Vita Ukraine: Vladimir Putin atoa wito kwa mataifa ya magharibi kumshinikiza Volodymyr Zelensky kusitisha vita

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema nchi za Magharibi zinaweza kusaidia kusitisha vita kwa kuweka shinikizo zaidi kwa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na kuacha usambazaji wa silaha kwa Kyiv.

Putin alitoa maoni hayo katika simu yake ya kwanza na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron takriban mwezi mmoja uliopita.

Kwa mujibu wa tovuti ya rais wa Urusi, Putin alisema kuwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zinapuuza "uhalifu wa kivita" unaoaminika kufanywa na vikosi vya Ukraine, akizishutumu kwa kulenga vitongoji vya makazi katika mkoa wa Donbass kwa mizinga.

Lakini vikosi vya Ukraine vinakanusha hili.

Macron alimwomba Putin kusitisha mapigano na kuruhusu raia zaidi kuondoka katika eneo la viwanda la Azovstal katika mji wa Mariupol nchini Ukraine.

Vikosi vya Urusi vilizidisha mashambulizi yao ya mabomu baada ya kundi la kwanza la raia kuhamishwa kutoka eneo hilo.

Macron alitangaza upya wito wake wa kusitisha mapigano nchini Ukraine, akionya juu ya "matokeo hatari ya uvamizi wa Urusi."

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Rais wa Ufaransa imeeleza kuwa Macron alionesha wasiwasi wake kuhusu hali ya Donbass na Mariupol, na kuitaka Urusi kuruhusu kuendelea kuondolewa kwa raia kutoka Azovstal.

Alitoa wito kwa Urusi kuwajibika, kama mwanachama wa Baraza la Usalama, kwa kukomesha "uchochezi mbaya".

Macron amekosolewa kwa kuweka mlango wazi wa mazungumzo na Kremlin na kwa kupiga simu na kuongea na Putin kwa muda mrefu, tangu kuanza kwa uvamizi.

Mwishoni mwa wiki, rais wa Ufaransa alizungumza kwa njia ya simu na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky.

Kwa upande mwingine, Waziri wa Ulinzi wa Slovakia Jaru Nad alisema kuwa Ulinzi wa Konstorkta, ambaye ni mtaalamu wa utengenezaji wa silaha, atasaidia kutengeneza na kuendeleza zana za kijeshi za Ukraine.

Waziri huyo alidokeza kuwa shehena ya kwanza ya vifaa hivyo ni pamoja na makumi ya magari ya kivita.

Slovakia hapo awali ilivipa vikosi vya Ukraine betri yake pekee ya ulinzi wa anga ya S-300.

Wachambuzi wanaamini kwamba kusaidia nchi jirani kutengeneza vifaa ni faida kubwa kwa vikosi vya Ukraine, kwa sababu vifaa vyao viko chini ya mabomu ya mara kwa mara ya makombora ya Urusi.

Unaweza pia kusoma