Jinsi unavyoweza kubaini picha za 'kukamatwa' kwa Trump ni za uongo

Trump

Chanzo cha picha, TRUTH SOCIAL

Picha ghushi zilizoundwa kwa kutumia zana za akili bandia (AI) zinazomuangazia Donald Trump zimeonekana kwenye mitandao ya kijamii wiki iliyopita.

Baadhi ya picha hizo zilionyesha kukamatwa kwa rais huyo wa zamani, ambaye huenda akakabiliwa na mashtaka ya kulipa pesa za kimnyamazisha mwanamke anayedaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi naye. Bado hajafunguliwa mashtaka ya uhalifu.

Wengine walioshirikisha picha hizo walionyesha kuwa zilikuwa za uwongo, na hazikuonekana kuwadanganya watu wengi - lakini wachache walionekana kuamini zilikuwa sahihi.

Siku ya Alhamisi, Bw Trump pia alishiriki picha iliyoundwa na AI kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social. Ilionyesha akipiga magoti akiwa katika maombi.

Lakini je unawezaje kutofautisha picha halisi na ile ambayo ni bandia?

Je, kuna kitu kinaonekana 'kutiliwa shaka'?

Trump

Chanzo cha picha, TWITTER

Picha zinazosambazwa mtandaoni, kama iliyo hapo juu, zinaonekana kuwa za kweli - zaidi kama picha za kisanii kuliko picha zilizopigwa wakati wa tukio.

Uangalizi wa karibu unaonyesha wazi kuwa kuna kitu hakijakaa sawa.

Angalia katikati ya picha. Mkono wa Bw Trump ni mfupi sana, na afisa wa polisi aliye upande wa kushoto anashika kitu ambacho kinafanana na ukucha kuliko mkono wa mwanadamu.

Vile vile, ukizingatia shingo ya Bw Trump, utagundua kuwa kichwa chake kinaonekana kana kwamba kimewekwa juu ya picha hiyo.

Henry Ajder, mtaalamu wa AI na mtangazaji wa kipindi cha redio cha BBC The Future Will be Synthesised, anasema teknolojia ya sasa si nzuri sana katika kuonyesha baadhi ya sehemu za mwili, hasa mikono.

"Ukivuta karibu picha mara nyingi unaweza kuona kutofautiana kama vile idadi ya vidole," anasema.

Watu wengine wanasemaje?

Uchunguzi rahisi wa tovuti chache za habari ni njia ya uhakika ya kuthibitisha kwamba Bw Trump hajakamatwa au hata kufunguliwa mashtaka - angalau, bado.

Ikiwa Bw Trump atakabiliwa na mashtaka, kukamatwa kwake kutakuwa habari kuu kote duniani. Na tukio hilo lingevuma katika vyombo vya habari kama kweli rais wa zamani angeonekana kwa namna fulani akiwakimbia polisi.

Wazo lingine nzuri ni kufikiria juu ya muktadha ambao picha inashirikiwa. Nani anaishiriki - na nia yao ni nini?

Mara nyingi watu hushiriki picha ili kukuza maoni yao mapana ya kisiasa, hata kama hawajaangalia kama picha hizo ni za kweli, Bw Ajder anasema.

"Tumeona mifano mibaya ya taarifa bandia kama vile rekodi ya sauti ya Nancy Pelosi kupunguzwa kasi ili kumfanya asikike kana kwamba amelewe," anaongeza. "Huo ulikuwa upotoshaji mbaya sana na bado watu wengi walihadaika - au angalau walikaribia kuamini."

Maelezo ya ajabu zaidi

Trump

Chanzo cha picha, ELIOT HIGGINS

Ukiangalia kwa karibu picha zenyewe zinaonyesha maelezo ya llutiliwa shaka zaidi.

Nyuso za ngozi zisizo asilia zilizo na nta au ukungu ni dalili tosha kwamba picha hiyo ni ghushi.

Katika picha iliyo hapo juu, mtu mwenye uso ulio na ukungu anaonekana vizuri katikati-kulia. Na nywele za Bw Trump zinaonekana kuwa na ukungu, huku uso wake ukionekana vizuri.

Je, ni kweli hao polisi wanamfukuza Trump au wanaangalia kitu kingine?

Chanzo cha picha, ELIOT HIGGINS

Maelezo ya picha, Je, ni kweli hao polisi wanamfukuza Trump au wanaangalia kitu kingine?

Teknolojia ya AI pia bado haijapata taswira sahihi ya macho.

Katika picha iliyo hapo juu, maafisa wanaonekana kumkimbiza Bw Trump - lakini wanaangalia upande tofauti kabisa.

Kuna shida huko mbele?

Wataalamu wa AI waliiambia BBC kwamba ingawa taswira za uwongo "si jambo jipya", kasi ya maendeleo katika uwanja huo, na uwezekano wa kutumiwa vibaya, ni jambo la kutia wasiwasi.

"Maudhui ya syntetisk yanabadilika kwa kasi na pengo kati ya maudhui halisi na bandia linazidi kuwa vigumu kufasirika," anasema Mounir Ibrahim wa Truepic, kampuni ya uchambuzi wa maudhui ya kidijitali.

Wataalamu hao wanakubali kwamba umaarufu wa Bw Trump hurahisisha kugundua picha bandia. Lakini picha za watu wasiojulikana zinaweza kufanya kazi kuwa ngumu zaidi - na teknolojia inaboreka kila uchao.