Wasifu wa mhubiri wa Kishia aliyeuawa Saudia

Chanzo cha picha, AFP
Sheikh Nimr al-Nimr, aliyenyongwa na serikali ya Saudi Arabia, alikuwa kiongozi wa kidini wa dhehebu la Washia walio wachache nchini humo.
Alikamatwa mwaka 2012, mwaka mmoja baada ya maandamano ya kupinga serikali kuzuka mkoa wa Mashariki wenye Washia wengi.
Maandamano hayo yalizuka wakati wa wimbi la mageuzi lililovuma mataifa ya Kiarabu na kuangusha serikali nyingi mwaka 2011.
Amekuwa na wafuasi wengi sana miongoni mwa vijana wa Kishia nchini Saudi Arabia, na pia nchini Bahrain.
Alikuwa akikosoa sana familia za kifalme za Kisuni zinazoongoza nchini Saudi Arabia na nchini Bahrain.
Alizaliwa mwaka 1959 au 1960 katika kijiji kimoja wilaya ya Qatif, Mkoa wa Mashariki.
Sheikh Nimr al-Nimr alisomea nchini Iran na Syria kwa miaka mingi.
Alirejea Saudi Arabia 1994 na kampeni yake ya kutetea uhuru wa kuabudu ilimfanya kuanza kuangaziwa na maafisa wa usalama wa Saudia.
Mhubiri huyu alikamatwa na kuzuiliwa kwa muda mfupi mara mbili kabla ya kukamatwa tena 2012, mwaka 2004 na 2006, kwa mujibu wa Al-Jazeera.
Nimr al-Nimr alikuwa akiendelea kupata umaarufu.
- <link type="page"><caption> Mhubiri wa Kishia anyongwa Saudi Arabia</caption><url href="http://www.bbc.com/swahili/habari/2016/01/160102_shia_cleric_executed_saudia" platform="highweb"/></link>
- <paragraph><link type="page"><caption> Iran: ‘Kisasi cha Mungu’ kitakumba Saudia</caption><url href="http://www.bbc.com/swahili/habari/2016/01/160103_iran_saudi_revenge.shtml" platform="highweb"/></link></paragraph>
Anaripotiwa kukutana na maafisa wa Marekani mwaka 2008, kwa mujibu wa ufichuzi wa Wikileaks, lengo la mkutano huo likiwa kujitenganisha na taarifa za kupinga Marekani na kuunga mkono Iran.

Chanzo cha picha, AFP
Wakati wa kukamatwa kwake 2012, alipigwa risasi mguuni mara nne baada ya kukimbizwa na maafisa wa usalama akiwa kwenye gari lake.
Watu watatu waliuawa kwenye maandamano yaliyotokea baada ya kukamatwa kwake.
Shirika la Amnesty International lilishutumu kukamatwa kwa Nimr na kusema ilikuwa sehemu ya juhudi za serikali ya Saudi Arabia kukandamiza wapinzani.
Mke wake Muna Jabir al-Shariyavi, alifariki akitibiwa New York mwaka 2012.
Kesi dhidi yake ilianza Machi 2013, na viongozi wa mashtaka walitaka ahukumiwe kuuawa kwa “kusulubiwa”, hukumu ambayo hushirikisha mtu kukatwa kichwa na kisha mwili wake kuonyeshwa hadharani kwa umma.
Alipatikana na hatia ya kutafuta watu wa nje wa kuingilia masuala katika ufalme huo, kutotii watawala na kuchukua silaha kukabiliana na maafisa wa usalama.
Hukumu ya kifo dhidi yake ilithibitishwa Oktoba mwaka 2014.












