Mauaji ya wivu wa kimapenzi Tanzania, yalianza kama kipele sasa ni jipu la kutumbuliwa

love

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Yusuph Mazimu
    • Nafasi, BBC Swahili

'Mapenzi hayana tiba lakini ndiyo dawa pekee ya magonjwa yote' ni kauli iliyowahi kutolewa na mwandishi nguli wa riwaya, mashairi na mwandishi wa nyimbo nchini Cadana, Leonard Cohen. Cohen anashabihisha kauli yake na utamu na uzuri wa mapenzi.

Mapenzi hujengwa na hisia, zinazowaunganisha watu wawili hasa mwanamke na mwanaume wanaoamua kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na mwishowe wengine huishia kuanzisha familia kabisa.

Lakini vitendo vya mauaji na ukatili mwingine wa vipigo vinavyoendelea sasa dunaini vikihusisha wapenzi umekuwa mjadala mkubwa.

Katika siku za hivi karibuni, ripoti na taarifa kuhusu kuenea kwa vitendo vya mauaji yanayohusishwa na wivu wa kimapenzi nchini Tanzania vimezua mjadala. Huko nyuma hayakusikika sana, ila kwa sasa yameonekana kushamiri. Swali la kujiuluiza kwanini mauaji haya na Je nini kinachoendelea nyuma ya pazia kuhusu mauaji haya?

Takwimu muhimu kuhusu mwendendo wa mauaji ya wivu wa kimapenzi duniani

Umoja wa Mataifa, UN unasema, mauaji baina ya wapenzi yanaongezeka hasa kutokana na wivu wa kimapenzi. Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha wanawake ndio waathirika zaidi wa mauaji hayo, ambapo 82% ya waliouawa mwaka 2017 walikuwa wanawake na 12% tu walikuwa wanaume.

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa asilimia 40% ya vifo vya wanawake duniani na asilimia 6% ya vifo vya wanawake vinatokea kwenye mikono ya wapenzi wao. Kwa takwimu hizi nyumbani, ama kwenye mikono ya wapenzi inaonekana ni mahala hatari zaidi kuishi.

Kwa Afrika hali ni mbaya zaidi, karibu robo tatu (69%) ya wanawake waliouawa mwaka 2017 kwa makusudi waliuawa na wapenzi wao.

'kila siku, wastani wa wanawake 137 wanuawa na wenza wao', alisema Phumzile Mlambo-Ngcuka, aliyekuwa Mkurugenzi mtendani wa shirika la Umoja wa Mastaifa linalohusika na masuala ya wanawake UN Women katika taarifa iliyotolewa miezi 24 iliyopita.

Wastani wa matukio 20 ya mauaji ya mapenzi huripotiwa katika kipindi cha miezi miwili Tanzania

Ingawa hakujatolewa takwimu rasmi za kitaifa katika siku za karibuni, takwimu za Jeshi la Polisi za zilizotolewa Julai, 2021 zilionyesha katika kipindi cha miezi miwili tu Mei mpaka Juni, 2021 mauaji yalikuwa 275 na kati ya hayo mauaji ya wivu wa mapenzi yalikuwa 21.

Hii inakuonyesha makadirio ya matukio angalau 10 kwa mwezi au 20 kwa miezi miwili, ukirejea taarifa hii ya Polisi, ingawa inaweza kuwa chini ama juu zaidi ya hayo.

'mie naamini matukio yanayoripotiwa ni machache, mengine yanazimwa kindugu au mengine yanapotoshwa, ukweli idadi inaweza kuwa kubwa maradufu', anasema Machia Shija mkazi wa Dar es Salaam.

Mumbai Live

Chanzo cha picha, Mumbai Live

Kituo cha Sheria na haki za binadamu nchini Tanzania, LHRC, kiliwahi kukusanya matukio makubwa ya aina hiyo katika miaka ya hivi karibuni. Mwaka 2017, kilikusanya matukio makubwa 13 na mwaka 2020 matukio yaliongezeka mpaka 39 yaliyotokana na wivu wa kimapenzi. Lakini kituo hicho kinasema mwezi Mei pekee mwaka huu, kumeripotiwa matukio 7 ya mauaji yatokanayo na wivu wa kimapenzi huku mwaka 2021 kuliripotiwa kuwa na mauaji ya ina hiyo 35, ambapo wanaume waliouawa walikuwa 4 na wanawake 31 sawa na asilimia 89%.

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga ameiambia BBC kwamba vitendo vya mauaji ya wivu wa mapenzi linapaswa kuchukuliwa kwa upana wake ili kulishughulikia lakini sio kwa namna moja tu'.

Anasema hivyo akirejea tukio la juma lililopita, lililoripotiwa na Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza huko Buswelu la mke (Salha) kuuawa kwa kupigwa risasi 7 kichwani na mumewe ambaye nayeye alidaiwa kujiua kwa risasi.

Mwanza

Chanzo cha picha, Google

Maelezo ya picha, Tukio la siku ya kuamkia Mei 29, 2022 la kuuwa kwa kupigwa risasi 7 Swalha huko Mwanza limeteka hisia za wengi nchini Tanzania

'mtu mpaka anakupiga risasi au mapanga, haianzi siku moja, haiwezekani , huwa kuna viashiria kwenye lugha ya kisheria tunaita 'process of normalisation' kwa maana ya mtu anaanza kukufanyia kitu kidogo kwanza kama kukutana, baadae anakusukuma kidogo, anakuja kukupiga kibao mpaka afikie hatua amekukata panga, inachukua hatua ndefu, kwa hivyo watu wanatakiwa kuondoa vitu hivi wanavyodhani vidogo, lakini vinatengeneza jambo kubwa', anasema Henga.

Tukio hili la Mwanza ni kama limeibua upya mjadala wa matukio ya mauaji yatokanayo na wivu wa kimapenzi nchini Tanzania.

Matukio ya kushtusha ya hivi karibuni ya mauaji ya kimapenzi Tanzania

Police

Chanzo cha picha, Eatv

Maelezo ya picha, Jumanne Murilo

Ukiacha tukio la Mei 29, huko Mwanza, mwezi Machi mwaka jana, aliyekuwa Kamanda wa Polis wa mkoa huo, Jumanne Muliro wakati anaeleza kukamatwa kwa watu wawili kutokana na mauaji yanayohusihwa kimapenzi yaliyotokea Kata ya Mkuyuni, alisema Polisi walikuta ujumbe unaosema 'mke wa mtu ni sumu'.

Tukio la Februari 24, 2022 huko Mwanga, Kilimanjaro lilihusisha wanaume wawili waliokuwa na uhusiano na mwanamke mmoja, kuamua kula njama na kumuua kwa sababu ya wivu wa kuwachanganya kimapenzi. Kabla ya kumuua kwa kumkatakata kwa mapanga walimbaka kwanza.

Januari 4, 2022, huko Nzega, Tabora, Mlinzi katika kiwanda Cha Machapati, Juma Mgunda,75, aliuawa kwa kupigwa shoka kichwani na mgongoni akiwa chumbani kwake.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Tabora, Richard Abwao alisema "Chanzo Cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi kwani mtuhumiwa (James) alimtuhumu marehemu na mganga wa kienyeji kumtorosha mkewe (Hadija Nyahindi) kwa muda wa mwezi mmoja Sasa"

Desemba 27, 2021 mwalimu wa Sekondari ya New Kiomboi mkoani Singida, Simon Roman (33) aliuawa kwa kuchomwa moto na mkewe baada ya kumtuhumu mumewe kuwa uhusiano na mwanamke mwingine.

Msiba

Chanzo cha picha, Muungwana

Maelezo ya picha, Vilio na misiba si utamaduni uliozoeleka, lakini ndugu wamekuwa wakilia kwa kuondokewa na wapendwa wao na ndugu zao kwa sababu mbalimbali ikiwemo wivu wa mapenzi

"Majibizano yalipoendelea, mwanamke alikwenda kuchukua maji ya moto yaliyochemshwa kwa ajili ya kuoga akamwagia mumewe wakiwa sebuleni na kabla hajajua la kufanya alimwagia tena mafuta ya petroli kisha akawasha moto wa kiberiti," alieleza Kamanda wa Polisi Mkoa Singida, Stella Mutabihirwa.

Oktoba 11, 2021 katika kitongoji cha Kanyabugulu mkoani Kagera, Emmanuel Mdende alimuua mkewe kwa kumkata panga nyumbani kwake akishuhudiwa na mtoto wake wa miaka 14, kwa kile alichodai mwanamke huyo alikuwa na mwanaume mwingine.

Mikoa ya Kagera, Kigoma, Mwanza na Dar es Salaam imekuwa ikiripoti matukio mengi ya aina hiyo.

Taarifa ya Utendaji ya Mahakama kanda ya Bukoka, Kagera iliyotolewa kwa Makatibu wakuu wa wizara za Katiba na sheria, Ofisi ya Rais Menejimenti ya utumishi wa Umma na utawala bora, Wizara ya Mambo ya ndani, afya, Maendeleo ya Jamii na Katibu mkuu wa Wizara ya ujenzi na Uchukuzi inaonyesha kuwa kati ya Januari - 15 Septemba, 2021, ilipokea mashauri ya mauaji 249, mengi yalihusu wivu wa kimapenzi na migogoro ya ardhi.

Kuua ni suala la kisaikolojia?

Sonona

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Upweke, Msongo wa mawazo na ugonjwa wa sonona kwa ujumla ni moja ya sababu inayodaiwa kupelekea mtu kuchukua uamuzi wa kuua ama kujiua

Kwa mujibu wa wanasaikolojia suala la mtu kumuua mtu mwingine ni 'suala la kisaikolojia kwa sababu linahusisha akili'.

Ni suala linaloanza na mtu, anayeamini kunufaika kihisia ama kwa mali ama kwa namna yoyote iwapo atamuua anayemlenga kumuua. Kwa upande wa Tanzania, Polisi imeendelea kuwakamata wanaohusika na mauaji hayo na kuwafikisha mahakamani. Ni jipu la kutumbuliwa, lakini linaloanza na mtu husika mwenyewe, anayepaswa kulitumbua kwa sababu ile ile ya 'kisaikolojia'.

'kuua ni uamuzi uliojengeka kwa muda, kutokana na mtu kukaa na vitu bila kuvitoa kwa muda mrefu, inawezekana ikawa ni mkusanyiko wa vitu vingi, ila kimoja kikachochea uamuzi huo', anasema Karoli Mabula, kutoka Counselling Tanzania Consulting.

Utafiti wa hivi karibu uliofanywa na Belinda Parker huko chuo Kikuu cha Queenslands nchini Australia unataja sababu 3 kubwa zinazosababisha mtu kuchukua uamuzi wa kumuua mwenza wake/mpenzi wake, mume au mke wake; Wivu, Tamaa ya mali na mapenzi.

Kwenye mapenzi ama upendo, utafiti huu unaonyesha kuwa, kisaikolojia muuaji hudhani ni bora kumuua mpenzi wake kuliko kuishi kwa maumivu ya mapenzi.

Namna gani ya kukabiliana na hisia za kuua?

SA

Chanzo cha picha, Getty Images

Mabula anasisitiza kuwa kwenye mahusiano ukiwa na uwezo wa kushughulika vyema na hisia za mwenzako, basi utakuwa na uwezo wa kudhibiti mambo yote na kuepusha mizozo inayoza hasira na chuki na kupelekea kufanya maamuzi ya kushangaza ikiwemo mauaji.

Ni 'migogoro katika maghusiano ni jambo la kawaida, ni lazima tujifunze, tukubali, kuzielewa, kuziheshimu na kuzifanyia kazi hisia za wapenzi wetu', anasema Mabula

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, anasema' kile kinachoonekana ni kidogo (kama kutukanwa na mwenza wako, kupigwa, kusukumwa, kunyanyaswa), shughulika navyo mapema, anapoanza kukudhuru kisaikolojia hapo hapo ukatae useme 'no' na kama anaendelea uchukue hatua nyingine za kisheria'.

Sheria katika mataifa yote duniani hairuhusu mtu kuua, uamuzi wa aina hiyo unakupeleka kwenye mikono ya sheria na kukabiliana na adhabu mbalimbali ikiwemo kifungo kirefu gerezani, wengine hata kupewa adhabu ya kunyongwa.

Ili kuepuka hilo Mabula anashauri 'haipaswi kufikia kuuana, muhimu wapenzi wanapaswa kutengeneza namna yao ya kuishi, wasiige wengine na jambo la pili mnanapaswa kukubaliana mlivyo na madhaifu yenu, na kukubaliana yale ambayo mnatofautiana, mpe uhuru mwenzio wa kuishi Maisha ayapendayo lakini mliyokubaliana, mtaepuka mengi', anamaliza.