Je, Trump anaweza kufungwa jela na maswali mengine muhimu

Trump

Chanzo cha picha, Reuters

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump amefunguliwa mashtaka kuhusiana na matukio ya ghasia za tarehe 6 Januari 2021 katika Bunge la Marekani.

Mwanasiasa huyo wa chama cha Republican anakanusha kufanya makosa na kuelezea kesi hiyo kuwa ya "kichekesho".

Tayari ameshtakiwa katika kesi nyingine mbili - kwa kupatikana na nyaraka za siri na kughushi rekodi za biashara ili kuficha malipo ya pesa kwa nyota wa filamu za ngono.

Haya hapa ni baadhi ya maswali muhimu yanayozunguka kesi hiyo.

Je, anakabiliwa na mashtaka yapi?

Bw Trump, ambaye alishindwa katika uchaguzi wa urais wa 2020 na Joe Biden, ameshtakiwa kwa kupanga njama ya kubatilisha matokeo hayo.

Anatuhumiwa kwa makosa manne:

  • njama za kuilaghai Marekani
  • njama za kuvuruga mchakato rasmi
  • kizuia kufanyika kwa shughuli rasmi
  • njama dhidi ya haki za raia

Mashtaka haya yanahusiana na hatua ya Bw Trump kwa muda wa zaidi ya miezi miwili mara baada ya siku ya uchaguzi (Novemba 3) hadi siku alipoondoka Ikulu ya Marekani tarehe 20 Januari.

Shitaka la kwanza linaangazia madai ya majaribio ya kutatiza ukusanyaji, kuhesabu na uidhinishaji wa kura.

Shitaka la pili na la tatu na linaangazia madai ya majaribio ya kuzuia uidhinishaji wa kura za wajumbe maalum katika Bunge la Marekani tarehe 6 Januari, ambayo iliishia katika ghasia katika majengo ya bunge.

Shitaka la nne ni la madai ya kujaribu kuingilia haki ya wananchi ya kupiga kura na kuhesabiwa kura zao.

Mashtaka ni mazito kiasi gani ikilinganishwa na mashitaka ya awali?

Hili ni shtaka la tatu dhidi ya Bw Trump na baadhi ya wataalamu wa sheria wamesema huenda isiwe kesi kali zaidi. Anaweza kukabili hatari kubwa zaidi ya kisheria mahali pengine.

Lakini kwa upande wa uzito wa mashtaka, haya ni makubwa zaidi na yenye athari, asema mhariri wetu wa Amerika Kaskazini, Sarah Smith.

Hii ni mara ya kwanza anashtakiwa kwa jambo ambalo lilifanyika akiwa bado ofisini, anasema.

Ingawa wakili maalum Jack Smith alikaribia kumshtaki Bw Trump kwa kuchochea watu ambao walishambulia Bunge la Marekani, mwendesha mashtaka alisema "ilichochewa na uwongo, uwongo wa mshtakiwa".

Mwendesha mashtaka wa zamani Renato Mariotti aliambia BBC Today kwamba hili lilikuwa shtaka la kwanza katika historia ya Marekani ambalo lilikuwa likimhusisha rais wa zamani kwa mwenendo ambao ulikuwa wa kipekee katika ofisi yake, kwa maneno mengine "kujaribu kusalia madarakani na kuzuia shughuli ya kupokezana madarakani kwa amani. "

Nini kitakachofuata baadaye?

Bw Trump anatarajiwa kufika mahakamani mjini Washington DC siku ya Alhamisi. Bado haijabainika ikiwa atahudhuria kibinafsi au kwa njia ya kimtandao.

Mshauri maalum Jack Smith, anayeongoza uchunguzi anataka "kesi kumalizika haraka", lakini hilo huenda lisifanyike kwa sababu kadhaa.

Kesi hii itakuwa inashindana kwa muda na kesi nyingine dhidi yake - zote haziwezi kuendeshwa kwa wakati mmoja. Pia hakuna uwezekano wa kuratibiwa kwa matukio muhimu wakati wa uchaguzi, kama vile Kongamano la Kitaifa la Republican wakati mgombeaji urais anachaguliwa rasmi.

Na kama Bw Mariotti anavyoonyesha, kuna njia nyingi katika mfumo wa haki wa Marekani kuruhusu muda zaidi wa kesi.

Kwa hivyo kuna uwezekano kwamba Bw Trump huenda tayari akawa amechaguliwa kuwa rais wakati kesi inaanza

Je, Trump anaweza kufungwa jela na bado agombee urais?

Rais huyo wa zamani, akiwa na umri wa miaka 77, anakabiliwa na uwezekano wa kifungo kigumu jela iwapo atapatikana na hatia.

Jaji aliyepewa jukumu la kusimamia kesi hiyo, Tanya Chutkan, ni mteule wa Obama, anayejulikana kwa kuhumu vikali kesi zingine za Januari 6.

Bw Trump pia anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 20 jela katika kesi ya nyaraka za siri.

Lyndon LaRouche

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Lyndon LaRouche, aliyepatikana na hatia ya ulaghai, aligombea urais mara nane

Chini ya sheria za Marekani, hakuna kinachomzuia mtu kuwania wadhifa huo ikiwa anakabiliwa na mashtaka ya uhalifu, au hata akiwa gerezani.

Bila shaka hii haimaanishi kwamba wapiga kura wangetaka kumuunga mkono mgombeaji kama huyo.

Viongozi wawili wa Marekani wamewahi kugombea urais wakiwa na hatia za uhalifu - mgombea wa kisoshalisti Eugene Debs mwaka 1920, alihukumiwa kwa hotuba ya kupinga vita mwaka 1918; na Lyndon LaRouche, aliyepatikana na hatia ya ulaghai, aligombea urais mara ya nane 1992 akiwa gerezani huko Minnesota.

Wote wawili walishindwa katika uchaguzi.

Je, Trump anaweza kujisamehe ikiwa atashinda uchaguzi?

Baadhi ya wachanganuzi wamependekeza kuwa Bw Trump anaweza kujaribu kujisamehe ikiwa atapatikana na hatia kisha akashinda uchaguzi.

Hali hii inayowezekana haijajaribiwa na sheria za Marekani, ambayo ina maana kwamba Mahakama ya Juu inaweza kuhitaji kuingilia kati.

Anaweza pia kujaribu kufanya kesi hiyo itupiliwe mbali ikiwa alichaguliwa kuwa rais wakati bado inaendelea.

Mgombea mmoja mpinzani wa uteuzi wa chama cha Republican, gavana wa zamani wa Arkansas, Asa Hutchinson, aliuambia mtandao wa NBC kuwa matukio yote mawili yanawezekana lakini akasema kwamba kujisamehe "sio kitu ambacho katiba inakusudia".

Aliongeza kuwa hatua kama hiyo itakuwa "isiyofaa" na "isiyo sawa".

Hata hivyo, mmoja wa wapinzani wa Bw Trump, Vivek Ramaswamy, ameapa kumsamehe Bw Trump iwapo atachaguliwa kuwa rais.

Naye mpinzani wake mkuu wa chama cha Republican, Ron DeSantis, aliambia CNN kuwa haitakuwa "vizuri kwa nchi" kwa Bw Trump kufungwa jela.