Mzozo wa Ukraine: Wanajeshi wa Uingereza wasiokuwepo huenda wapo Ukraine, Jeshi la Uingereza linasema

Baadhi ya wanajeshi wa Uingereza inawezekana wamekaidi amri na kusafiri hadi Ukraine kupigana, Jeshi la Uingereza limethibitisha.

Wanajeshi hao hawapo hapo bila likizo na huenda walienda Ukraine "kwa maamuzi yao binafsi", Jeshi lilisema.

"Tunawasisitiza sana warudi Uingereza," msemaji aliongeza.

Urusi yaishambulia Ukraine:Mengi zaidi

Wafanyakazi wote wamepigwa marufuku kusafiri hadi Ukraine hadi taarifa nyingine itakapotolewa.

Awali, Waziri wa mambo ya nje Liz Truss alisema anaunga mkono raia wa Uingereza ambao wanaweza kutaka kwenda Ukraine kusaidia kupigana, na kwamba ilikuwa juu ya watu kufanya maamuzi yao wenyewe.

Lakini serikali baadaye ilifafanua kuwa Ofisi ya Mambo ya Nje inatoa angalizo dhidi ya safari zote za kwenda Ukraine.

Wizara ya Ulinzi imesema kujiunga na mapigano huenda ni kinyume cha sheria na kunaweza kusababisha kufunguliwa mashtaka.

Taarifa ya Jeshi inafuatia ripoti katika gazeti la Sun kuhusu kijana mwenye umri wa miaka 19 kutoka kwa Walinzi wa Coldstream ambaye aliondoka kwenye kambi ya Windsor na kununua tiketi ya kwenda Poland ,mwishoni mwa wiki.

Wizara ya Ulinzi haijathibitisha ripoti hiyo lakini ilisema wanajeshi wanaosafiri kwenda Ukraine, wawe likizo wakati huo au la, watapewa adhabu za kinidhamu.

Wiki iliyopita wanajeshi walionywa kutokuelekea Ukraine kupambana na uvamizi wa Urusi pia kuna hatari ya kutoa "mtazamo potofu" kwa Urusi kwamba Uingereza ilituma wanajeshi kupigana.

Mamia ya wanajeshi wa zamani wa Uingereza wamesema wanataka kwenda Ukraine kupigana au kusaidia katika juhudi za matibabu au za kibinadamu. Wengi wameambia BBC kuwa wanapata taarifa zinazochanganya kutoka serikalini kuhusu iwapo wanafaa kwenda.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amewataka wageni kujiunga na kile anachokiita "jeshi la kimataifa". Haijulikani ni watu wangapi wameitikia wito wake, lakini mamia ya Waingereza walionesha nia yao ya kujitolea.

Licha ya kuwa Uingereza imetuma silaha kwa Ukraine ili kuisaidia kujilinda dhidi ya Urusi, mara kwa mara imesema haitatuma wanajeshi wa Uingereza kupigana nchini Ukraine.

Nchi za Magharibi zimekuwa wazi kwamba hazitahusika katika makabiliano ya kijeshi ya moja kwa moja na Urusi na nchi zilizo katika muungano wa kijeshi wa Nato - ikiwa ni pamoja na Uingereza - imekataa mara kwa mara wito wa Rais Zelensky wa kuweka eneo la kutoruka ndege katika anga ya Ukraine.