Matamshi ya Mesut Ozil: China yafutilia mbali mechi kati ya Arsenal na ManCity

Mesut Ozil

Chanzo cha picha, Huw Evans picture agency

Maelezo ya picha, Ozil, aliyekuwa mchezaji wa Ujerumani amekuwa Arsenal tangu mwaka 2013

Shirika la habari nchini China CCTV limefutilia mbali mechi ya Jumapili kati ya Arsenal na ManCity kufuatia matamshi ya kiungo wa kati wa Arsenal Mesut Ozil , chombo cha habari cha serikali kimesema.

Ozil alichapisha katika mitandao ya kijamii kuhusu jinsi Waislamu wa Uighurs wanavyoteswa nchini China.

Arsenal ilijitenga kutokana na matamshi ya raia huyo wa Ujerumani ikisema kuwa shirika haliingilii maswala ya kisiasa.

''Arsenal haipendi kujihusisha katika maswala ya kisiasa kama shirika'', ilisema klabu hiyo ya London.

''Kufuatia ujumbe katika mitandao ya kijamii kutoka kwa Mesut Ozil, klabu ya Arsenal lazima iweke wazi kwamba hayo ni maoni ya kibinafsi ya Mesut''.

Taarifa hiyo ya Gunners ilichapishwa katika mtandao wa Weibo nchini China.

Gazeti la The GLobal Times lilitaja matamshi ya Ozil kuwa ya 'kusikitisha'.

Na kuongezea Shirika la soka nchini China lilisema kwamba matamshi ya Ozil 'hayakubaliki' na yameumiza hisia za wafuasi wengi wa China.

CCTV sasa itaonyesha mechi kati ya Tottenham dhidi ya Wolves , badala ya ile ya moja kwa moja kati ya Arsenal dhidi ya mabingwa hao wa ligi.

Makundi ya haki za kibinadamu yanasema kwamba karibia watu milioni moja wengi wao kutoka kwa jamii ya Uighur walio Waislamu wanadaiwa kuzuiliwa bila kufunguliwa mshtaka katika kambi moja ya jela.

China inasema kwamba Waislamu hao wanapatiwa mafunzo katika kambi ili kukabiliana na ghasia na itikadi kali za kidini.

Katika chapisho lake Ozil ambaye ni Muislamu aliwaita Uighurs ''mashujaa ambao wanapinga mateso'' na kuikosoa China pamoja na idadi kubwa ya Waislamu waliolifumbia macho jambo hilo.

China mara kwa mara imepinga kwamba inawatesa Waislamu wa jamii ya Uighurs katika taifa hilo.

Taarifa hiyo ya Arsenal ilipokea maoni mengi, wengi wakikosoa ama kusema kwamba sio vyema. Mtu mmoja aliandika ''ni hilo tu''? huku mwengine akijibu na tisheti ya Ozil ambayo imekatwa.

Watumizi wengine pia waliandika machapisho yaliokua na alama ya reli "#Protesting against Ozil" na "#Ozil alitoa matamshi machafu dhidi ya China".

Mwezi Oktoba , Shirika la mpira wa vikapu nchini Marekani lilikumbwa na hasara kubwa ya kifedha baada ya tamko la mtandaoni kutoka kwa afisa mmoja mwandamizi katika timu hiyo.

Meneja wa klabu ya Houston Rocket Daryl Morey alituma ujumbe wa Twitter akiunga mkono waandamanaji wanaounga mkono demokrasia Hong Kong.

Kutokana na hatua hiyo kampuni za China zilisitisha ufadhili wao na ule wa runinga kwa timu hiyo.