Jinsi mtu wa tatu kwa utajiri duniani alivyopoteza dola bilioni 100 ndani ya siku chache

Gautam Adani ameshuka kutoka miongoni mwa watu 10 matajiri zaidi duniani

Chanzo cha picha, Getty Images

Bilionea wa India Gautam Adani amejaribu kuwatuliza wawekezaji baada ya kampuni yake kupata mshangao kwa kusitisha uuzaji wake wa hisa.

Siku ya Jumatano, Adani Enterprises ilisema itarejesha $2.5bn (£2bn) iliyopatikana kutokana na mauzo kwa wawekezaji.

Uamuzi huo hautaathiri "operesheni zetu zilizopo na mipango ya siku zijazo", Bw Adani amesema.

Hatua hiyo inakamilisha wiki yenye matukio mengi ambayo ilianza kwa kampuni ya uwekezaji ya Marekani kutoa madai ya ulaghai dhidi ya makampuni ya Adani Group.

Adani anakanusha madai hayo.

Lakini kampuni imeshuhudia $108bn zikifutwa kwnye soko la thamani katika siku chache zilizopita.

Bw Adani mwenyewe amepoteza $48bn ya utajiri wake binafsi, na sasa ni wa 16 kwenye orodha ya Forbes ya mabilionea.

Hii ilitokeaje?

Chini ya wiki mbili zilizopita, Bw Adani alikuwa mtu wa tatu tajiri zaidi duniani.

Hisa za Adani Enterprises, kampuni kuu ya kampuni yake ya bandari na nishati, zilipaswa kuanza kuuzwa tarehe 25 Januari katika toleo kubwa zaidi la hisa la upili kuwahi kutokea nchini India.

Lakini siku moja kabla ya hapo, kampuni ya uwekezaji yenye makao yake makuu nchini Marekani ya Hindenburg Research ilichapisha ripoti ikilishutumu kundi la Adani kwa miongo kadhaa ya udanganyifu wa hisa na uhasibu.

Hindenburg mtaalamu wa "mauzo ya hisa ambazo hazimilikiwi na mfanyabiashara" - kuweka kamari dhidi ya bei ya hisa ya kampuni kwa matarajio kwamba itashuka.

Kundi la Adani lilijibu kwa kuita ripoti hiyo "mchanganyiko mbaya wa habari potofu na tuhuma za zamani, zisizo na msingi na zisizothibitishwa", lakini hiyo haikutosha kuzuia hofu ya wawekezaji.

Hisa za Adani Enterprises zilianza kuuzwa tarehe 25 Januari katika toleo la hisa kubwa zaidi kuwahi kutokea nchini India

Chanzo cha picha, Getty Images

Kundi la Bw Adani lina kampuni saba zinazouzwa hadharani ambazo zinafanya kazi katika sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na biashara ya bidhaa, viwanja vya ndege, huduma, bandari na nishati mbadala.

Benki nyingi za India na kampuni za bima zinazomilikiwa na serikali ama zimewekeza au kukopesha mabilioni ya dola kwa kampuni zinazohusishwa na kampuni hizo.

Ni hilo tu?

Hapana. Wakati msukosuko wa soko ukiendelea, Kundi la Adani lilitoa pingamizi la kina lililo katika zaidi ya kurasa 400 na kuita ripoti ya Hindenburg "mashambulizi dhidi ya India".

Ilisema kuwa ilikuwa imefuata sheria zote za ndani na imetoa ufichuzi unaohitajika wa udhibiti. Pia ilishutumu ripoti hiyo kwa lengo la kuwezesha Hindenburg "kuhifadhi faida kubwa ya kifedha kupitia njia zisizo sahihi kwa gharama ya wawekezaji wengi".

Hindenburg, hata hivyo, ilisimama na ripoti hiyo na kusema kwamba Makampuni ya Adani "yameshindwa kujibu maswali yetu 62 kati ya 88".

Je, majibu ya soko yalikuwa yapi?

Mauzo ya hisa ya Adani Enterprises yalipoanza tarehe 25 Januari, ilipata jibu lililoshtua. Ni 3% tu ya hisa zake zilizokuwa zimesajiliwa kufikia siku ya pili kwani wawekezaji wa reja reja walikaa mbali.

Lakini wawekezaji wa kigeni wa taasisi na fedha za shirika zilisaidia kundi hilo - tarehe 30 Januari, Kampuni Hodhi ya Kimataifa ya Abu Dhabi, ikiungwa mkono na mwanafamilia wa kifalme wa UAE, iliwekeza dola milioni 400 katika mauzo ya hisa.

Katika harakati za dakika za mwisho, matajiri wa Kihindi Sajjan Jindal na Sunil Mittal pia walijiandikisha kwa uuzaji wa hisa katika uwezo wao wa binafsi, Bloomberg iliripoti.

Mchambuzi Ambareesh Baliga aliiambia Reuters baada ya mauzo ya hisa kwamba kikundi kimeshindwa kutimiza lengo lake la "kueneza umiliki wa hisa".

Hisa za kampuni mbalimbali za kikundi nazo ziliendelea kushuka.

Kipi kinachofuata?

Ripoti za Reuters na Bloomberg zinasema kuwa benki kuu ya India imewauliza wakopeshaji wa nchi hiyo kwa undani wa kuhusu sakata hilo.

Katika taarifa yake kwa mabadilishano ya India, Bw Adani alisema, "Mizania yetu ni mizuri sana na mtiririko wa pesa na mali salama, na tuna rekodi nzuri ya kulipa deni letu."

Lakini Edward Moya, mchambuzi katika kampuni ya udalali ya OANDA, aliiambia Reuters kwamba uondoaji wa mauzo ya hisa ulikuwa "wa kutatanisha" kwa sababu "ilipendekezwa kuonesha kampuni hiyo bado inaaminiwa na wawekezaji wake wenye thamani kubwa".

Shirika la utajiri la benki ya uwekezaji ya Marekani la Citigroup limeacha kupokea dhamana za Adani kama dhamana ya mikopo ya kiasi huku Credit Suisse ikiacha kukubali bondi za Adani Group.

Kitengo cha wakala wa ukadiriaji wa Moody ICRA kimesema kilikuwa kikifuatilia athari za maendeleo ya hivi karibuni kwenye hisa za Adani Group.

Wawekezaji wa reja reja walikaa mbali na mauzo ya hisa za Adani Enterprises

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Lakini Vinayak Chatterjee, mwanzilishi na mdhamini mkuu wa Wakfu wa Infravision, alikuwa na matumaini, akiita hali ya sasa "ni ya muda mfupi".

"Nimeangalia makampuni haya kwa robo karne kama mtaalamu wa miundombinu. Ninaona miradi mbalimbali ya uendeshaji kutoka bandari, viwanja vya ndege, saruji hadi nishati ambayo ni imara, na inazalisha mzunguko wa fedha wenye afya. Ni salama kabisa kutokana na kupanda na kushuka ya kile kinachotokea katika soko la hisa," alimwambia mwandishi wa BBC Arunoday Mukharji.

Hata hivyo, Hemindra Hazari, mchambuzi huru wa utafiti, alisema kuwa alishangaa kwamba "hatujasikia chochote kutoka kwa mdhibiti wa soko la SEBI au serikali hadi sasa".

"Walipaswa kuzungumza ili kutuliza wasiwasi wa wawekezaji," aliiambia BBC.

Suala hilo pia limezua mzozo wa kisiasa.

Bw Adani anachukuliwa kuwa karibu na Waziri Mkuu Narendra Modi na kwa muda mrefu amekuwa akikabiliwa na madai kutoka kwa wanasiasa wa upinzani kwamba amefaidika na uhusiano wake wa kisiasa, madai ambayo anakanusha.

Siku ya Alhamisi, vyama vya upinzani vilidai mjadala bungeni kuhusu hatari kwa wawekezaji wa India kutokana na kuanguka kwa hisa za kampuni ya Adani. Pia wameomba uchunguzi ufanyike kuhusu madai ya Hindenburg.