Matokeo ya uchaguzi Kenya 2022: Jinsi makabidhiano ya uongozi yanavyofanyika Kenya

Kenya inajitayarisha kuukaribisha utawala mpya wa serikali baada ya matunda ya mshindi wa moja kwa moja katika duru ya kwanza ya upigaji kura .

Mojawapo ya taratibu muhimu sana na ambazo zilianza mapema pindi tu matayarisho ya uchaguzi yalipokamilishwa.

Utaratibu huo umelindwa na katiba na una miongozo ya kimsingi ili kuufanikisha ni makabidhiano ya uongozi kutoka kwa rais mmoja hadi mwingine.Rais Uhuru Kenyatta ambaye amemaliza kipindi chake cha mihula miwili ya miaka 10 atakuwa akimkabidhi hatamu mrithi wake.

Kwa mujibu wa Sheria ya Makabidhiano ya Ofisi ya Rais, Serikali iliyopo madarakani inafaa kuunda kamati ijulikanayo kwa jina la Kamati ya kukabidhi madaraka ya Ofisi ya Rais ili kuendesha mchakato huo angalau siku 30 kabla ya Uchaguzi Mkuu.

Rais kenyatta tayari alishaitangaza kamati hiyo ambayo itasimamia mchakato mzima wa serikali yake kuipa madaraka serikali ijayo .

Lakini mchakato huu unahusisha nini na akina nani?

Rais anayeondoka kupoteza mamlaka

Rais Uhuru Kenyatta alipoteza mamlaka kadhaa mnamo Agosti 9, wakati Wakenya walipoanza kupiga kura kuchagua viongozi wapya .

Rais siku hiyo aliingia kwenye awamu ya "Uongozi wa muda" maana yake atakuwa ameshikilia kiti kama kiongozi wa muda akijiandaa kumkabidhi Mkuu wa nchi ajaye.

Katiba inamnyima mamlaka fulani katika awamu hii.

Sura ya Tisa (9), Sehemu ya Pili (2), Ibara ya 134 ya Katiba ya Utekelezaji wa Madaraka ya Urais Wakati wa Uongozi wa Muda inasema Mkuu wa Nchi anayemaliza muda wake anapoteza mamlaka ya kuteua majaji wa Mahakama za Juu.

Wakati huo huo, rais anapoteza mamlaka ya kuteua afisa yeyote wa umma; kuteua au kumfukuza kazi waziri (CS), Katibu wa kudumu (PS) na maafisa wengine wa Serikali.

Pia anasalimisha mamlaka ya kuteua, kuchagua au kutengua kamishna mkuu, balozi, au mwakilishi wa kidiplomasia au ubalozi.

Rais pia amenyimwa uwezo wa kutumia nguvu ya huruma, maana yake hawezi kuwasamehe wafungwa.

Kenyatta pia ataacha mamlaka ya kutoa heshima kwa jina la wananchi na Jamhuri.

Kipindi cha "uongozi wa muda" huanza siku ambayo Wakenya watapiga kura na kinaisha wakati rais mpya aliyechaguliwa anaanza kutekeleza majukumunyake.

Maandalizi ya kuapishwa kwa rais mteule

Siku ya kuapishwa, msafara wa rais utakuwa umesimama katika makao ya rais mteule na naibu wake na watalindwa vikali na kikosi cha maafisa wa Kitengo cha (GSU) ambao watawaongoza kwenye hafla ya kuapishwa.

Msafara wa rais ambao utakuwa na idadi sawa ya magari na yale ya kawaida ya rais anayeondoka, utaelekea kwenye eneo la kuapishwa ambalo huenda likawekwa katika uwanja wa kitaifa ama ukumbi wowote utakaotangazwa kutumiwa na kamati ya makabidhiano .Rais Uhuru Kenyatta aliapishwa katika uwanja wa Kasarani.

Rais Mteule anatarajiwa kuapishwa Jumanne ya kwanza kufuatia siku ya kumi na nne baada ya tarehe ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais, ikiwa hakuna ombi lililowasilishwa kortini kupinga matokeo hayo, atapewa haki zote za urais anazopata mtangulizi wake hata kabla ya kula kiapo.

Wakati akielekea kwenye uwanja vya kuapishwa, rais ajaye atafahamishwa kuhusu vipengele vya serikali kama vile miundo ya serikali, taarifa za ujasusi, hali ya uchumi na maelezo kamili ya mchakato wa kuapishwa.

Kabla ya hafla hiyo, kamati ya maandalizi itatuma bendera ya rais kwa Kamati ya Sare za nchi ili kufanyiwa muundo. Bendera hiyo maalum ya rais itatengezwa kumpendeza rais mteule.

Majina ya wageni na viongozi wote watakaohudhuria hafla hiyo pia yatatumwa kwa kamati ya uongozi na rais mteule na Mkuu wa nchi anayemaliza muda wake.

Sherehe ya kuapishwa

Sherehe za kuapishwa zitaanza saa nne asubuhi hadi saa nane mchana huku eneo la hafla hiyo likifunmguliwa kwa umma mapema saa kumi na mbili asubuhi.

Mara tu Wakenya na wageni wote wanaohudhuria watakapotulia, msafara wa Rais mteule na ule wa naibu wake utaingia katika uwanja huo ukiambatana na gwaride la kijeshi ambalo litakuwa tayari watakapowasili.

Baada ya hapo rais anayemaliza muda wake atajitokeza kwa sherehe ya makabidhiano na itatanguliwa na kipindi kifupi cha maombi na burudani kutoka wasanii mbalimbali.

Jaji Mkuu atamuapisha rais mteule pamoja na Msajili wa Mahakama Kuu.

Mara tu rais mteule atakapoapishwa naibu wake vile vile atakula kiapo cha afisi ambapo Rais Kenyatta atakabidhi vyombo vya mamlaka kama vile Katiba na upanga wa mamlaka kwa rais mpya.

Naibu rais aliyeapishwa atapanda jukwaani kutoa hotuba na kisha atamwalika rais anayeondoka madarakani. Hotuba zao zitatayarishwa na kamati ya maandalizi.

Baada ya hayo, Mkuu wa Nchi anayeondoka atamkaribisha rais ajaye wa Kenya jukwaani kutoa hotuba yake. Wimbo wa taifa utapigwa huku bendera ya rais ikibadilishwa ili kuendana na utawala mpya.

Rais anayemaliza muda wake ataondoka kuelekea Ikulu ili kukabidhi rasmi ikulu kwa mrithi wake. Wakati huo huo, rais aliyeapishwa atazungushwa uwanjani kwa gari la wazi kuwasalimu Wakenya waliohudhuria na kisha atapelekwa hadi Ikulu kwa mazungumzo na rais anayeondoka madarakani.

Baada kikao kifupi , rais anayemaliza muda wake ataondoka katika majengo hayo kuashiria kuwa utawala mpya umeingia rasmi madarakani.

Uchaguzi Kenya 2022:Unaweza pia kusoma