Je, mazungumzo ya Rais Samia na Tundu Lissu yanatoa pambazuko jipya la kisiasa?

Chanzo cha picha, Ikulu Tanzania
- Author, Damas Lucas
- Nafasi, Mchambuzi wa kisiasa
Baadhi ya mambo hayo ni kesi inayomhusu mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, haki ya vyama vya upinzani kufanya mikutano ya hadhara na maandamano, Katiba mpya, na suala la yeye Lissu na watu wengine waliokimbia nchi kwa sababu za kisiasa kurudi nyumbani.
Mambo mengine ambayo Lissu anasema alizungumza na Rais Samia ni kuhusu suala la wabunge 19 wa viti maalum wa Chadema walio bungeni ambao chama chao kinadai kilishawafukuza uanachama, hivyo kuwanyima haki ya kuwa bungeni, na suala la umuhimu wa Rais kutekeleza ahadi yake ya kukutana na wapinzani kutafuta maridhiano ya kisiasa.
"Rais Samia amefanya jambo la maana sana kunipa fursa ya kuzungumza naye. Tunafahamu kwamba kuna mambo mengi ambayo yanahitaji yajadiliwe, na nimemwambia mheshimiwa rais kuwa sisi (Chadema) tuko tayari kuendelea na majadiliano ya masuala yote yanayotutatiza kama taifa… tuko tayari kushirikiana naye kuyaweka sawa mambo yote ambayo yanahitaji kuwekwa sawa ili mradi tu kuwe na nia ya dhati na ya pamoja ya kuyashughulikia masuala hayo…" Lissu alisema kwenye video fupi aliyoiweka katika ukurasa wa mtandao wake wa Twitter.
Kufungua fursa ya maridhiano
Pamoja na umuhimu mkubwa wa mkutano wa Rais Samia na Tundu Lissu kwa siasa za Tanzania, ni mapema sana kushangilia. Hii ni kwa sababu yote yanategemea jinsi pande zote mbili, za vyama husika vya siasa; CCM na Chadema, zitakavyotumia fursa iliyotolewa kuanzisha maridhiano ya kweli.
Pamoja na kuwa muelekeo wa kisisiasa wa Rais Samia haukujulikana sana kabla hajawa makamu wa rais mwaka 2015, dalili zinaoesha kuwa anapendelea siasa za kidiplomasia zaidi. Kitendo chake cha kumtembelea Tundu Lissu hospitalini alikokuwa amelazwa jijini Nairobi Novemba 29, 2017 kumjulia hali kilithibitisha hilo.
Ndiyo maana kauli yake bungeni kuwa alikuwa na mpango wa kukutana na viongozi wa upinzani kwa mazungumzo ilipokewa kwa bashasha na viongozi wa upinzani na wanaharakati.
Hata hivyo, yaliyotokea baada ya hotuba ya Rais Aprili 22, 2021, ikiwemo kesi ya Mbowe yanaonyesha kuwa nia nzuri ya Rais Samia lazima iendane na mkakati thabiti wa kuwashawishi na hata kuwadhibiti wahafidhina ndani ya chama chake.

Chanzo cha picha, Tundu Lissu
Tatizo haliko kwa Rais Samia tu. Viongozi wa Chadema na vyama vingine vya upinzani nao wana kazi kubwa ya kuwashawishi wahafidhina katika vyama vyao kukubali ukweli kwamba mazungumzo ya kisiasa ni magumu na huchukua muda, na kuwa baadhi ya marekebisho ya kisiasa na kisheria wanayoyadai yanaweza kuchukua muda mrefu zaidi ya wanavyodhania. Utayari wa Chadema kukaa meza moja na CCM, kama alivyosema Lissu baada ya mazungumzo yake na Rais, utaleta matunda kama wafuasi wao wataonesha uvumilivu usiotikisika. Sio kazi rahisi kwa pande zote mbili.
Msukumo mpya kwa Rais Samia
Ni wazi kuwa mazungumzo ya Ubelgiji yataweka msukumo wa umma au shinikizo kwa Rais Samia kufanya jambo kupunguza au kuondoa kabisa mtafaruku wa kisiasa ulioikumba Tanzania kwa miaka kadhaa sasa. Nia yake njema ya kukutana na Tundu Lissu itapimwa pia kwa hatua atakazoanza kuchukua kurekebisha baadhi ya masuala ya kisiasa mara baada ya kurejea nchini.
Shinikizo kwa Rais Samia kurekebisha mambo tayari limeshaongezewa uzito pia na matarajio ya jumuiya ya kimataifa kwake yeye kama Rais wa kwanza mwanamke kuonesha tofauti na kutumia busara, upendo na huruma ya kimama kuleta maridhiano katika siasa za Tanzania. Kitendo cha mazungumzo kufanyika nje ya nchi kumeongeza mwangaza wa jumuiuya ya kimataifa na wa vyombo vya habari vya nje kwenye siasa za Tanzania.
Isitoshe Rais Samia ameshatangaza waziwazi nia yake ya kuhakikisha Tanzania inachangamana na jumuiya ya kimataifa. Katika hotuba yake kwa Umoja wa Mataifa Septemba 23, 2021 Rais Samia aliihakikishia dunia kuwa Tanzania haitajifungia bali itatimiza wajibu wake wa kuhakikisha mashirikiano ya kiuchumi na kimaendelo yanapewa kipaumbele kimataifa hasa katika kipindi hiki cha janga la ugonjwa wa Covid-19.
Kwa hiyo umuhimu mkubwa zaidi wa mkutano kati ya Tundu Lissu na Rais Samia ni kuwa unatoa fursa ya kuanza upya kwa siasa za maridhiano Tanzania. Baada ya sintofahamu na uhasama wa waziwazi wa kisiasa uliotokea Tanzania kwa miaka zaidi ya sita iliyopita Tanzania inahitaji maridhiano.

Chanzo cha picha, Getty Images
Tofauti kati ya wapinzani na wana CCM ni kubwa sana. Kuna maswali magumu yanayotakiwa kujibiwa. Hatua za kisiasa na hata za kisheria zinahitaji kuchukuliwa kutoa haki kwa walioonewa na makundi ya watu wasiojulikana. Moyo wa dhati unahitajika kerekebisha mapungufu makubwa ya kisiasa yaliyotokea nyuma. Ni busara kukubali kuwa maridhiano, kama yakianza, yatakuwa magumu na machungu, hasa mwanzoni. Lakini bila kuikumbatia fursa iliyotolewa kwa mazungumzo yaliyofanyika Jumatano Februari 16, maelfu ya kilomita kutoka Tanzania, vidonda vya kisiasa havitapona na vinaweza kusababisha mpasuko wa hatari kwa amani ya nchi miaka ijayo.
Kutumia fursa hii ya mazungumuzo kuanzisha maridhiano inahitaji ujasiri na ukomavu mkubwa wa kisiasa kutoka kwa Rais Samia. Inamtaka awe na uwezo wa kung'amua na kuweka maslahi mapana ya taifa mbele.
Wapinzani nao wanahitaji kuonesha uvumilivu na utulivu wakizingatia kuwa Rais Samia naye anahitaji muda kidogo kutikisa matawi ya chama chake kujua kuti kavu liko wapi na kuona wapi panavuja kabla hajajikinga mvua chini ya mti wa CCM wakati wa maridhiano.
Iwapo wanasiasa wataichukua kikamilifu fursa hii ya maridhiano iliyojitokeza au la ni suala la muda kuzungumza.












