Madrid vs Liverpool: Liverpool inapigiwa chapuo, historia inaipa nafasi Real kwenye fainali ya Ulaya

FAINAL

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Yusuph Mazimu
    • Nafasi, BBC Swahili

Juma lililopita Simba na Yanga, mahasimu wa kubwa wa soka Tanznaia ziliwapa burudani bora ya soka watanzania, licha ya kwenda sare tasa. Likiwa joto halijapoa Jumapili hii katika uwanja wa Kasarani Gor Mahia watakipiga na AFC Leopards katika 'debi' maarufu ya mashemeji kwenye ligi kuu ya Kenya.

Mechi za namna hii ndizo zinazoleta ladha ya soka, kwa hamasa na ushabiki. Lakini wiki tatu zijazo, mashemeji, wajomba, dada na kaka watakuwa kwenye makochi, viti vya nyumbani na baa na hata kwenye mikeka wakiangalia mchezo mkubwa zaidi kwenye soka kwenye michuano mikubwa zaidi ya soka kwa ngazi ya klabu, ligi ya mabingwa Ulaya.

Liverpool na Real Madrid zinakutana Mei 28 katika fainali ya kihistoria ya ligi ya mabingwa Ulaya itakauopigwa kwenye dimba la Stade de France huko Ufaransa.

Liverpool iliiondosha Villareal kwa jumla ya mabao 5-2 katika nusu fainali huku Madrid ikifanikiwa kuwaondosha Manchester City kwa jumla ya mabao 6-5, kufuatia ushindi wa kusisimu hapo jana wa mabao 3-1.

Pamoja na ubora wa timu zote mbili, Liverpool anapigiwa chapuo na wabashiri wengi kwamba itatwaa taji la Ulaya mwaka huu, huku historia ikiipa nafasi Real Madrid.

'Michuano hii ya Ulaya ni kama imetengenezwa kwa ajili ya Real Madrid, hawa jamaa wanaweza kucheza mechi kubwa na kupata matokeo, bila kujali wamechezaje, Liver ategemee kupanda mlima mrefu', anasema Omary Mkambara mwandishi wa habari za michezo wa BBC.

UEFA

Chanzo cha picha, Getty Images

Wekundu wa Anfield wamekutana na Real Madrid mara tatu katika kipindi cha miaka minne iliyopita, lakini mechi yakukumbukwa zaidi ni ile ya fainali ya 2018 huko Kyiv - fainali ya kwanza ya michuano ya Ulaya kwa Klopp akiwa na klabu ya Liverpool.

Ulikuwa ni usiku ambao kila kitu kilienda mrama kwa upande wa Liverpool, hivyo fainali ya sasa ni ya kulipiza kisasi zaidi. Timu hizi mbili ziliwahi kukutana katika fainali ya ya michuano ya Ulaya mwaka 1981 huko Paris, Liverpool ikaibuka kidedea.

Historia inavyoikataa Liverpool inayopigiwa chapuo kutwaa taji

Kyiv

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Madrid wakishangilia taji lao la Ulaya baada ya kuwatandika3-1 Liverpool katika fainali ya huko Kyiv, 2018

Wachambuzi na wabashiri wengi wa soka wanaipa nafasi Liverpool, kutokana na kiwango chake katika miaka 5 iliyopita, kimeimarika sana lakini historia inaipa nafasi Madrid.

Liverpool itaingia uwanjani ikipigiwa chapuo kutwa taji lake la 7 la Ulaya, wakati Madridi itakuwa inasaka taji lake la 14 la Ulaya. Madrid wameshinda michezo minne kati ya minane iliyopita dhidi ya Liverpool, ambao wameshinda mara tatu, huku kukiwa na sare moja.

Katika kipindi hicho Madridi wamefunga mabao 10 na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara 8 tu. Historia ya hivi karibuni inawabeba zaidi Real Madrid ambvao hawajapoteza katika michezo yao mitano ya iliyopita dhidi ya Liverpool, ambapo wameshinda mechi tatu za kwanza kati ya timu hizo.

Ushindi maarufu wa Liverpool kwenye michuano ya ulaya ulikuwa ule wa mjini Paris, mwaka 1981, ambapo Alan Kennedy alifunga bao pekee wakati Liverpool ilipoilaza Real 1-0 na kutwa taji la Ulaya.

Liver

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Liverpool walitwaa taji lao la mwisho la ligi ya mabingwa Ulaya mwaka 2018, wakiwafunga Tottenhman Hotspurs.

Lakini Real ililipiza kisasi katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ya mwaka 2018, ambapo Gareth Bale alipofunga mabao mawili katika ushindi wa 3-1 mjini Kyiv. Hii ndiyo fainali ya mwisho ya ligi ya mabingwa Ulaya kwa Madrid. Wakati Liverpool ilitwaa taji lake la mwisho la Ulaya mwaka 2019.

'pamoja na historia kuegemea kwa Madrid, Liverpool ya sasa ina mabadiliko makubwa hasa kutafuta ushindi kwa jasho na damu', anasema Raphael Magoha, mfuatilia wa soka la Ulaya.

Hii itakuwa fainali ya 10 kwa Liverpool, ambayo imetwaa mataji 7 ya Ulaya. Ni Real Madrid pekee (13) na AC Milan (7) ndio wametwaa mataji mengi zaidi ya majogoo hayo ya Anfield. Buyern Munich (6) na Barcelona (5), ziko nyuma ya Liverpool.

Madrid imecheza fainali 16 kati ya hizo imepoteza 3 tu.

Ubora na viwango katika msimu huu

Liverpool imekuwa na msimu mzuri zaidi pengine kuliko miaka mingi iliyopita. Inawania mataji manne msimu huu. Iko nyuma ya Manchester City kwa alama moja, ikisalia michezo minne ligi kumalizika, inacheza fainali dhidi ya Chelsea Mei 14, imetwaa tayari Carling Cup, ikiisubiri Madrid kwenye fainali ya mabingwa Ulaya.

Mfumo wao wa 4-3-3, ukibebwa zaidi na kasi ya washambuliaji wake, unaleta wasiwasi kwa Real Madrid kwenye mchezo huo wa fainali. Katika michuano hiyo msimu huu ikishinda mechi 10, sare 1 na kupoteza mmoja.

Ikiwa klabu ya 3 kwenye viwango vya ubora Ulaya, chini ya meneja Jurgen Klopp, kitacheza fainali yake ya 3 katika misimu mitano iliyopita.

Real Madrid, chini ya Muitalia, Carlo Ancelotti, imekuwa na wakati mzuri pia msimu huu, imetoka kutwaa taji la Laliga, likiwa ni la 35 katika historia. Inashika nafasi ya 5 kwa vilabu bora Ulaya, msimu huu ikishinda michezo 8 na kupoyteza minne katika ligi ya mabingwa Ulaya.

Ni kati ya Benzama vs Salah

Ulaya

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Benzema (kushoto) na Salah katika fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya, 2018

Timu zote zinajivunia kuwa na wachezaji mahiri wanaoweza kuwapa matokeo bora wakati wowote. Real Madrid wanaye Kareem Benzema, mshambuliaji mfaransa anayepigiwa chapuo la kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia Ballon d'or mwaka huu.

Ni kinara wa mabao katika ligi ya mabingwa Ulaya akiwa na mabao 15, huku akiongoza pia kwa mabao 26 katika ligi kuu ya Hispania 'Laliga'

Mohamed Salah ni sura ya Liverpool kwa sasa, amekuwa mfungaji tegemeo wa Liver, akipachika mabao 8 katika michuano ya ligi ya mabingwa Ulaya mwaka huu, na 22 katika ligi kuu England.

'Ingawa haitakuwa mechi itakayoamuliwa na Benzema na Salah kutokana na timu hizi kuwa na nyota wengine kama Luca Modric na Vinícius (Madrid) au kina Sadio Mane, Luis Diaz na Diego Jota (Liverpool), ila hawa wawili watakuwa na mchango mkubwa sana kwenye matokeo', anasema Magoha.

Salah anatarajiwa kuwika lakini takwimu zinampendelea zaidi Benzema. Mbali na kufunga katika fainali ya mwaka 2018 dhidi ya Liverpool , ndiye kinara katika michezo ya Real Madrid vs Liverpool, akiwa na mabao 4.

Aliwafunga mabao mawili alipokutana não katika michuano hiyo, mwaka 2014, Madrid ikishinda ugenini 3-0, bao lingine likifungwa na Christiano Ronaldo. Ziliporejeana pale Bernabéu , Madrid ilishinda 1-0, likifungwa na Benzema. Mwaka 2018 katika fainali ya Kyiv, Benzema alipachika 1, Gareth Bale mawili, Madrid ikishinda 3-1 na kutwaa taji. Haitashangaza Benzema aliye katika fomu zaidi mwaka huu kuibema Madrid pale Ufaransa.

Baada tu ya Liverpool kufuzu fainali, Mo Salah alisema anatamani sana kukutana na Madrid, ombi lake ni kama limekubaliwa na sasa anatazamwa kuona nini anaweza kufanya kuisaidia Liverpool kutwaa taji la saba la Ulaya au kuizuia Madrid kutwaa taji lake la 14.

Salah hakufanikiwa kumaliza katika mchezo wa fainali ya mwaka 2018 dhidi ya Madrid, aliumizwa na Sergio Ramos, pengine ametamani kukutana não kumalizia utamu aliouacha mwaka 2018 au kulipiza kisasi cha kupoteza fainali hiyo.