EPL : Liverpool na ManCity zashinda, Man United yazuiwa

Liverpool yapanda katika kilele cha jedwali

Chanzo cha picha, Getty Images

Liverpool imejipatia uongozi katika jedwali la ligi ya Uingereza kufikia sasa kwa kuilaza Southampton katika uwanja wa Anfield katika ushindi wa saba mfululizo katika mashindano yote.

Wenyeji walichukua uongozi baada ya dakika 10 kufuatia krosi ya Xhedan Shaqiri iliomgonga beki West Hoedt kwa bao la kujifunga mwenyewe.

Joel Matip baadaye aliruka na kufunga krosi iliopigwa na Trent Alaxander Anold na kufanya mambo kuwa mbili bila.

Liverpool ilijihakikishia uongozi huo pale Mo Salah alipofunga baada ya mpira wa adhabu uliopigwa na Shaqiri kugonga mwamba wa goli na kurudi uwanjani.

Man United yazuiwa

Chanzo cha picha, Getty Images

Kwengineko shambulio kali la Joao Moutinho liliipatia Wolves sare uwanjani Old Trafford huku wageni hao waliopandishwa daraja wakiendelea na mwanzo mzuri katika ligi ya Uingereza.

Kiungo huyo wa kati wa Ureno alipata mpira karibu na lango la de Gea kabla ya kufunga mkwaju huo.

Wolves walionyesha mchezo mzuri katika kipindi cha kwanza na ilikuwa bahati mbaya kujipata nyuma baada ya mchezaji wa Brazil Fred kuifungia Man United kufuatia pasi nzuri ya Pogba.

Sergio Aguero

Chanzo cha picha, Getty Images

Manchester City iliinyorosha Cardiff City 5-0 na kupanda hadi nafasi ya pili katika jedwali la ligi ya Uingereza.

Wageni hao walikuwa mbele baada ya kipindi cha kwanza kwa kufunga magoli 3 ya haraka kupitia Sergio Aguero, Bernado Silva na Iikay Gundogan.

City ilijihakikishia ushindi huo katika kipindi cha pili baada ya raia wa Algeria Riyad Mahrez kufunga bao lake la kwanza na la nne kwa jumla na baadaye kuongeza la tano .