Yusuf Ali Abdi: Raia wa Somalia aliyemuua mwanae Ireland ataka kufidiwa

Mwanaume mmoja raia wa Somalia aliyehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa mauaji ya mtoto wake amezua utata baada ya kubainika kuwa alikamatwa visivyo na kuruhusiwa kutafuta fidia.
Mnamo 2019, kifungo chake kilibatilishwa baada ya miaka 16 jela, na anatarajiwa kuachiliwa.
Yusuf Ali ni nani?
Machache yanajulikana kumhusu Yusuf Ali Abdi, lakini alikuwa mmoja wa Wasomali wachache waliokimbia Somalia wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Mnamo 1997, Yusuf alihamia Ireland, ambapo alianza tena maisha yake.
Daud Abdullahi Gilingil, Msomali anayeishi Ireland, aliwasiliana na BBC Somali ili kutoa maelezo kuhusu Yusuf. Anatuambia kuwa Yusuf alikutana na mwanamke wa Ireland mwaka 1998 na wakafunga ndoamwaka uliofuatia. Daud amekuwa akifuatilia kesi hiyo kwa karibu.
Mauaji ya mtoto yalitokeaje?
Wakati wa mwaka mmoja ambao Yusuf Ali na mke wake wa Ireland walikuwa pamoja walipata mtoto.
"Mnamo Aprili 2001, mwanamke huyo aliyekuwa na mtoto alimtembelea Yusufu nyumbani kwake, alisema. Alimchukua mtoto akiwa amelala na kumfungia chumbani," alisema Daud Abdullahi, akisimulia jinsi mauaji yalivyofanyika.
Aliendelea kueleza: "Mwanamke huyo alisikia kelele na akaamka na kumuona Yusuf akimgonga mtoto kwenye ukuta . Alipiga kelele na askari wakafika huku wakimkuta mtoto akiwa amekufa.
"Yusuf alikamatwa, akafikishwa katika mahakama ya sheria, na mwaka 2003 alihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa mauaji ya mtoto."

"Uchungu unamwambia kuua"
Baada ya kukamatwa, Yusuf alisema mara kwa mara kwamba alikuwa na ugonjwa wa akili na alikimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Somalia.
Pia alisema babake aliuawa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
"Amekuwa akisema mara kwa mara kuwa ana ugonjwa unaomwambia aue, kwani ameona madhara ya vita vya wenyewe kwa wenyewe," Daud alisema.
Hatimaye serikali imeamua kumpeleka katika hospitali ya wagonjwa wa akili, kuangalia afya yake ya akili.

Chanzo cha picha, PA
Baada ya kuzuiliwa kwa takriban miaka 10, tume ya uchunguzi iliundwa mwaka 2013 kuchunguza madai yake ya ugonjwa.
Kamati maalum iliyopewa jukumu la kuripoti afya yake iligundua kuwa hakika Yusuf Ali Abdi alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa akili, ambao ulimfanya kumuua mtoto wake .
Kwa mujibu wa sheria za nchi, mgonjwa wa akili hawezi kuhukumiwa kwa kosa alilofanya na kusababisha kufutwa kwa kifungo chake cha maisha mwaka 2019.
Mwanamume huyo anatarajiwa kuachiliwa wiki ijayo, Daud aliambia BBC, na anataka kulipwa fidia kwa kuwekwa kizuizini bila haki.
Hatima ya raia huyo wa Somalia itajulikana siku chache zijazo baada ya mapitio zaidi ya kesi yake.












