Ukraine na Urusi: Jinsi bei ya chakula kutoka Mashariki ya Kati hadi China inavyoweza kuathirika

Kwa mamilioni ya watu wanaoishi umbali wa maelfu ya kilomita, uvamizi wa Urusi nchini Ukraine unaweza kusababisha matokeo ya maisha halisi - kwenye meza yao ya chakula cha jioni.

Ukraine, inayojulikana kwa karne nyingi kama kitovu cha mkate barani Ulaya, ni muuzaji mkuu wa nafaka kwa nchi za Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati hadi Kusini Mashariki mwa Asia.

Miongoni mwa mazao yake, ngano ina umuhimu mkubwa kama chanzo kikuu cha chakula kwa wakazi wanaotegemea mauzo ya nje ya Ukraine.

"Lebanon inaagiza tani 700,000 za ngano ya Ukraine - ambayo ni sawa na 50% ya usambazaji wao wa bidhaa hiyo," Alex Smith, mchambuzi wa utafiti wa chakula na kilimo kutoka Taasisi ya Breakthrough nchini Marekani, aliiambia BBC.

Nchini Libya, ambapo ngano pia ni muhimu katika kulisha taifa, 43% ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje zinatoka Ukraine.

Nchini Tunisia, hali ni sawa.

"Utegemezi wao kwa ngano ya Ukraine ni 32%," Alex Smith anasema.

"Kwa ujumla, kuna nchi 14 ambazo zinategemea Ukraine kwa angalau 10% ya ngano yao."

Bei ya ngano duniani tayari imekuwa ikipanda, na uvamizi wa Urusi umesababisha hofu kwamba uwezo wa uzalishaji wa ngano Ukraine utatatizwa kwa kiasi kikubwa, na hivyo kusababisha kupanda zaidi kwa bei.

Kulingana na makadirio, baadhi ya 35% ya ngano Ukraine inalimwa katika mashariki ya nchi, kati ya mji mkuu wa Kyiv na maeneo ya waliojitenga katika mpaka wa Urusi, eneo lililo katika hatari zaidi ya uvamizi wa Urusi.

Mara tu baada ya habari za uvamizi huo kuenea, bei ya ngano Ulaya ilipanda hadi juu kabisa kuwahi kurekodiwa.

Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) la Umoja wa Mataifa lilikuwa tayari limeonya juu ya kupanda kwa gharama kabla ya mzozo wa hivi punde kati ya Ukraine na Urusi kuibuka, likionyesha kuwa bei ya chakula duniani ilikuwa imefikia rekodi ya miaka 10 mnamo 2021.

Huku yenyewe ikiwa inakabiliwa na athari za janga hili na ukame mkali ambao umeathiri nchi kadhaa za Afrika Kaskazini, ulimwengu wa Kiarabu uko katika hatari ya kuathiriwa zaidi na ongezeko zaidi la bei kwa sababu ya vita.

Mkate ndio chanzo cha chakula cha bei ya chini katika eneo hilo, ambapo serikali hazina rasilimali za kifedha za kukabiliana na bei kama vile mataifa ya Ulaya yanavyoweza.

Wataalamu katika eneo hilo mara nyingi wanataja hasira ya umma kutokana na kupanda kwa bei ya vyakula kama sababu mojawapo ya maandamano ya Arab Spring mwaka 2011.

Mauzo ya nje ya Urusi

Kando na Ukraine, msambazaji mwingine mkuu wa ngano kwenye soko la dunia ni Urusi, ambayo imetoka kuwa mwagizaji wa 50% wa chakula hadi muuzaji nje ya nchi katika miaka 20 iliyopita.

Kwa hakika, Urusi imekuwa nchi inayoongoza kwa uzalishaji wa ngano duniani, ikisafirisha zaidi ya tani 35m kwa mwaka, mbele ya Ukraine ambayo inashika nafasi ya tano kama msafirishaji wa ngano nje ya nchi.

Huku uvamizi wa Ukraine unavyoendelea, mahitaji ya ngano ya Urusi yanaweza kuongezeka, na hivyo kuchochea wasiwasi wa usalama wa chakula zaidi.

Urusi na Ukraine kwa pamoja zilichangia takriban robo ya ngano duniani, kulingana na ripoti ya 2019 ya Observatory of Economic Complexity (OEC), tovuti ya data kwa biashara ya kimataifa.

Kwa Misri, muagizaji mkubwa zaidi wa ngano duniani, ni jambo linalotia wasiwasi.

Msambazaji mkuu wa ngano wa Misri ni Urusi, ambayo hutoa karibu 80% kulingana na ripoti ya hivi punde iliyochapishwa na Idara ya Kilimo ya Marekani, ikifuatiwa na Ukraine.

Gazeti la Al Ahram lilimnukuu msemaji wa baraza la mawaziri Nader Saad akionya kwamba mzozo wa Urusi na Ukraine unaweza kuvuruga usambazaji wa ngano nchini humo, na kuwataka Umma kuwa uwiano katika matumizi ya mkate.

Wasiwasi juu ya mahindi

Ingawa ngano inapendwa zaidi kwa sababu ya athari zake za kijamii na kisiasa kwa nchi nyingi, mazao mengine makuu ya kilimo ya Ukraine pia yanakabiliwa na kupanda kwa bei.

Ripoti ya Reuters inaiweka Ukraine kama nchi inayoongoza duniani kwa kusambaza mafuta ya alizeti na mahindi ya Ukraine yanachangia 16% ya mauzo ya nje duniani.

Takriban 90% ya mahindi yanayoagizwa kutoka China yanatoka Ukraine.

Wakati mauzo ya ngano ya Ukraine nje ya nchi yakishika kasi katika miezi ya Agosti na Septemba, usafirishaji wake wa mahindi ni suala la dharura zaidi.

Kabla ya uvamizi huo kuanza, zaidi ya nusu ya kiasi cha mahindi kilichotarajiwa cha Ukraine kiliwekwa kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi katika muda wa miezi mitano ijayo.

Kwa Alex Smith, ulimwengu unapaswa kuangalia kwa karibu athari za vita kwa kilimo cha Ukraine na Urusi.

"Mazungumzo kote Urusi na Ukraine yamejikita zaidi kwenye mafuta na gesi," aliiambia BBC, "lakini pia kuna suala la usalama wa chakula la kufikiriwa."