Matokeo ya Uchaguzi Kenya 2022: Vigogo wa Raila Odinga na Uhuru Kenyatta waliolambishwa sakafu

    • Author, Abdalla Seif Dzungu
    • Nafasi, BBC Swahili

Wandani wa Rais Uhuru Kenyatta akiwemo kinara wa walio wengi bungeni Amos Kimunya, Mkurugenzi wa Uchaguzi katika chama cha Jubilee Kanini Kega, katibu mkuu wa Jubilee Jeremia Kioni ni miongoni mwa viongozi waliokubali kushindwa baada ya uchaguzi mkuu wa tarehe tisa.

Viongozi hao walimuunga mkono Raila Odinga aliyekuwa akiungwa mkono na Uhuru Kenyatta katika kinyang'anyiro hicho wakijua kwamba kulikuwa na uwezekano mkubwa kupoteza viti vyao kutokana na wimbi la chama cha UDA katika eneo la Mlima Kenya.

Wimbi la chama cha UDA cha William Ruto liliwafurusha viongozi wote wa eneo hilo waliokuwa wakimuunga Raila Odinga wa Muungano wa Azimio.

Chama cha Jubilee cha Uhuru Kenyatta kilikuwa na wagombea wengi waliowania na wengine kutetea viti vyao katika eneo la Mlima Kenya.

Wakikiri kushindwa kwao viongozi hao walisema kwamba wapinzani wao walikuwa wamechukua uongozi mkubwa wakati wa kuhesabiwa kwa kura.

Bwana Kimunya, ambaye alichukua nafasi ya Mbunge wa Garissa mjini, Aden Duale kama kiongozi wa wengi bungeni mwaka 2020 baada ya mzozo kati ya Rais Kenyatta na naibu wake William Ruto, alishindwa na aliyekuwa mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Bi Wanjiku Muhia wa chama cha William Ruto cha United Democratic Alliance (UDA).

Bwana Kega, ambaye alikuwa akiwania muhula wa tatu hakuwa na bahati kwani kura zilizohesabiwa zilionesha kwamba mpinzani wake kutoka chama cha UDA Njoroge Wainaina alikuwa akiongoza kwa wingi wa kura.

Kwa upande wake bwana Kioni alipoteza kwa mgombea wa chama cha UDA bwana George Gachagua.

Viilevile mbunge wa siku nyingi katika eneo la Taita Taveta Naomi Shaban amekiri kushindwa katika harakati zake za kuchaguliwa kwa muhula wa tano na mgombea wa chama cha Wiper.

Naomi ambaye amekuwa akimuunga mkono Uhuru kenyatta aliwaambia wafuasi wake kwamba matokeo ya mapema yaliotolewa na tume ya Uchaguzi ya IEBC yalionesha kwamba hatohifadhi.

Naomi aliyejiunga na siasa mwaka 2002 ni mmoja ya wanasiasa wakongwe kutoka pwani ya kenya.

Kwingineko mgombea mwenza wa Raila Odinga Martha Karua aliyeteuliwa kuwa mgombea kwa lengo la kuvutia kura ya mlima Kenya katika Muungano wa Azimio pia naye hakuweza kuhimili kishindo cha wimbi la chama cha UDA mlima Kenya.

Martha Karua ambaye alimshinda Kalonzo Musyoka na wagombea wengine waliokuwa wakiwania wadhfa huo wa mgombea mwenza anatoka katika eneo bunge la Gichugu kaunti ya Kirinyaga.

Kulingana na matokeo ya mapema ya eneo hilo wapiga kura wa eneo bunge la Gichugu ambalo Bi Karua aliwahi kuwa mbunge walimpigia kura kwa wingi mpinzani wake William Ruto.

Hatua hiyo imezua mjadala katika mitandao ya kijamii miongoni mwa wafuasi wa Muungano wa Azimio iwapo ushawishi wa mgombea mwenza wa Raila Odinga katika eneo la Mlima Kenya ulimsaidia.

Katika uchaguzi uliopita Raila Odinga alidaiwa kupata asilimia 3 pekee ya kura za eneo hilo lenye idadi kubwa ya wapiga kura nchini Kenya.