Uchaguzi Kenya 2022: Maafisa na taasisi zitakazohusika katika makabidhiano ya mamlaka

    • Author, Abdalla Seif Dzungu
    • Nafasi, BBC Swahili

Makabidhiano ya mamlaka kutoka kwa utawala mmoja wa rais hadi mwingine ni mojawapo ya mchakato muhimu zaidi katika demokrasia ya Kenya kwani yanahusisha mabadiliko ya sera na wafanyakazi.

Wengi hudhani kwamba mchakato wa mpito hutokea mara tu baada ya uchaguzi lakini kwa kweli, huanza mapema zaidi kuliko hapo.

Kwa mujibu wa Sheria ya Kuchukua Ofisi ya Rais, Serikali iliyopo madarakani inatarajiwa kuunda kamati ijulikanayo kwa jina la Kamati ya Kuchukua madaraka ya Ofisi ya Rais ili kuendesha mchakato huo angalau siku 30 kabla ya Uchaguzi Mkuu.

Huku muda wa kuelekea katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9 ukizidi kuyoyoma, Rais Kenyatta tayari amechapisha katika gazeti rasmi la serikali orodha ya maafisa watakao keti katika kamati itakayosaidia kukabidhiwa kwa mamlaka kwa rais mteule, ikiwemo kumkabidhi maelezo ya usalama pamoja na ushauri

Kamati hiyo imepewa mamlaka chini ya kifungu cha sita cha katiba kuwezesha mchakato wa kumkabidhi Rais anayemaliza muda wake kwa Rais Mteule, kutoa maelezo ya usalama na taarifa za usalama kwa Rais Mteule miongoni mwa kazi nyingine muhimu.

Lakini je maafisa gani hao na taasisi zinazohusika katika uhamisho huo wa mamlaka kutoka raias anayeondoka hadi rais mpya?

Maafisa walioteuliwa na rais na majina yao kuchapishwa katika gazeti rasmi la serikali ni pamoja na

Joseph Kinyua, Dr. Fred Matiangi, Karanja Kibicho, Hillary Mutyambai, Gen. Robert Kibochi, Mkurugenzi wa Huduma ya Intelijesia ya Kitaifa(NIS) director Philip Kameru, Anne Amadi, Kinuthia Mbugua, Mwanasheria Mkuu Kihara Kariuki, Katibu wa Kudumu Jerome Ochieng, Katibu wa Kudumu Julius Muia, Katibu wa Kudumu Macharia Kamau, Katibu wa Kudumu Julius Korir, Katibu wa Kudumu Joe Okudo, na Msimamizi Mkuu wa Kesi za Serikali Ken Ogeto.

Joseph Kinyua - Mkuu wa Utumishi wa Umma

Kinyua ni Mkuu wa Watumishi wa Umma. Akiwa mmoja wa watumishi wakongwe zaidi wa umma nchini Kenya, aliteuliwa wakati Uhuru alipochukua mamlaka mwaka wa 2013. Bwana Kinyua ni kiungo muhimu katika hafla hii ambapo mtumishi mmoja wa serikali {Rais anayeondoka} atakuwa anamkabidhi madaraka mtumishi mpya wa serikali {Rais anayeingia} mamlaka.

Karanja Kibicho - Katibu wa Wizara ya usalama wa Ndani

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Uratibu wa Serikali ya Kitaifa ina jukumu muhimu katika operesheni za usalama wa kitaifa. Wizara hii inasimamia utawala, usalama wa ndani, uchapishaji wa nyaraka za Serikali, Uhamiaji na Usajili wa Watu, Huduma za Udhibiti, Huduma za Magereza na kampeni ya utetezi dhidi ya dawa za kulevya. Wizara hii pia inaratibu shughuli za serikali na inatoa huduma za mapokezi kwa wizara zote za Serikali. Kwa kuzingatia kazi hizi mbalimbali, kazi za wizara hii zimepangwa katika idara kuu tano, hivyo Huduma za Utawala wa Mkoa, Polisi wa Kenya, Polisi wa Utawala, Vyombo vya Habari vya Serikali, na Wakala wa Kitaifa wa Kampeni Dhidi ya Matumizi Mabaya ya Madawa ya Kulevya (NACADA).Bila shaka waziri wa wizara hii atakuwa na jukumu kuu la kumshauri rais mpya kuhusu yanayoendelea katika vitengo hivi muhimu vya usalama.

Hillary Mutyambai -Inspekta Mkuu wa Polisi

Hillary Mutyambai ndiye Inspekta Jenerali wa polisi nchini Kenya. Akiwa mkuu wa huduma ya Polisi lengo lake kuu litakuwa kumshauri kiongozi anayeingia mamlakani kuhusu hali ya usalama nchini na vilevile kuhakikisha kuwa eneo ambalo kiongozi mpya atakuwa akiapishwa lipo salama.

Jenerali Robert Kariuki Kibochi - Mkuu wa Jeshi

Jenerali Robert Kariuki Kibochi ndiye Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya. Akiwa mkuu wa majeshi yote Kenya , Bw. Kibochi ana jukumu kuu la kumshauri rais mpya kuhusu usalama wa mipaka ya Kenya na changamoto zake. Vilevile Jeshi lake linahusika katika jukumu muhimu wakati wa sherehe ya kukabidhi mamlaka kwasababu hutoa upanga unaoashiria mamlaka na kumkabidhi rais mpya anayeingia madarakani. Vilevile jeshi hilo humbadilisha afisa anayemlinda rais .

Philip Kameru, - Mkuu wa kitengo cha Ujasusi Kenya

Ndiye mshauri mkuu wa Rais mpya anayeingia madarakani juu ya usalama wa taifa kwa kuzingatia ujasusi ili kuimarisha usalama wa taifa. Kazi yake ni kuripoti kwa Rais, Baraza la Usalama la Kitaifa na Katibu wa Baraza la Mawaziri akiwajibikia masuala yanayohusiana na ujasusi wa kitaifa na vitisho vinavyoweza kukabiliwa kwa usalama wa taifa na masilahi ya kitaifa kama inavyostahili.

Mwanasheria Mkuu - Kihara Kariuki

Mwanasheria mkuu ndio mshauri mkuu wa serikali kuu. Kazi yake ni kuangalia haki za kibinadamu na kuidhinisha katiba, kuhakikisha kuwa kuna haki kupitia kukuza usaidizi wa kisheria, utawala bora , mikakati ya kukabiliana na Ufisadi ,maadili, elimu ya sheria , mabadiliko ya kisheria. Jukumu lake ni kuhakikisha kwamba arais anaapishwa kwa mujibu wa sheria ya katibana kwamba sheria inafuatwa wakati wa kuapishwa kwa rais mpya.

Msimamizi mkuu wa Kesi za Serikali - Ken Ogeto

Huyu ndiye mwenye dhamana ya kuandaa, kuratibu na kusimamia kazi za utawala na sheria za ofisi pamoja na kumsaidia Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kutekeleza majukumu yake kama Mshauri Mkuu wa Sheria wa Serikali.

Yeye ndiye mwenye dhamana ya kuendesha au kupanga na kusimamia kesi zote za mahakama ikiwa ni pamoja na rufaa au maombi kwa niaba ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Taasisi zinazohusika pakubwa na makabidhiano ya mamlaka Kenya

1.Tume ya Uchaguzi Kenya IEBC

Tume ya uchaguzi ndio kiungo muhimu katika shughuli yote ya kuwachagua viongozi katika taifa lolote lile. Punde tu baada ya kukamilika kwa shughuli yote ya uchaguzi, tume hii humkabidhi rais mteule cheti cha ushindi kabla ya kiongozi huyo kuapishwa rasmi kuwa rais.

2. Idara ya Mahakama

Idara ya Mahakama ndio kiungo muhimu katika kuhakikisha kuwa sheria zote zinafuatwa wakati wa makabidhiano ya mamlaka. Jaji Mkuu ambaye ndiye afisa wa kiwango cha juu katika Idara ya mahakama ndiye anayehusika katika kumuapisha rais mpya na kuandaa mahakamaya juu zaidi iwapo kutakuwa na kesi ya rufaa ambayo itakuwa imewasilishwa na mgombea anayepinga matokeo.

Uchaguzi Kenya 2022:Unaweza pia kusoma