Je, Trump anaweza kugombea urais baada ya kuenguliwa Maine na Colorado?

Chanzo cha picha, REUTERS
- Author, Tom Geoghegan
- Nafasi, BBC
Donald Trump ameenguliwa kuwania urais katika majimbo mawili ya Colorado na Maine. Ina maana gani kwa uchaguzi mkuu mwakani?
Trump yuko mstari wa mbele kupitia chama cha Republican kugombea uchaguzi wa Novemba 2024. Anatoa changamoto kwa Joe Biden katika Ikulu ya White House. Katika kampeni zake ameyataja maamuzi yote mawili kama "ya kikatili" na "jaribio la wizi wa uchaguzi."
Afisa mkuu wa uchaguzi huko Maine aliamua kuwa rais Trump hastahili kugombea kwa sababu ya vitendo vyake wakati wa ghasia katika Bunge la Mareakani. Nayo Mahakama ya juu zaidi ya Colorado ilitoa uamuzi kama huo.
Lakini bado haijafahamika iwapo jina la Trump litaonekana kwenye kura wakati majimbo hayo mawili yatakapomchagua mgombea wao wa chama cha Republican katika miezi ijayo, kwani maamuzi yote mawili yanasubiri mchakato wa rufaa.
Kwa nini Maine ilitoa uamuzi huo?
Tofauti na Colorado, ambapo Mahakama ya Juu ya jimbo hilo ilitoa uamuzi wa kumzuia Trump. Maine iliamuliwa na afisa mkuu wa uchaguzi kwa kufuata kipengele katika katiba.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jimbo la Maine, Shenna Bellows, ambaye ni mwanachama wa chama cha Democratic, alitoa uamuzi wa kurasa 34 uliosema, 'Trump lazima aondolewe kwenye kinyang’anyiro cha mchujo wa chama cha Republican kwa sababu ya Kifungu cha 3 cha Marekebisho ya 14 ya Katiba.'
Kifungo cha 3 kinakataza watu wanaojihusisha na "uvamizi au uasi" kushikilia ofisi ya shirikisho.
Agizo lake lilisema Trump "katika muda wa miezi kadhaa na kufikia Januari 6 2021, alitoa taarifa za uwongo kuhusu uchaguzi ili kuwachochea wafuasi wake na kuwaelekeza kwenda Capital (Bunge la Marekani)."
Bi Bellows, alishutumiwa kwa kufanya uamuzi uliochochewa kisiasa na kampeni ya Trump. Lakini alikanusha hilo na kusema "unatokana na msingi wa kisheria."
Akizungumza na BBC baada ya uamuzi wake, Bi Bellows alisema ni wajibu wake kuzingatia sheria za uchaguzi katika jimbo lake, na anatumai "Mahakama kuu itasuluhisha suala hili nchi nzima."
Nini kilitokea Colorado?
Tarehe 19 Disemba, Mahakama ya Juu ya Colorado ilisema imepata "ushahidi wa wazi na wa kuridhisha kwamba Rais Trump alihusika katika uasi."
Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Kifungu cha 3 kutumika kumuondoa mgombeaji urais.
Uamuzi huo mrefu wa kurasa 213 ulisema vitendo vya Trump kuelekea Januari 6, 2021 vilijumuisha uasi.
Mawakili wake walisema hapaswi kuondolewa kwa sababu hakuhusika na ghasia hizo. Pia walieleza Trump hajashtakiwa kwa kuchochea uasi.
Je, Trump anaweza kugombea 2024?
Ndio. Maamuzi haya yanahusu Colorado na Maine tu. Saa chache baada ya uamuzi wa Maine, Waziri wa Mambo ya Nje wa California aliyechaguliwa na chama cha Democrat, alipuuza wito wa kumwondoa Trump kwenye mchujo wa chama cha Republican - akisema ni suala la mahakama.
Mahakama ya juu ya Michigan wiki hii ilikataa kusikiliza kesi iliyokuwa ikitaka Trump kuondolewa.
Trump yuko mbali sana na wapinzani wake wa chama cha Republican - kwa hivyo bado anaweza kushinda uteuzi wa chama chake bila kushindana huko Colorado au Maine.
Colorado na Maine, Joe Biden alishinda dhidi ya Donald Trump 2020 kwa tofauti kubwa, na kuna uwezekano Trump hatahitaji kushinda majimbo hayo ili kuingia Ikulu ya White House kwa mara nyingine.
Nini kitatokea baadaye?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kuna uwezekano Mahakama kuu ya Marekani itaingilia kati kutoa uamuzi ambao utatumika kitaifa. Kwa sababu Republican imekata rufaa dhidi ya uamuzi wa jimbo hilo kwenye Mahakama ya Juu.
Mahakama kuu ya Marekani itaamua muda wa kusikilizwa kesi hiyo - kwani haijabainika ni lini. Jina la Trump litasalia kwenye kura huko Colorado hadi Mahakama kuu itakapotoa uamuzi au hata iamue kutosikiliza kesi hiyo.
Uamuzi wa Maine pia umesitishwa kusubiri rufaa ya kisheria katika mahakama za serikali. Uamuzi wowote wa Mahakama Kuu ya Marekani unaweza kutumika kitaifa.
Majaji wa Marekani watalazimika kuzingatia mabishano ya kisheria ambayo yatachukua muda, lakini watakuwa chini ya shinikizo la kuamua kabla ya uchaguzi wa mchujo wa Colorado na Maine wa Machi 5.
Mahakama hiyo imebadilika na kuwa na misimamo ya kihafidhina zaidi katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na majaji watatu ambao waliteuliwa na Trump alipokuwa rais.
Kuna masuala mawili muhimu ya kisheria ya kuzingatia. Mojawapo; vitendo vya Trump kuelekea uvamizi wa Januari 6 ni sawa na uasi. Pili; ni ikiwa Kifungu cha 3 kinachowazuia wagombea kinajumuisha na marais.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi












