Mzozo wa Ukraine: MONUSCO DRC kuziba pengo la wanajeshi 250 wa Ukraine wanaorejea nyumbani kulinda nchi yao

Tume ya Umoja wa Mataifa (MONUSCO) nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), inaangalia namna ya kuziba pengo la wanajeshi 250 wa Ukraine wanaotarajia kurudi Ukraine kusaidia vita dhidi ya Urusi.

MONUSCO imetangaza kuanza mazungumzo na washirika wake ili kuona namna ya kuziba pengo hilo la wanajeshi hao wa kikosi maalum cha kulinda amani nchini DRC.

Serikali ya Ukraine imeijulisha Umoja wa Mataifa lengo lake la kutaka wanajeshi wake wote ambao wako katika vikosi vya kulinda amani vya umoja wa mataifa kurudi Ukraine kupambana kulinda taifa hilo.

Mpaka sasa hakuna taarifa rasmi ni lini wanajeshi hao wengi wao katika kambi iliyopo Kivu Kaskazini, mashariki mwa DRC, kwenye mji wa Goma, wataanza kurejea Ukraine.

Urusi yaishambulia Ukraine:Mengi zaidi

Msemaji wa msemaji wa tume ya Umoja wa Mataifa MONUSCO nchini Congo Mathias Gilman, anasema MONUSCO inaangalia namna ya kuziba pengo hilo la wanajeshi wa Ukraine pamoja na vifaa vake vya kijeshi zikiwemo ndege za kivita.

Pamoja na kuishukuru Serikali ya Ukraine kwa mchango wake kwa MONUSCO na katika vikosi vya amani vya Umoja wa Mataifa kwa ujumla, Mathias anasema, 'kwa sasa tunatathimini athari za uamuzi huo katika shughuli zetu, ni jana ndio tuliarifiwa kuhusu hatua hiyo na kwa sasa tunaangalia ni kitu gani tutakachofanya ili kuondoka kwa kikosi hicho kuthiathiri shughuli zetu'.

Kuondoka kwa kikosi hicho nchini DRC, kumepokelewa kwa hisia tofauti na wananchi, viongozi na mashirika ya kiraia. Mbunge wa bunge la nchi hiyo na msimamizi wa kamati ya usalama ya bunge hilo, Juvenal Munubo, kwa upande wake anasema kuondoka kwa kikosi hicho chenye uzoefu na utaalamu wa kutumia ndege za kivita hakutakuwa na athari zozote.

Amesema kwa sasa nguvu zielekezwe kwa jeshi la Congo kwa kuwapa vifaa vya kisasa vya kivita na maslahi mazuri.

Wazo la kutoa maslahi mazuri kwa Jeshi la Congo linaungwa mkono na mshauri wa rais wa DRC, Felix Tshisekedi, Jean Jacques Elakano ambaye anasemas 'nchi ya Ukraine inakuwa na matatizo, hatua ya kwanza nchi yoyote inategemea kwanza jeshi lake la ndani na sisi wacongoman ni lazima tutie imani na jeshi letu, hicho kikosi kina wanaheshi zaidi ya 12,000 kama wanaenda 250 haitadhorotesha kitu', Elakano aliiambia BBC

Vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa mataifa nchini DRC, vimehudumu kwa zaidi ya miaka 20, kufuatia machafuko na migogoro ya kisiasa na wenyewe kwa wenyewe yanayoendelea nchini humo na kusababisha vifo.

Nchini Ukraine ni wiki ya pili sasa ya mapigano ya uvamizi wa Urusi, mabali na vifo na majeruhi kadhaa, zaidi ya watu milioni mbili wameikimbia nchi hiyo kwa ajili ya usalama wao