Virusi vya Corona: Kanisa Katoliki Tanzania latahadharisha juu ya wimbi jipya la corona

KANISA

Chanzo cha picha, ST.JOSEPH-INSTAGRAM

Kanisa Katoliki nchini Tanzania limetoa tahadhari juu ya wimbi jipya la maambukizi ya corona na kuwataka wananchi kuchukua hatua zote za kujikinga.

Tahadhari hiyo imetolewa kupitia waraka ulioandikwa na Rais wa Baraza la Maaskofu wa Katoliki Tanzania (TEC) Askofu Gervas Nyaisonga leo Jumanne.

Hata hivyo, waraka huo hausemi kuwa wimbi hilo jipya la maambukizi limeshaingia Tanzania na kutoa tahadhari kutokana na yanayoripotiwa kwingineko.

"Nchi kadhaa zimethibitisha kuwa zinapitia katika kipindi kigumu cha kuenea kwa Korona na kutokea vifo vya watu. Nchi yetu sio kisiwa, hatuna budi kuzingatia hekima ya wahenga kuwa: 'mwenzio akinyolewa wewe tia maji,'…" imeeleza sehemu ya waraka huo.

Kanisa Katoliki nchini humo limekuwa likichukua hatua kadhaa kutoka mwaka 2020 mara tu mlipuko wa corona ulipothibitishwa kuingia Tanzania, na waraka unataka hatua hizo ziendelee kuchukuliwa.

Maelezo ya sauti, Kanisa Katoliki Tanzania latahadharisha juu ya wimbi jipya la corona

"Tuhimize mapambano dhidi ya virusi vya korona kwa kutumia silaha zote za kiroho, kimwili, kisayansi na kijamii. Tusikome kuhimiza sala, kuepuka kugusana, kunawa na kujitakasa kila wakati, kuchukua hatua tuonapo dalili za ugonjwa na kuepuka misongamano hatarishi," umesisitiza waraka.

Wiki iliyopita, serikali ya Uingereza ilitangaza kuziongeza nchi za Tanzania na Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) katika marufuku ya wasafiri kutoka nchi hizo katika juhudi za kukabiliana na ya wimbi jipya la virusi hivyo ambavyo vinatambulika kama aina ya Afrika Kusini.

Nchi nyingine 12 za kusini mwa Afrika tayari zilishapigwa na marufuku hiyo baina ya Disemba na mwanzoni mwa Januari.

Hata hivyo, serikali ya Uingereza haikuweka wazi vigezo ilivyovitumia kuijumuisha Tanzania ambayo mpaka sasa haijathibitisha uwepo wa aina hiyo mpya ya virusi. Msimamo wa serikali ya Tanzania ni kuwa hakuna virusi vya corona nchini humo.