Uchaguzi Kenya 2022:Utaratibu wa kupiga kura Kenya

Wapiga kura nchini Kenya wanajitayarisha kuwachagua viongozi wao tarehe tisa mwezi Agosti mwaka huu .

Mojawapo ya masuala muhimu yatakayofanyika siku hiyo ni kwa wapiga kura kufahamu jinsi ya kutekeleza haki hiyo yao-kupiga kura .

Uchaguzi wa Agosti 9 utashuhudia idadi kubwa zaidi ya vituo vya kupigia kura , pamoja na wapiga kura waliojiandikisha.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imebainisha kuwa jumla ya vituo 46,232 vimesajiliwa mwaka wa 2022, ikiwa ni ongezeko la asilimia 13.08 kutoka 2017 ambapo vituo 40,883 vilisajiliwa. Idadi ya wapiga kura waliojiandikisha pia imeongezeka kutoka 19,611,423 hadi 22,120,458 sawa na ongezeko la asilimia 12.79.

Mtu anapiga vipi kura?

•Mpiga kura anafika kituo alichosajiliwa kupiga kura. Kisha anatakiwa kutoa kitambulisho cha kitaifa au pasipoti aliyotumia kujiandikisha kupiga kura .

•Maafisa wa tume ya uchaguzi watahakiki ikiwa aliyefika amesajiliwa kupiga kura katika kituo hicho, kwa kuweka kidole chake kwenye mtambo wa kuwatambua wapiga kura kwa kutumia alama ya kidole.

•Mpiga kura atakabidhiwa karatasi sita za kupigia kura - ya rais, mbunge, gavana, seneta, mwakilishi wa wanawake na diwani (mwakilishi wa wadi) - zilizopigwa muhuri na zenye majina na vyama vya wagombeaji .

•Mpiga kura atasonga hadi eneo la faragha na kumchagua mgombea anayemtaka kwa kuweka alama ndani ya sehemu (kisanduku) iliyotengwa katika karatasi ya kura.

•Tumbukiza karatasi yako ya kura ndani ya sanduku lifaalo kwa kila kura (rais, mbunge na kadhalika).

•Kidole chako kitapakwa rangi isiyofutika kwa urahisi kuzuia watu waliopiga kura kurudia kupiga kura tena.

•Ondoka kutoka kituo cha kupiga kura.

Nani anayeruhusiwa kupiga kura?

Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi nchini kenya mtua anaruhusiwa kupiga kuwa iwapo atatosheleza vigezo vifuatavyo;

(a) ni raia mtu mzima;

(b) hajatangazwa kuwa na akili taahira; na

(c) hajatiwa hatiani kwa kosa la uchaguzi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Raia ambaye ana sifa za kuandikishwa kama mpiga kura ataandikishwa katika kituo kimoja tu cha uandikishaji.

Mipango ya kiutawala ya uandikishaji wa wapiga kura na uendeshaji wa uchaguzi itaundwa ili kuwezesha, na haitamnyima raia anayestahiki haki ya kupiga kura au kugombea.

Kunyimwa Haki ya kupiga kura nchini Kenya

Hali ambayo inaweza kusababisha mtu kunyimwa haki ya kupiga kura nchini Kenya ni pamoja na zifuatazo:

1. Sio Raia wa Kenya

Mtu anaweza kunyimwa haki ya kupiga kura nchini Kenya ikiwa mtu huyo si raia wa Kenya. Kuna njia tatu za kuwa raia wa Kenya ambazo ni kwa kuzaliwa, kujiandikisha au kupata uraia. Uthibitisho wa kitambulisho cha kitaifa (ID) au pasipoti halali ya Kenya unahitajika ili kupiga kura nchini Kenya.

Kwa hivyo, ikiwa mtu si raia wa Kenya, hawezi kupiga kura katika uchaguzi.

2. Sio Wa Umri wa ufaao kupiga kura.

Ikiwa mtu yeyote yuko chini ya umri wa miaka kumi na minane, hastahili kupiga kura nchini Kenya. Kwa hivyo watoto wadogo hawawezi kupiga kura kwa vile umri wa kupiga kura nchini Kenya ni miaka 18 na zaidi. Ushahidi wa kuwa mtu mzima ni aidha kitambulisho cha taifa (ID) au pasipoti halali ya Kenya.

3. Mtu asiyekuwa na akili timamu

Kuwa na akili timamu maana yake mtu anaweza kufikiri, kuelewa na kujiamulia. Watu wazima kwa ujumla hufikiriwa kuwa na akili timamu isipokuwa hali zibadilike. Kwa hivyo, mtu asiye na akili timamu anaweza kunyimwa haki ya kupiga kura nchini Kenya.

4. Kutiwa hatiani kwa Kosa la Uchaguzi

Kunyimwa haki ya kupiga kura nchini Kenya kunatumika kwa yeyote aliyepatikana na hatia ya makosa ya uchaguzi katika kipindi cha miaka mitano iliyotangulia.

5. Mahali pabaya pa kujiandikisha

Ikiwa mpiga kura atajiwasilisha katika kituo cha kupigia kura ambacho ni tofauti na alichojiandikisha, basi anaweza kunyimwa haki ya kupiga kura. Kila mpiga kura anapaswa kuhakikisha kuwa anajitokeza katika kituo cha kupigia kura alichojiandikisha.

6. Kujisajili kama mpiga kura mara mbili

Iwapo mtu atagundulika kuwa amejiandikisha mara mbili katika rejista ya wapiga kura, basi mtu huyo anaweza kunyimwa haki ya kupiga kura.

7. Hana Kitambulisho

Wakati wa siku ya uchaguzi, ikiwa mtu hana kitambulisho chake cha kitaifa (ID) au pasipoti halali ya Kenya aliyojiandikisha nayo, au ikiwa mojawapo ya hati hizi ina kasoro, anaweza kunyimwa haki ya kupiga kura.

8. Hakuna Jina Katika Daftari la Wapiga Kura

Ikiwa jina la mtu halipo kwenye rejista ya wapiga kura, basi mtu huyo anaweza kunyimwa haki ya kupiga kura. Kwa hivyo, ni muhimu kujiandikisha kama mpiga kura wakati wa mchakato wa usajili wa wapiga kura.

9. Kizuizi cha Wakati/Muda

Ikiwa mtu atajiwasilisha kwenye kituo cha kupigia kura nje ya saa alizopangiwa za kupiga kura wakati wa siku ya uchaguzi, anaweza kunyimwa haki ya kupiga kura.Hata hivyo hilo linaweza pia kutegemea muda ambao upigaji kura ulianza katika kituo hicho ama wakati kituo husika kilifunguliwa.Tume ya uchaguzi hutoa mwongozo kuhusu hali ambazo zinaweza kulazimisha muda kuongezwa katika baadhi ya vituo.

Kura iliyoharibika ni ipi?

Kuna sababu nyingi ambazo husababisha kura kuharibika na hivyo kutohesabiwa.

Kuu zaidi huwa ni mpiga kura kuweka alama kwa njia isiyofaa wakati wa kuchagua mgombea au chama anachokitaka.

IEBC inasema mpiga kura anatakiwa kuweka "alama kwenye nafasi iliyotengwa kwa jina la chama/mgombeaji au picha ya chama unachokichagua."

Mpiga kura anafaa "kuweka alama kwa mgombeaji mmoja tu." Hufai kuweka alama yoyote nyingine kwenye karatasi ya kura.

Alama unayoweka inaweza kuwa alama ya ndio (✓), mkasi (✕), au hata alama ya kidole. Hata hivyo, huruhusiwi kuandika jina lako au kuweka sahihi yako kama alama ya kumchagua mgombea unayemtaka. Iwapo utafanya makosa bila kukusudia wakati wa kuweka alama yako kwenye karatasi ya kura na utambue hilo kabla ya kutumbukiza karatasi yako kwenye sanduku, unaweza kupewa karatasi nyingine ya kura. Unaweza kupewa karatasi mpya ya kura mara mbili pekee.

Baada ya kumaliza kuweka alama, unafaa kuikunja karatasi katikati -kutoka kushoto kwenda kulia ili kuweka siri uliyemchagua halafu utumbukize karatasi hiyo kwenye sanduku lifaalo.

Tume ya uchaguzi imepiga marufuku kurandaranda katika kituo baada ya kupiga kura. Vile vile, ni hatia kupiga picha katika kituo cha kupiga kura au kupiga picha karatasi za kura.

Uchaguzi Kenya 2022:Unaweza pia kusoma