Namna tuhuma za hongo zinazomwandama Adani zitaathiri uchumi na siasa za India

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Soutik Biswas
- Nafasi, Mwandishi wa BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Wiki chache zilizopita, bwanyenye mkubwa duniani Gautam Adani ,alisherehekea ushindi wa rais mteule Donald Trump na kutangaza kuwekeza dola bilioni 10 katika miradi ya kawi na miundo msingi nchini Marekani.
Bilionea ambaye ni raia wa India,mwenye umri wa miaka 62 na rafiki wa karibu wa waziri mkuu wa India Narendra Modi, sasa anadaiwa kuhusika katika hongo ya mabilioni ya dola na udanganyifu ambayo huenda ikamharibia sifa India na pia mataifa ya ughaibuni.
Waendesha mashtaka wa Marekani wamemshutumu kwa kupanga mpango wa kutoa rusha ya takriban dola milioni 250 (Sh35 bilioni) na kuficha ili kukusanya fedha zaidi nchini Marekani.
Wanamtuhumu bwana Adani pamoja na wakurugenzI wake walilipa hongo kwa maafisa wa serikali ya India ili kupata kandarasi za zaidi ya dola bilioni 2 ndani ya miaka 20 ijayo.
Hata hivyo shirika la Adani limekanusha mashtaka hayo, wakiyataja "siyo ya msingi".
Lakini hili tayari limeanza kuharibia sifa kampuni hiyo ya Adani na uchumi wa India.
Makampuni ya kundi la Adani yalipoteza thamani ya soko ya dola bilioni 34 Alhamisi na hivyo kufanya jumla ya mtaji wa masoko ya makampuni yake 10 kushuka hadi dola bilioni 147.
Adani Green Energy ,kampuni inayohusishwa na tuhuma hizo,pia ilisema haitatekeleza mpango wake wa kutoa hati fungani za dola milioni 600.
Zaidi ya hayo ,kuna maswali kuhusu athari za mashtaka haya kwa biashara na siasa za India.

Chanzo cha picha, Getty Images
Uchumi wa India umefungamana sana na Bw Adani, tajiri mkuu wa miundombinu nchini humo. Anaendesha bandari 13 (asilimia 30 ya sehemu ya soko), viwanja vya ndege saba (23% ya trafiki ya abiria), na biashara ya pili kwa ukubwa ya saruji nchini India (20% ya soko).
Akiwa na mitambo sita ya nishati ya makaa ya mawe, Bw. Adani ndiye mwekezaji binafsi mkubwa zaidi nchini India.Vile vile, ameahidi kuwekeza dola bilioni 50 katika teknolojia ya hidrojeni ya kijani na anaendesha mtandao wa bomba la gesi asilia lenye urefu wa kilomita 8,000 (maili 4,970).
Aidha,anajenga njia ndefu zaidi ya haraka ya India na anajitahidi kuboresha makazi duni makubwa zaidi ya India.Ameajiri zaidi ya watu 45,000, lakini biashara zake zinaathiri mamilioni ya watu kote nchini.
Bwenyenye Gautam Adani ni nani?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Matarajio ya kimataifa ya Bw. Adani yanahusisha migodi ya makaa ya mawe nchini Indonesia na Australia, viwanja vya ndege, na miradi ya nishati nchini Kenya na Morocco. Kundi lake linatarajia zaidi ya dola bilioni moja katika miradi ya miundombinu katika nchi za Tanzania na Kenya.Hata hivyo serikali ya Kenya siku ya Alhamisi imevunjilia mbali mikataba yake na kundi hilo la Adani.
Katika maeneo mengine, biashara ya Bw. Adani inaendana kwa karibu na vipaumbele vya sera za Waziri Mkuu Narendra Modi, kuanzia katika sekta ya miundombinu hadi hivi karibuni kwenye nishati safi.
Amefanikiwa licha ya wakosoaji kudai kuwa himaya yake ya biashara ni mfano wa ubepari , hasa kutokana na uhusiano wake wa karibu na Modi, wakiwa wote wanatoka Gujarat, na kutokana na urafiki wao tangu akiwa waziri mkuu wa jimbo hilo hadi sasa akiwa waziri mkuu wa India.
Kama ilivyo kwa wafanyabiashara wengine waliofanikiwa, Bw. Adani pia amejenga uhusiano na viongozi wa upinzani kwa kuwekeza katika majimbo yao.
“Madai haya ya hongo ni makubwa. Bw. Adani na Modi wamekuwa wakiungana kwa muda mrefu. Hii itaathiri uchumi wa kisiasa wa India,” anasema Paranjoy Guha Thakurta, mwandishi wa habari wa India ambaye ameandika sana kuhusu kundi hili la biashara.

Chanzo cha picha, AFP
Mgogoro huu unajitokeza wakati ambapo Bw. Adani amekuwa akijitahidi kurekebisha sura yake baada ya ripoti ya Hindenburg Research ya 2023, inayohusisha tuhuma za udanganyifu na ukiukwaji wa sheria kwa miongo kadhaa.
Ingawa Bw. Adani alikanusha madai hayo, yalileta athari kubwa kwenye soko la hisa na kusababisha uchunguzi wa kina na mdhibiti wa soko la India, SEBI.
“Bw. Adani amekuwa akijitahidi kurekebisha sura yake na kuonyesha kuwa madai hayo ya awali ya udanganyifu kutoka kwa Hindenburg hayakuwa ya kweli, na kwamba kampuni yake na biashara zake zilikuwa zikifanya vizuri. Kumekuwa na mikataba mipya na vitega uchumi vingi vilivyofanywa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, hivyo hili ni pigo kubwa kwa bilionea huyu ambaye alifanya kazi nzuri ya kuondoa madhara ya madai hayo,” anasema Michael Kugelman kutoka Kituo cha Wilson, mchanganuzi wa Marekani, katika mahojiano na idhaa ya BBC.

Chanzo cha picha, AFP
Tuhuma hizi za hivi punde huenda zikapunguza kasi ya kupanua kampuni ya Adani kaika mataifa ya Ughaibuni.Tayari amekosolewa nchini Kenya na Bangladesh kuhusiana na kuchukua uwanja wa ndege wa kimataifa kuuboresha na dili yenye utata ya kawi.
'Tuhuma hizi za kutoa hongo zitasitisha mkakati wake wa kupanua miashara yake ulimwneguni inayohusisha Marekani."alisema Nirmalya Kumar, Profesa wa Lee Kong Chian katika Chuo Kikuu cha Usimamizi cha Singapore, katika mahojiano na BBC.
Ni kipi kitakachofuata?
Kisiasa, kiongozi wa upinzani Rahul Gandhi ameitaka serikali kumkamata Bw. Adani na ameahidi kuhamasisha bunge kumchukulia hatua.
“Kuhonga maafisa wa serikali nchini India sio jambo jipya, lakini kiasi kilichotajwa ni cha kushangaza. Nadhani Marekani inajua majina ya baadhi ya wale waliolengwa. Hii inaweza kuleta mabadiliko katika hali ya kisiasa ya India. Kuna mengi zaidi yajayo,” alisema Bw. Kumar.
Timu ya Bw. Adani inatarajiwa kukusanya utetezi wa kisheria wa kiwango cha juu. “Kwa sasa, tuna hati ya mashtaka pekee, na mengi bado yanaendelea,” alisema Michael Kugelman.

Chanzo cha picha, AFP
Ingawa uhusiano wa kibiashara kati ya Marekani na India unaweza kuchunguzwa, haionekani kuwa na athari kubwa, hasa ikizingatiwa mkataba wa hivi majuzi wa dola milioni 500 kati ya Marekani na Bw. Adani kwa mradi wa bandari nchini Sri Lanka.
Hata baada ya madai haya mazito, uhusiano wa kibiashara kati ya Marekani na India bado ni imara.
“Uhusiano wa kibiashara kati ya Marekani na India ni mkubwa sana na wa kina. Hata na madai haya mazito dhidi ya mtu muhimu katika uchumi wa India, sidhani kama tunapaswa kuharakisha kudhani kuwa hii itavuruga uhusiano huo,” alisema Bw. Kugelman.
Pia, haijulikani ikiwa Bw. Adani atachukuliwa hatua, licha ya makubaliano kati ya Marekani na India kuhusu kurejesha kesi hizo, kwani itategemea kama utawala mpya utaendelea na kesi hizo. Bw. Baliga anaamini kuwa hawezi kuwa mwisho wa safari kwa familia ya Adani.
“Bado nadhani wawekezaji wa kigeni na benki watakuwa tayari kuunga mkono kama walivyofanya baada ya ripoti ya Hindenburg, hasa ikizingatiwa kwamba ni sehemu muhimu ya sekta zinazofanikiwa katika uchumi wa India,” alisema.
“Katika soko, inawezekana kuwa hii itapita na kutatuliwa, hasa ikizingatiwa kuwa utawala wa Donald Trump utaingia madarakani hivi karibuni,” aliongeza.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid












