Mandamano Tanzania: Maswali 9 magumu kwa Tume ya Oktoba 29

Chanzo cha picha, UN
Mwenyekiti wa Tume huru ya uchunguzi iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuchunguza matukio ya Oktoba 29, Jaji Othman Chande, amesema tume yake itafanya uchunguzi wa kina na wa wazi, huku ikiomba ushirikiano kutoka kwa makundi yote yanayohusika moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja na matukio hayo.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika mkutano na wahariri wa vyombo vya habari, Jaji Chande alisema tume hiyo yenye wajumbe tisa imeanza rasmi kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria kwa siku 90 ilizopewa kukamilisha uchunguzi.
"Tume hii ina mamlaka ya kutoa wito kama Mahakama kuu inavyotoa wito… tunaomba ushirikiano," alisema, akisisitiza kuwa kundi lolote litakalotakiwa kutoa taarifa litaitwa bila upendeleo.
Kwa mujibu wa hadidu za rejea, tume inatakiwa kuchunguza: Chanzo na mazingira ya matukio kabla, wakati na baada ya uchaguzi, malengo ya waliopanga au kushiriki vitendo hivyo, madhara yaliyotokea yakiwemo vifo, majeruhi na uharibifu wa mali;, hatua zilizochukuliwa na Serikali na vyombo vya usalama, maeneo yanayohitaji kuimarishwa katika utawala bora, maridhiano na haki za binadamu na masuala yoyote mengine ambayo tume itaona yana umuhimu.
Jaji Chande alisema uchunguzi utafanyika zaidi katika maeneo yaliyoathirika na ghasia Tanzania Bara, lakini pia tume itakusanya ushahidi kutoka maeneo ambayo hakukuwa na matukio ili "kuelewa tofauti za mazingira na sababu."
"Tujifunze kwa nini hapa imetokea, na hapa haijatokea," alisema.
Mbinu za kukusanya ukweli uliotokea
Tume imesema itatumia nyaraka, mahojiano ya ana kwa ana na mtandaoni, barua pepe, dodoso za mtandaoni, ushahidi wa maandishi na ziara za moja kwa moja katika maeneo husika. Wadau watakaoshirikishwa ni pamoja na waathirika, watuhumiwa, vyama vya siasa, asasi za kiraia, viongozi wa dini, wafanyabiashara, vyombo vya ulinzi na usalama, wanafunzi, vijana, waandishi wa habari na wataalamu wa sekta mbalimbali.
"Ni imani yetu kuwa kwa njia hizi tutaweza kupata taarifa pana na za kina," alisema Chande.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Aliongeza kuwa tume haina mamlaka ya kijinai hivyo haitashtaki mtu, bali itatoa mapendekezo na tathmini ya kina kuhusu kilichotokea na kinachopaswa kufanyika.
Lakini baada ya mazungumzo yake, aliulizwa maswali magumu kadhaa na waandishi wa habari. Wahariri walihoji pamoja na mengine masuala tisa ambayo yamekuwa yakizungumzwa kwa upana katika mjadala wa umma, na Jaji Chande alitoa ufafanuzi katika maeneo mbalimbali.
1. Je, uchunguzi wa matukio ya siku tatu pekee kuanzia Oktoba 29, 2025 hautaacha chanzo halisi kilichoanzia muda mrefu kabla?
Chande alisema ingawa matukio makuu yalitokea ndani ya siku tatu, uchunguzi utafika "nyuma sana" ili kubaini chanzo na mienendo iliyopelekea matatizo hayo.
2. Vyama vya siasa na wanaharakati ambao hawana imani na tume watawezaje kushirikiana nayo?
Alisema tume itatafuta ushirikiano bila kushurutisha, akibainisha kuwa kutokuamini ni jambo la kawaida katika tume za aina hii. "Hata anayekataa tutamwomba. Tutamwomba hata mara tatu," alisema.
3. Kutokuwepo kwa vijana kwenye tume ilhali wao ndio walikuwa kundi kubwa kwenye matukio kunashughulikiwaje?
Alisema vijana watashirikishwa kwa upana kupitia mahojiano, mijadala na vikundi maalum, na kwamba tume itatumia mbinu mbalimbali kuwafikia "waliosoma na wasiosoma, wenye ajira na wasio na ajira."
4. Je, kauli za viongozi kwamba baadhi ya waandamanaji 'walilipwa' hazitoa mwelekeo wa mapema kuhusu kilichotokea?
Chande alisema Tume inaanza 'zero' hatua ya kwanza kukusanya majibu. "Hatuna ushahidi hata kidogo. Tutapima ushahidi, tutapima nyaraka," akiongeza kuwa tume haitafuata hisia bali uthibitisho.
5. Kwa siku 90 na maeneo mengi, tume itafaniki majukumu yake vipi?
Amekiri kuwa muda ni mfupi, lakini akasema: "Tunaomba mtupime baada ya kazi, si kabla ya mtihani."
6. Wito kwa mjumbe Stergomena Lawrence Tax aliyekuwa waziri wa ulinzi na vyombo alivyosimamiwa vilishiriki wakati wa matukio je, hakuna mgongano wa maslahi?
Alisema kamati nyingi za Jumuiya ya Madola huwa zinaundwa kwa utaratibu fulani ambao rais ana mamlaka hayo, na ikiwa maslahi yataonekana, "mjumbe anaweza kuomba kujitoa au tume inaweza kumwomba ajitoe."
7. Tume itachukuliaje taarifa za maandamano mengine yanayodaiwa kuandaliwa Disemba 9?
Amesema tume inachunguza matukio ya Oktoba 29 na siku chache baada yake, lakini inaweza kuangalia yaliyotokea kabla au baada "kama kuna uhusiano wa moja kwa moja."
Swali la 8 lililohusu itakuwaje kama uchunguzi utaonesha kuwahusu viongozi walioteua tume yenyewe? na Kauli kama 'watakinukisha' iliyo kwenye kesi mahakamani inayomuhusu kiongozi wa upinzani, Tundu Lisu, Tume itafanyaje
Maswali haya hayakujibiwa moja kwa moja na Mwenyekiti.














