Uchaguzi Kenya 2022: Fahamu makosa ambayo hustahili kufanya wakati wa kupiga kura

    • Author, Asha Juma
    • Nafasi, BBC Swahili

Siku ya Jumanne, Agosti 9, 2022 Wakenya zaidi ya milioni ishirini watapiga kura wakiwa wanatimiza haki yao ya kikatiba nchini Kenya, kwa kushiriki kwenye uchaguzi mkuu.

Hili ni zoezi ambalo hufanyika Jumanne ya pili ya mwezi Agosti kila baada ya miaka mitano.

Hiki ni kinyang'anyiro ambacho kinahusisha kuchaguliwa kwa rais, gavana, wabunge,wawakilishi wa wanawake na wawakilishi wa wadi.

Lakini je, kama mpiga kura, unafahamu ni kitu gani ambacho hustahili kukifanya utakapokuwa kwenye kituo cha kupiga kura?

  • Ni hatia kutumia utambulisho wa kupiga kura ambao si wako yaani kadi ya kupiga kura au kitambulisho kisicho chako.
  • Hustahili kwenda kwenye kituo cha kupiga kura ukiwa umevalia sare zinazoashiria mrengo fulani.
  • Ni makosa kuanza kushawishi watu waliopanga foleni kwa nia ya kuwataka kumpigia kura mgombea fulani.
  • Ni hatia kuanza kuhonga wapiga kura kwa ajili ya kuwataka kumchagua mgombea.
  • Pia ni hatia kuanza kupiga picha ovyo wakati zoezi la kupiga kura linaendelea.
  • Ni hatia kuanza kuchana au kuharibu karatasi ya kupiga kura hovyo bila kuruhusiwa kufanya hivyo.
  • Hairuhusiwi kuanza kupiga muhuri au kuweka alama yoyote kwenye karatasi ya kupiga kura.
  • Karatasi za kupiga kura hazistahili kuuzwa kwa yeyote.
  • Pia huruhusiwi kuanza kupeana karatasi ya kupiga kura kwa yeyote tu unayemuona bila kupewa ruhusa.

Kama mpiga kura ukishapewa karatasi ya kupiga kura unafaa kufanya uamuzi wako mwenyewe wala sio kuanza kuuliza wengine wanayempigia au nani utakayempigia kura.

Ukimaliza kupiga kura, karatasi za kupiga kura kila mmoja inastahili kuwekwa kwenye sanduku husika wala sio kuweka popote tu unapojisikia.

  • Hairuhusiwi kuweka kitu kingine chochote kwenye masanduku ya kupiga kura zaidi ya karatasi ya kupiga kura.
  • Ni makosa kuondoka na karatasi ya kupiga kura kutoka kwenye kituo cha kupiga kura.
  • Pia usiharibu chochote ambacho kinaweza kutatiza shughuli ya upigaji kura.
  • Ni makosa makubwa kupiga kura zaidi ya mara moja.
  • Ni hatia kupatikana na karatasi ya kupiga kura ukiwa nje ya eneo la kupiga kura.

Wewe ikiwa sio afisa wa Tume huru, bila ruhusa yoyote kutoka kwa afisa husika, haustahili kuondoa chochote cha kupiga kura kabla, wakati au baada ya kupiga kura.

Bila ruhusa, kuchapisha karatasi yoyote ya kupiga kura, au kile kinachoonekana kuwa karatasi hiyo au kile kinachoweza kutumika kama karatasi ya kupiga kura kunaweza kukuweka hatiani.

Sio ruhusa kuanza kusumbua wengine kwa namna yoyote ile wakati wanapiga kura. Na iwapo utakuwa unahitaji usaidizi wowote, kutakuwa na maafisa wa tume ya IEBC watakaokuwepo kujibu swali lako.

Kwa madhumuni ya uchaguzi, ni hatia kutengeneza, kuagiza, kumiliki, vifaa au matumizi yanayoweza kutumika katika utaratibu ambao karatasi ya kupigia kura inaweza kutolewa, kuathiriwa au kufanyiwa ulaghai baada ya kuwekwa kwenye sanduku la kura wakati wa upigaji kura katika uchaguzi wowote.

Kuweka alama yoyote kwenye karatasi yoyote ya kupigia kura kwa mtu yeyote isipokuwa yeye mwenyewe.

Kupiga kura katika uchaguzi wowote wakati huna haki ya kupiga kura.

kujifanya kuwa hajui kusoma au kuandika ili kusaidiwa katika kupiga kura.

Kujifanya kuwa na ulemavu wa macho au ulemavu mwingine wowote ili kusaidiwa katika kupiga kura.

Ukimaliza kupiga kupiga kura, unachotakiwa kufanyani kuondoka kituoni kwa utulivu na kwenda nyumbani kwako kusubiri matokeo.

Kufanya makosa na kupatikana na hatia utawajibika kulipa faini isiyozidi shilingi milioni moja au kifungo kisichozidi miaka sita au vyote kwa pamoja.

Zoezi hili la kupiga kura litafanyika katika vituo 46,229 vilivyotambuliwa rasmi kama vya kupigia kura na Tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) na watakaochaguliwa wakiwa ni pamoja na wafungwa na raia wa Kenya wanaoishi kwenye nchi za nje katika balozi za Kenya.

Makosa ya wajumbe na wafanyakazi wa Tume

Mjumbe wa Tume, mfanyakazi au mtu mwingine mwenye jukumu la kutekeleza kwa mujibu wa sheria yoyote inayohusiana na uchaguzi ni pamoja na:

Kuweka kumbukumbu ya hati yoyote ambayo unajua au una sababu nzuri ya kuamini kuwa ni uwongo, au haamini kuwa ni kweli.

Kumruhusu mtu yeyote ambaye utamfahamu au kuwa na sababu za msingi za kuamini kuwa anaweza kusoma au kuandika kupiga kura kwa namna iliyotolewa kwa watu wasiojua kusoma na kuandika.

Kumruhusu mtu yeyote ambaye unafahamu au kuwa na sababu za msingi za kuamini kuwa si mwenye ulemavu wa macho au mtu mwenye ulemavu kupiga kura kwa njia iliyoelezwa kwa watu wenye ulemavu wa macho au watu wenye ulemavu wowote ule.

Kwa makusudi kumzuia mtu yeyote kupiga kura kituoni.

Kwa makusudi kukataa kuhesabu karatasi yoyote ya kupigia kura.

Kwa makusudi kutaa kuhesabu karatasi yoyote iliyopigiwa mgombea

Kuingilia mpiga kura katika upigaji kura wake kwa siri.

Utakapohitajika chini ya Sheria ya Uchaguzi (Na. 24 ya 2011) au sheria nyingine yoyote kutangaza matokeo ya uchaguzi, na kushindwa kutangaza matokeo ya uchaguzi.

Isipokuwa kwa mwanachama, afisa au mtu aliyeidhinishwa kufanya hivyo, ni makosa kutoa tamko au tangazo rasmi la matokeo ya uchaguzi.

Bila sababu za msingi kufanya jambo lolote katika misingi ya kukiuka wajibu rasmi.

Kushirikiana na chama chochote cha siasa au mgombea kwa madhumuni ya kufaidi isivyostahili chama cha siasa au mgombea

Kukiuka sheria kwa makusudi ili kutoa faida isivyostahili kwa mgombea au chama cha siasa kwa upendeleo, kikabila, kidini, jinsia au masuala yoyote kinyume cha sheria.

Kushindwa kuzuia au kutoa taarifa kwa Tume au mamlaka nyingine yoyote husika, kutendeka kwa kosa la uchaguzi lililofanywa chini ya Sheria hii.

Kutenda kosa na kupatikana na hatia, utawajibika kulipa faini isiyozidi shilingi milioni moja au kifungo kisichozidi miaka mitatu au vyote kwa pamoja.

Pia unawezakusoma: