokuja kupata madhara ya kiafya baadaye.

Chanzo cha picha, Getty Image
Kama ilivyo michezo mingine ukiweko soka, Mchezo wa ngumi unahitaji bondia aingie ulingoni akiwa timamu kiafya. Vyama na Kamisheni zote za ngumi duniani zinakubaliana kwenye hili na zimeweka sheria inayomtaka bondia kupimwa afya yake angalau saa 24 kabla ya kupanda ulingoni.
World Boxing Association (WBA) , World Boxing Council (WBC), World Boxing Organization (WBO) na International Boxing Federation (IBF) ambavyo ni vikubwa zaidi, vyote vinasisitiza afya.
Leo kufanyika Tanzania, kwa Mandonga kutakiwa kupima, limeonekana kama jambo tofauti kidogo.
Je mabondia wetu hufanya hivyo?
"Sidhani sana, naona kinavhofanyika siku moja kabla ya pambano ni kupima uzito wao na kuhamasisha pambano ili kuvutia mashabiki kuingia kutazama, mapromota wanaangalia pesa si afya ya bondia", anasema Raphael Magoha, mdau wa ngumi anayeungwa mkono na Seif Hopkins.
"Mie pia nina mashaka, maana hatujawahi kusikia katika nchi zetu hizi kwamba pambano limehairishwa kwa sababu bondia amekutwa na tatizo fulani la kiafya", anasema Seif.
Pengine hoja ya Seif inajielekeza kwenye mtazamo wa wanaoandaa mapambano, kwamba ameshatumia fedha zake kuandaa pambano husika, ameshafanya matangazo, amelipia ukumbi, amendaa tiketi, vifaa, ulinzi leo pambano lisifanyike kwa sababu ya afya? nani atafidia hasara atakayopata?
Kwa hoja hizi unagundua , suala la afya linabaki kuwa suala la bondia mwenyewe zaidi
Hofu ya wengi ilikuwa si anachokipata Mandonga ama promota kibiashara, hofu ilikuwa kwenye afya yake akiwakilisha mabondia wengine duniani wanaopigana kila leo. Hasa mara kadhaa akiangushwa chini. Asalie kupigana tu aingize pesa? au afyake yake imuelekeza apigane lini tena?












