Rais wa zamani Marekani na Nyota wa picha za ngono: Kwa nini simulizi hii ya Trump na Daniels ni muhimu

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais wa zamani Donald Trump anakanusha madai yaliyotolewa na Stormy Daniels

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump alisema anatarajia kukamatwa Jumanne kutokana na malipo ya $130,000 aliyotoa mwaka 2016 kwa nyota wa picha za ngono yaani ponografia Stormy Daniels.

Uamuzi kuhusu hatima ya kesi hiyo ni wa Wakili wa Wilaya ya New York, Alvin Bragg.

Inategemea majadiliano yao, Trump anaweza kuwa rais wa kwanza wa Marekani kukabiliwa na mashtaka ya uhalifu.

Hata hivyo chama cha Republican kimekanusha madai hayo.

Tunachojua kufikia sasa kuhusu kesi hiyo.

Stormy Daniels ni nani?

Stephanie Clifford alizaliwa mwaka 1979 katika Jimbo la Louisiana.

Jina la kisanii Stormy Daniels lilitokana na jina la binti wa mpiga besi Nikki Sixx, Storm, na whisky ya Marekani Jack Daniels.

Alianza tasnia ya filamu ya watu wazima kama mwigizaji, na kuanzia 2004 na kuendelea, alianza kuelekeza na kuandika pia.

Unaweza pia kumtambua kwa maonyesho yake maalum katika filamu za ‘The 40 Year Old Virgin na Slightly Pregnant, pamoja na video ya wimbo Wake up call, ya kundi la Maroon Five.

Daniels pia alipanga kugombea kiti cha useneta huko Louisiana mnamo 2010, lakini alijiondoa baada ya kusema kwamba hakuchukuliwa kwa uzito.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Stormy Daniels anasema alikutana na Trump mnamo 2006

Je, ni mashtaka gani dhidi ya Trump?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Simulizi za Trump na Daniels zilijitokeza mnamo Julai 2006.

Anasema alikutana naye kwenye mashindano ya hisani ya gofu katika Ziwa Tahoe, eneo la mapumziko kati ya California na Nevada.

Katika mahojiano ya 2011 na jarida la In Touch Weekly, ambayo hayakuchapishwa kikamilifu hadi Januari 2018, Daniels alisema kwamba Trump alimwalika kwa chakula cha jioni na kwamba alikwenda kukutana naye katika chumba cha hoteli.

"Alikuwa amejitupa kwenye kochi, akitazama televisheni au kitu," alisema katika mahojiano hayo. "Alikuwa amevaa suruali ya kulalia."

Daniels anadai wawili hao walifanya mapenzi chumbani, jambo ambalo wakili wa Trump anasema mteja wake "anakanusha vikali."

Ikiwa maelezo ya Daniels ni ya kweli, ina maanisha haya yote yalitokea miezi minne tu baada ya kuzaliwa kwa mwana mdogo wa Trump, Barron.

Katika mahojiano ambayo yalipeperushwa kwenye runinga mnamo Machi 2018, Daniels alisema alitishiwa kukaa kimya kuhusu mahusiano hayo.

Alidai kuwa alifuatwa mwaka wa 2011 na mwanamume katika eneo la maegesho la Las Vegas, muda mfupi baada ya kukubali mahojiano ya In Touch Weekly. Mwanamume huyo anadaiwa kumwambia "wachana na Trump".

Kwa nini simulizi hii iliibuka?

Mnamo Januari 2018, Jarida la Wall Street lilichapisha nakala iliyoonyesha kwamba wakili wa wakati huo wa Trump, Michael Cohen, mnamo mwezi Oktoba 2016 - mwezi mmoja kabla ya uchaguzi wa rais wa Marekani, ambao Republican ilishinda – alifanya malipo ya $ 130,000 kwa Daniels.

Gazeti hilo lilisema kuwa pesa hizo zilikuwa sehemu ya makubaliano ya usiri na nyota huyo wa picha za ngono ili asizungumze hadharani kuhusu uhusiano aliokuwa nao na Trump.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kulingana na Daniels, yeye na Trump walikuwa na uhusiano miezi minne baada ya kuzaliwa kwa Barron, mtoto wa mfanyabiashara na Melania Trump.

Je, kulikuwa na uharamu wowote na hilo?

Malipo yenyewe si kinyume cha sheria.

Hata hivyo, Trump alipomrudishia Cohen, rekodi ya malipo ilikuwa ya ada za wakili.

Kwa waendesha mashtaka wa New York, kughushi ni kosa katika jimbo.

Waendesha mashtaka wanaweza pia kudai kuwa sheria za uchaguzi zilikiukwa, kwa sababu jaribio la kuficha malipo yaliyofanywa wa Daniels lilikuwa na nia ya kuficha jambo hilo kwa umma.

Trump atashtakiwa?

Uamuzi wa kuwasilisha mashtaka au la unategemea Wakili wa Wilaya Alvin Bragg.

Amekusanya baraza kuu la mahakama kutathmini kama kuna ushahidi wa kutosha wa kumshtaki, na ndiye pekee anayejua kama - au lini - hati ya mashtaka itatangazwa.

Mawakili wa Trump walisema wiki ya Machi 13 kwamba rais huyo wa zamani alipewa nafasi ya kufika mbele ya mahakama kuu, ambayo inachukuliwa kuwa ishara kwamba uchunguzi unakaribia kukamilika.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Michael Cohen alikamatwa kwa jukumu lake katika malipo hayo

Pia walipuuza utabiri kwamba Trump angekamatwa na shutuma ambazo anazijua kwa sababu angepewa taarifa mapema.

Kulingana na wanasheria hao, rais huyo wa zamani alifikia hitimisho hili kufuatia machapisho kwenye vyombo vya habari.

Michael Cohen alihukumiwa kifungo mwaka 2018 baada ya kukiri makosa ya ukiukaji wa fedha za kampeni zinazohusiana na malipo ya Daniels na mwanamke mwingine wakati wa kampeni ya urais 2016.

Stormy Daniels pia alikutana na waendesha mashtaka waliohusika katika uchunguzi huo.

Kwa nini yote haya yana umuhimu?

Wafuasi wa Rais Trump, hata wale wa haki za kidini, wamepuuza kwa kiasi kikubwa tabia yake ya zamani na shutuma za wanawake dhidi yake.

Lakini kashfa ya Stormy Daniels inaweza kumfanya Trump kuitwa kutoa ushahidi mahakamani - na kupelekea kufichuliwa zaidi kwa kesi hiyo wakati ambapo Republican inatayarisha mgombea mpya wa urais.

Kushtakiwa au hata kupatikana na hatia hakutamzuia Trump kuendelea na kampeni yake ya urais, anaeleza mwandishi wa BBC Amerika Kaskazini Anthony Zurcher.

"Ukweli ni kwamba, hakuna chochote katika sheria ya Marekani kinachomzuia mgombea anayepatikana na hatia ya uhalifu kufanya kampeni na kuhudumu kama rais - hata kutoka gerezani."

"Hata hivyo, kukamatwa kwa Trump bila shaka kutatatiza kampeni yake ya urais."