Karim Benzema kutwaa tuzo ya Ballon d'Or mwaka huu?

Benzema
    • Author, Yusuph Mazimu
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Ligi nyingi za soka duniani ziko ukingoni wakati huu; Ulaya, Amerika, Asia na Afrika mataifa mengi yanakamilisha ligi zao na ligi za kimataifa za kikanda. Mfano barani Afrika zimeshapatikana timu 4 zilizotinga hatua ya nusu fainali ya ligi ya mabingwa na 4 kwenye nusu fainali ya kombe la Shirikisho. Simba ya Tanzania iliaga mashindano ya kombe la Shirikisho Afrika kwa mikwaju ya penati dhidi ya Orlando Pirates, TP Mazembe ikisalia kama mwakilishi pekee wa Afrika Mashariki katika mashindano hayo ikifuzu nusu fainali kwa kuiondosha Pyramids kwa mabao 2-0.

Lakini macho mengi ya wapenda soka yalikuwa katika ligi ya mabingwa Ulaya. Wiki hii kulishuhudiwa michezo ya nusu Liverpool ikiichapa 2-0 Villareal pale Anfield katika mzunguko wa kwanza, huku Manchester City ikipata ushindi wa mabao 4-3 dhidi ya Real Madrid. Lakini matokeo ya mechi hizi hayakuwa masuala pekee yaliyovutia bali 'kiwango bora' cha Mfaransa Karim Benzema.

Benzema

Chanzo cha picha, Gonzalo Arroyo Moreno

Kiwango chake kwenye hatua za mtoano za ligi ya mabingwa, achilia mbali kwenye timu ya taifa na ligi kuu ya Hispania, mshambuliaji huyu 'amethibitisha' kwamba anastahili kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia Ballon d'Or msimu huu.

Kwanini Ballon d'Or ya mwaka huu ni ya Benzema?

Karim Benzema amekuwa na msimu mzuri akiwa na klabu yake ya Real Madrid, msimu unaomfanya kuwaacha kwa mbali washindani wake kwenye tuzo ya mwaka huu ya Ballon d'Or.

Jumanne wiki hii Benzema alipachika mabao mawili dhidi ya kikosi cha Pep Guardiola, Manchester City, kilichoshinda kwa mabao 4-3 katika mzunguko wa kwanza wa nusu fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya.

Mabao hayo ya Benzema yameipa matumaini 'Los Blancos' kusaka angalau goli 1 tu kwenye mzunguko wa pili nyumbani pale Bernabeu, ili kuifanya nusu fainali hiyo ilale kwenye uwiano sawa, kabla ya kusaka ushindi na kufuzu fainali.

Nyota wengi wa soka wa zamani wanamtaja Benzema kama mshindi ajaye wa Ballon d'Or. Thierry Herny, mfaransa mwenzake na gwiji la zamani la Arsenal, na kocha msaidizi wa Ubelgiji anasema hata kama hajatwaa ubingwa wa Ulaya, Benzema atatwaa Ballon d'Or. Mwandishi na mchambuzi wa soka Italia, Fabrizio Romano, na yeye amempigia chapuo Benzema kutwaa Ballon d'Or.

Ruka X ujumbe
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: Imetoka kwingine na inaweza kuwa na matangazo

Mwisho wa X ujumbe

Katika mashindano yote mpaka akiwa na klabu yake na timu ya taifa Ufaransa, mkongwe huyo mwenye miaka 34 amepachika mabao 46 goals na kutoa pasi 14 za mabao katika michezo 48, takwimu hizi zinambeba mbali.

Akiwa na Madrid, amepachika mabao 41 katika michezo 41 msimu huu na kuwa mchezaji wa kwanza kufikisha idadi hiyo ya mabao katika msimu mmoja, baada ya Cristiano Ronaldo, Ferenc Puskas, Alfredo Di Stefano na Hugo Sanchez.

Ni hii ni kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2017/18, Benzema kufunga mabao 41, na kuwa mchezaji wa kwanza wa Real Madrid kufanya hivyo tangu Ronaldo.

Benzema amekuwa na mchango mkubwa katika ushindi wa Real Madrid wa Supercopa de Espana na taji la Nations League akiwa na Ufaransa. na Sio muda mrefu atatwaa taji la ligi kuu ya Hispania, kwa sababu ya pengo la alama 15 lililopo kati ya timu yake ya Madrid na Barcelona inayoshika nafasi ya pili. Kwa sasa kikosi cha Carlo Ancelotti kinaongoza ligi kwa alama 78 ilizozoa kutokana na michezo 33, huku Benzema akiongoza kwa kupachika mabao 25 mpaka sasa kwenye ligi hiyo.

Mwaka uliopita Karim Benzema alimaliza katika nafasi ya nne kwenye tuzo za Ballon d'Or nyuma ya Lionel Messi, Robert Lewandowski na Jorginho.

Wanaomfuatia kwa karibu kwenye Ballon d'Or

Mane

Chanzo cha picha, Getty Images

Kwa sasa Benzema anawashindani watatu wa karibu kwenye kuwania tuzo ya mwaka huu ya Ballon d'Or. Msenegali Sadio Mane anayechezea Liverpool ambaye amekuwa na msimu mzuri wa mataji akitwaa kombe la Afrika (AFCON 2022) akiwa na Senegal, akifunga penati ya ushindi dhidi ya Misri kama alivyofanya tena dhidi ya Mafarao hao hao alipoipeleka Senegal kwenye fainali za kombe la dunia za Novemba huko Qatar. Bila shaka tuzo ya mchezaji bora wa Afrika mwaka huu ni yake lakini kwa nafasi ya Liverpool sasa inayowania kutwaa mataji manne msimu huu Mane anatishia nafasi ya Benzema kwenye Ballon d'Or.

Ameshaisaidia Liverpool kutwaa kombe la Community Shield msimu huu na kombe la ligi (League Cup), wako nyuma kwa alama 1 dhidi ya Manchester City kwenye mbio za kuwania taji la ligi kuu msimu huu. Amefunga bao muhimu jumatano wiki hii, Liverpool ikiichapa Villareal 2-0 kwenye mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya.

Mo salah

Chanzo cha picha, Getty Images

Nyota mwenzake wa Liverpool Mohamed Salah nae hayuko mbali na Ballon d'Or ya mwaka huu. Mmisri huyo mwenye miaka 29 ameifungia Liverpool mabao 30 na kutoa pasi za mabao 13 katika mechi 43 alizoichezea Liverpool msimu huu. Mwingine ni kiungo matata wa Manchester City, Kevin De Bruyne ambaye amekuwa akifunga na kuto pasi muhimu za mabao kuisaidia City kufanya vyema kwenye ligi kuu na ligi ya mabingwa Ulaya. Katika ushindi wa City wa mabao 4-3 wa nusu fainali dhidi ya Real Madrid, De Bruyne alifunga bao moja na kutoa pasi moja. Tuzo za mwaka huu pengine zitashudia kwa mara ya kwanza katika muongo mmoja uliopita ikiwakosa muargentina Lionel Messi mwenye rekodi ya kutwaa tuzo hiyo mara 7 na Christiano Ronaldo anayeshikilia nafasi ya pili kwa wachezaji waliotwaa tuzo hiyo mara nyingi toka kuanzishwa, akitwaa mara 5.