Vita vya Ukraine: "Nilimwona mwanajeshi wa Urusi akimpiga risasi baba yangu na kumuua huko Bucha '

Mwendo wa saa 11:00 mnamo Machi 17, Yuriy Nechyporenko na baba yake, Ruslan, walikuwa wakiendesha baiskeli hadi jengo la utawala la Bucha ambapo misaada ilikuwa ikitolewa. Umeme, gesi na maji vilikuwa vimekatwa, na mahitaji muhimu yalikuwa haba mjini humo , mmoja wa mji wa kwanza kukaliwa na wanajeshi wa Urusi waliposonga mbele kuelekea mji mkuu wa Ukraine wa Kyiv.

Yuriy na baba yake walitarajia kuchukua dawa na chakula. Yuriy alisema askari wa Urusi alimsimamisha yeye na baba yake huko Tarasivska St. Mara moja waliinua mikono yao.

Akiongea na BBC kwa njia ya simu pamoja na mamake, Alla, mtoto huyo wa miaka 14 alitoa maelezo yake kuhusu kilichotokea baadaye. "Tuliwaambia kuwa hatukuwa tumebeba silaha yoyote na kwamba hatukuwa na hatari yoyote," alisema.

"Kisha baba yangu akageuza kichwa chake upande wangu, na hapo ndipo alipopigwa risasi... Alipigwa risasi mbili kifuani, pale moyo ulipo. Kisha akaanguka."

Wakati huo, kijana huyo alisema, askari huyo alimpiga risasi katika mkono wake wa kushoto na akaanguka pia. Akiwa chini, alisema, alipigwa risasi tena, safari hii mkononi.

"Nilikuwa nimelala juu ya tumbo langu, sikuweza kuona chochote kilichokuwa kikitokea karibu yangu," Yuriy alisema. Yule askari, alisema, alipiga tena risasi akilenga kichwa chake. "[Lakini] risasi ilipitia kwenye kofia yangu."

Yuriy alisema askari huyo alimpiga risasi tena, wakati huu katiaka kichwani cha baba yake. Lakini Ruslan alikuwa tayari amekufa. "Nilipata mshtuko mdogo wa hofu, nikiwa nimelala huku mkono wangu uliokuwa na jeraha ukiwa chini yangu. Niliona mkono wangu ukivuja damu," alisema.

Ilikuwa tu baada ya muda, wakati askari alipoenda nyuma ya kifaru , Yuriy aliinuka na kukimbia, alisema.

BBC haijathibitisha kwa uhuru maelezo ya Yuriy, lakini inakuja huku ushahidi ukiongezeka wa ukatili uliofanywa na vikosi vya Urusi wakati walipokuwa wakidhibiti Bucha na miji mingine kaskazini mwa Kyiv.

Huko Bucha pekee, miili ya watu waliokufa ilipatikana barabarani, wengi wao wakiwa na majeraha makubwa. Wengine walikuwa wamepigwa risasi kwenye vichwa, kana kwamba wameuawa. Wengine walikuwa wamefungwa mikono au miguu nyuma ya migongo yao. Baadhi yao walikuwa wamevamiwa na mizinga.

Miili mingi ilionekana kando kando ya Yablonska St, kilomita 2 tu (maili moja) kutoka mtaani ambako Ruslan anasemekana kuuawa.

Mamake Yuriy Alla aliambia BBC jinsi alivyoenda kumuona mumewe baada ya kijana huyo kurudi nyumbani na kumweleza kilichotokea. Alifikiri Yuriy anaweza kuwa na makosa, na kwamba Ruslan alijeruhiwa, akihitaji msaada wa matibabu.

"Mwanangu alinisihi nisifanye hivyo," Alla alisema. "Alisema wataniua pia."

Alipojaribu kutembea barabarani, alisema, majirani zake walimzuia. "[Waliniambia] nisiende mbali zaidi, wakisema Warusi walikuwa wakiua kila mtu katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wao."

Unaweza pia kusoma

Asubuhi iliyofuata, Alla alimwomba mama yake amsaidie. Wakiwa wamevaa mitandio ya rangi nyeupe, walikwenda kwenye eneo la shambulio hilo. Mama yake alizungumza na askari wa Urusi na wakafanikiwa kupita. Hatimaye waliuchukua mwili wa Ruslan, na kuuleta nyumbani.

Picha ya mwili uliokuwa umefunikwa sehemu, iliyopigwa na Alla na kusambazwa na BBC, inaonekana kuthibitisha ushuhuda wa Yuriy. Inaonyesha jeraha la risasi upande wa kulia wa kifua, karibu na moyo.

Ruslan, mwanasheria, alikuwa na umri wa miaka 49 alipouawa. Alikuwa "mtendaji katika jamii," Alla alisema. "Hangeweza tu kuketi kwenye makao na kusubiri. Kwa hiyo, alikuwa akijitolea na kusaidia watu."

Walimzika kwenye bustani ya nyumba ya familia.

Yuriy alisema askari aliyemuua ni Mrusi. Sare yake ilikuwa ya kijani kibichi, alisema, mfano wa jeshi la Urusi. "Niliona kwenye koti lake la ubavu limeandikwa 'Russia' kwa Kirusi," alisema.

"Hatukuwa hatari kwa wanajeshi, tulikuwa raia, tulivaa skafu nyeupe kuonyesha hilo," Yuriy alisema. "Ni mjinga sana."

Ripoti ya ziada na Svetlana Libet