Matokeo ya Uchaguzi Kenya: Je, kuchaguliwa kwa William Ruto kuwa rais kunamaanisha nini?

    • Author, Dr. Alutalala Mukhwana
    • Nafasi, Mchambuzi

Jumatatu, tarehe 15-8-2022, William Samoei Ruto alitangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais nchini Kenya baada ya kupata zaidi ya kura milioni saba.

Tofauti kati ya zile kura alizozipata Rais huyo Mteule na zile alizozipata mpinzani wake wa karibu na Waziri mkuu wa zamani wa Kenya Raila Odinga ilikuwa 233,211.

Kwa vigezo vingi, ushindi wake William Ruto unaashiria mapinduzi makubwa ya kijamii kwa misingi kwamba yeye kapigana na kushinda vizuizi vya kijamii vilivyojengwa kuanzia Kenya inyakue uhuru mwaka wa 1963.

Viongozi wa kiafrika waliotwikwa uongozi wa Jamuhuri mpya ya Kenya mwaka huo, wakiwemo Rais wa kwanza, Jomo Kenyatta(babake Rais Uhuru Kenyatta anayeondoka madarakani) na Makamu Rais wa kwanza, Jaramogi Oginga Odinga (babake Raila Odinga na mpinzani wake Ruto katika uchaguzi huo wa Jumanne iliyopita) waliweka misingi kwamba uongozi ulisalia katika mikono ya wachache walio karibiana nao.

Mwaka wa 1978, Makamu wake Kenyatta, Rais wa pili wa Kenya, Daniel Arap Moi naye alichukuwa mamlaka licha ya kwamba waandani wa karibu wake Kenyatta walio kuwa wa kabila lake Kenyatta (Wakikuyu) walimpangia njama kubwa asispate.

Lakini Moi naye aliendeleza misingi iyo hiyo, kwa kufuata nyayo zake Kenyatta. Akafanya jamii za wanasiasa wakongwe kuweka mizizi ya dhati katika nyanja zote za kitaifa zikiwemo nyanja za kiuchumi na kisiasa.

Hivyo basi, William Ruto, kwa ushindi wake huo, amevunjilia mbili misingi hiyo ya kudhibiti mali na uongozi kusalia katika mikono ya vizazi vya waanzilishi wa taifa na ametwaa uongozi kwa ari, bidii na ukakamavu wa mwana wa maskini na asiyetarajiwa kukwea ngazi ya jamii na uongozi hadi kuchaguliwa Rais wa Jamuhuri ya Kenya.

Ushindi wa Ruto unamaanisha nini

Ushindi huu umedhihirisha kwamba inawezekana mkenya ye yote kufaulu katika azma na ndoto zake ziwazo zile, bora mazingira mwafaka yawepo. Inawezekana kina yahe kunawiri Kenya!.

Katika kampeni zake William Ruto, alidai kuwaakilisha raia maskini almaarufu "hustlers" ambao, alidai,walipuuzwa na serikali za awali kwa misingi kwamba wao maskini hawakuwa na lao katika nchi ya Kenya. Hivyo basi, ushindi wake William Ruto unaashiria mchipuko wa uongozi mpya kabisa nchini Kenya, uongozi unaowapa wana walio zawa katika jamii na wazazi maskini uwezekano wa kukwea ngazi ya kisiasa hadi upeoni kuwa Rais wa Jamuhuri.

Ushindi huu waashiria kwamba inawezekana raia wa hali ya chini kufaulu maishani chini ya serikali yake "mwana hustler" na hili litawapa matumaini na matarajio mapya halaiki ya Wakenya wa kawaida.

Katika kampeni zake William Ruto, alidai kwamba zaidi ya Wakenya, haswa vijana, milioni 15 walikwisha fungiwa kupata mikopo ya aina yoyote kutoka kwenye benki za Kenya kwa vile wameripotiwa katika "Credit Reference Bureau" almaarufu "CRB" baada ya kukopa na kushindwa kulipa mikopo fulani, hususan mkopo unaopeanwa kupitia njia ya simu na uitwao "fuliza". Aliwaahidi kufutilia mbali hizo ripoti za CRB ili kuwapa fursa mpya maishani.

Kigezo kingine cha kihistoria ni kwamba kabla na wakati wote wa kampeni, Dr. Ruto amerushiwa lawama za ufisadi kwa fujo kubwa. Alidaiwa kutia mkono wake katika jungu la fedha za umma na kwamba kwayo, asiwe ni mwenye kuaminiwa hadi kutunukiwa Urais.

Kwa kushinda uchaguzi huu, kunaashiriwa kwamba swala la ufisadi si hoja kuu katika uchaguzi wa Kenya, kwani lingalikuwa hoja kuu, raia wasingelimtunuku na fahari hii ya urais kinyume na njama na matakwa ya wapinzani wake.

Kadhalika, ushindi huu unaashiria kwamba madai hayo ya Rais anayeondoka na waandani wake dhidi yake Ruto kwamba yeye Ruto ni mfisadi na mlaji rushwa, labda, hayakuwa na msingi wowote katika mboni na macho ya mamilioni ya Wakenya ambao wamekwisha mchagua William Ruto kuwa Rais wa tano wa Kenya. Isitoshe, hata kama madai yao yalikuwa na msingi wowote, wao, waandani wao na hata jamii zao pia hawakusazwa kwa madai yayo hayo.

Kwa jumla, matarajio ya raia walio mchagua yatakuwa kwamba mifumo mizima ya serikali mpya yake "Hustler" italenga kina yahe kwa kuwainua wale wote ambao hali zao, chini ya serikali inayoondoka, zilikuwa si hali tena.

Ushindi wa Ruto unamaanisha nini kimataifa

Kimataifa, mtazamo utakuwa ni wa ngoja ngoja. Hii ni kwa sababu William Ruto, pamoja na Rais Kenyatta waliwahi kushtakiwa katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa jinai ICC nchini Uholanzi kwa madai ya uhalifu dhidi ya binadamu mauaji mwaka wa 2007-2008 katika ghasia zilizozuka baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.

Ingawa mashtaka hayo yalifutiliwa mbali kwa kukosa ushahidi, hivi majuzi Wakili Paul Gacheru, aliyekuwa mwandani wake William Ruto, amejisalimisha Uholanzi katika korti jinai ya Kimataifa(ICC). Duru zisizoaminika zilidai kwamba ushahidi mpya umeanza kujitokeza, nao ushahidi huo ukashukiwa kumlenga Dr. Ruto. Hivyo basi, wingu hilo la tuhuma lingaliko na jamii ya kimataifa itakuwa ni yenye kufuatilia uongozi mpya wa Bw Ruto kwa karibu sana.

Kadhalika, uongozi wake Ruto utaangaliwa kwa macho ya karibu mno na waekezaji na mabwenyenye wa Kenya, zikiwemo jamii kongwe za wanasiasa wa zamani wa Kenya kwa sababu rais huyo mteule huenda akaanzisha mifumo ya kuwasaidia maskini na pengine, bila kukusudia, akawatelekeza na kuwaadhiri matajiri.

Lakini je, ni nini kilichosababisha wapiga kura wapige kura namna walivyopiga?

Kwa mtazamo wangu, sababu zao zilikuwa zenye mchanganyiko. Kwa mfano, wanaotoka katika jamii ya Wakikuyu, anamotoka Uhuru Kenyatta, walimchagua William Ruto kwa sababu walitaka kuasi dhidi ya Uhuru Kenyatta na kumfunza somo kwamba wao ndio wenye uwezo wa kumchagua wampendaye. Kwa ajili hiyo na kwa mara ya kwanza katika historia ya chaguzi za Kenya, Agikuyu walimkataa mmoja wao.

Vile vile na kwa sababu iyo hiyo, kwa mara ya kwanza tangu Kenya ijinyakulie uhuru mwaka wa 1963, Wakikuyu walimchagua kiongozi kutoka kabila tofauti. Isitoshe, mwaka wa 2007-2008, waliyemchagua huyo, aliyedaiwa na mahasidi wake, kuhusika katika visa vya kuwadhulumu Wakikuyu wanaoishi mkoa wa Rift Valley na jamii hizo mbili kihistoria, si marafiki wa haja.

Jamii hii yake Rais anayeondoka imekuwa ikisikika, japo kupitia fununu tu, ikidai kwamba biashara zao zilizoroteka pakubwa wakati wa utawala wake Uhuru Kenyatta. Imedai kuwa Rais anayeondoka hakutimiza maendeleo ambayo aliwaahidi kutekeleza walipompigia kura mara mbili mtawalia (2013-2017 na 2017-2022). Isitoshe, akitafuta kura zao, aliwaomba wampe nafasi aongoze kwa miaka kumi kisha amuachie suhuba wake wakati huo, William Ruto, naye akaongoze kwa miaka mingine kumi.

Kukawaaje sasa anampiga kumbo mwaandani wake huyu (Ruto)? Je, mbona hakuwaambia hadharani sababu za kumtema Ruto? Basi haya yote yaliwakosesha Wakikuyu imani kwake mwana wa Jomo, wakampiga kumbo alivyompiga Ruto kumbo.

Kwa njia h iyo hiyo, kwa sababu hizo hizo, wakamkataa Raila Odinga kwa kuwa ndiye aliyechangia masaibu yake William Ruto. Walimuona Ruto kama aliyefanywa kafara ili mwana wa Jomo amridhie uongozi mwana wa Jaramogi kwa misingi kwamba baba zao walikuwa wenye ukuruba na walijiona wenye haki ya kutawala Kenya milele pasiwe na nafasi kwa "mwana wa nje". Kama alivyowabatiza William Ruto, wawili hawa walikuwa wategemea urathi ("dynasty") kutawala Wakenya.

Yote tisa, la kumi ni kwamba Ruto alifaulu kuwagawanya Wakikuyu kwa misingi ya wale wana wa Mau Mau na wale wana wa waliokuwa waliinzi wa Mkoloni almaarufu "Homeguards". Kihistoria, inadaiwa, japo kwa fununu tu, kwamba baada ya Mkoloni kugura Kenya, wengi wa wana wa wapiganiaji huru wa (Mau Mau) walisalia maskini huku uongozi na mali za taifa zikinyakuliwa na waliokuwa waliinzi na washirika wa Mkoloni, kwa jina la chukizo "Wabeberu weusi". Hivyo, Uhuru Kenyatta amekataliwa na kutemwa kwa misingi hiyo naye William Ruto kakubaliwa na kutunukiwa kwa misingi hiyo hiyo.

Kwa upande wa kabila lake William Ruto, walimpigia yeye Ruto kwa wingi sana kwa ajili ya kuwa mmoja wao, sawia na Wajaluo walivyompigia Raila Odinga kwa wingi kwa misingi hiyo hiyo.

Aidha, wengine waliompigia Raila Odinga walifanya hivyo kwa misingi ya ubabe wa makabila k.m mkoa wa magharibi ulifuata ukuruba wao wa miaka mingi na chama chake cha ODM. Aidha, jamii ya Wakamba ilimpigia Raila kura kwa kushinikizwa na kuraiwa na mbabe wao wenyewe, Mheshimiwa Kalonzo Musyoka. Vivyo hivyo, kupitia urai wake Ali Hassan Joho, Gavana anayeondoka Mombasa, Raila alipigiwa kura, n.k..

Kwa ujumla, kura zilipigwa kwa misingi ya vyama, makabila na sera za wawaniaji. Miaka ijayo mitano yake William Samoei Ruto itakuwa ni yenye kusubiriwa kwa matamanio makubwa na wafuasi wake.

Mwisho, Chembilecho Wahenga, Mgalla muue, lakini haki yake mpe -William Ruto yuastahili kongole maradufu kwa kibarua alichokichangamkia kwa udi na uvumba hadi kuchaguliwa Rais wa tano wa Jamuhuri ya Kenya.

Pia unaweza pia kusoma