Wayne Rooney akamatwa akiwa amelewa Marekani kutokana na dawa na pombe

Wayne Rooney alikamatwa baada ya kupatikana akiwa amelewa na "kukanganyikiwa" baada ya kunywa dawa za kupa usingizi na pombe kwa pamoja, msemaji wake amesema.

Mchezaji huyo wa zamani wa England alifanya hivyo akiwa safarini kwenye ndege.

Nahodha huyo wa zamani wa Manchester United alikamatwa 16 Desemba katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dulles jimbo la Virginia akirejea kutoka safari ya siku moja nchini Saudi Arabia.

Rooney, 33, alishtakiwa na akalipa faini ya $25 na gharama ya kesi ya $91 mnamo 4 Januari kwa mujibu wa nyaraka za mahakama kutoka Mahakama ya Hakimu ya Wilaya ya Loudoun.

Taarifa ya msemaji wa mchezaji huyo imesema : "Akiwa safarini kwenye ndege Wayne alimeza tembe alizokuwa ameagizwa na daktari kuzinywa na akachanganya na pombe jambo ambalo lilimfanya kuchanganyikiwa alipowasili uwanja wa ndege.

"Polisi alimpata katika hali hiyo na akamkamata kwa kosa dogo la uvunjifu wa amani.

"Alipokezwa faini ya moja kwa moja ya kawaida na akaachiliwa huru muda mfupi baadaye katika uwanja huo wa ndege. Kisa hicho sasa kimehitimishwa.

"Wayne angependa shukrani zake kwa jinsi kisa hiki kilishughulikiwa na wahusika wote zipokelewe."

Rooney, anayechezea klabu ya DC United inayocheza Ligi Kuu ya Marekani na Canada alishtakiwa kosa la ngazi ya 4 ambazo adhabu yake ya juu zaidi ni faini ya $250.

Rooney alikuwa amepigwa marufuku kutoendesha magari kwa miaka miwili Septemba 2017 baada yake kukiri kwamba alikuwa ameendesha gari akiwa mlevi eneo la Cheshire, Uingereza.

Mshambuliaji huyo alihamia Marekani Juni 2018 baada ya kutia saini mkataba wa miaka mitatu na nusu na DC United.

Rooney aliongoza klabu hiyo kufika hatua ya mechi ya muondoano wa baada ya msimu msimu punde baada ya kujiunga nao, ambapo walishindwa mechi yao ya kwanza, mchezaji huyo wa zamani wa Everton akipoteza mkwaju wa penalti dhidi ya Columbus Crew.

Taarifa kutoka DC United imesema: "Tunafahamu kuhusu taarifa zinazodokeza kwamba Wayne Rooney alikamatwa Desemba.

"Tunafahamu hamu ya vyombo vya habari kutaka kujua zaidi kuhusu suala hili lakini tunaamini hili ni suala la faragha kwa Wayne ambalo DC United italishughulikia kwa mifumo ya ndani. Hatuna jambo jingine la kusema kuhusu hili."