Mwanamke katili aliyejulikana kama "mwanamke aliye na mbwa" aliyewatesa wapinzani wa kisiasa nchini Chile

Íngrid Olderöck

Chanzo cha picha, Wikimedia Commons

Maelezo ya picha, ngrid Olderöck alikuwa binti wa wazazi Wajerumani

Akijulikana kama "mwanamke aliye na mbwa", Íngrid Felicitas Olderöck Bernhard alikuwa ajenti wa zamani wa Idara ya Kitaifa ya Ujasusi (DINA), huduma ya usalama iliyoundwa na Augusto Pinochet baada ya kumpindua Salvador Allende mnamo mwaka 1973.

Lakini hakuwa hakuwa tu ajenti wa chombo hicho kilichohusika na kuwatesa na kuwaondoa wapinzani wa kisiasa wa serikali ya kijeshi.

Olderöck, afisa wa zamani wa Carabineros, alikuwa mwanamke bora zaidi ndani ya DINA na moja ya kazi zake ilikuwa kutoa mafunzo kwa wanawake vijana ambao aliwafunza kukabiliana na maadui wa kisiasa.

Waathiriwa wanamshutumu kwa kuwa na mbwa waliofunzwa kuwabaka wafungwa wa kisiasa vizuizini ambapo wengi walitoweka.

Hasa katika moja ya maeneo ya siri na ya kikatili zaidi, "La Venda Sexy" , nyumba ya ghorofa mbili katika makazi ya watu wa tabaka la kati wilaya ya Macul, huko Santiago, ambako Íngrid Olderöck alikuwa akifanyia kazi.

Mawakala hao walikipa kituo hicho cha siri jina hilo kwa sababu mbinu iliyopendekezwa zaidi ya utesaji ilikuwa unyanyasaji wa kijinsia, kama ilivyobainishwa katika ripoti ya kwanza ya tume ya kitaifa ya vifungo vya kisiasa na mateso, inayojulikana zaidi kama ripoti ya Valech.

Unaweza pia kusoma:

Ukiukwaji wa matumizi ya mbwa

Manusura waliopitia Bendi ya Sexy, kama vile Beatriz Bataszew, wamekashifu matumizi ya mbwa kama njia ya mateso, pamoja na kunyongwa, kuzamishwa majini, kunyonga kwa dhihaka, mimba za kulazimishwa, kutoa mimba kwa lazima au kupigwa na umeme kwenye sehemu za siri."Beast" is the Oscar-nominated animated short film inspired by the life of Olderöck.

Ingrid Olderöck

Chanzo cha picha, La Nación/U. Diego Portales. Museo de la Memoria.

Maelezo ya picha, Olderöck alikana shutuma zote na hakuwahi kushitakiwa mahakamani

"Katika nyumba ya Sexy Venda kulikuwa na mbwa aitwaye Volodia aliyefunzwa kuwadhalilisha wanawake kingono," alisema katika taarifa kwa vyombo vya habari vya eneo hilo.

Kisa kama hicho ni cha Alejandra Holzapfel, ambaye alikamatwa akiwa na umri wa miaka 19 tu katika nyumba hiyo.

"Nilinyanyaswa kingono na mbwa aina ya German shepherd ambaye maajenti wa udikteta walimwita Volodia," Holzapfel aliliambia gazeti la The Clinic.

"Ingrid alielekeza mnyama huyo, huku watesaji wengine wakiwalazimisha wafungwa kuruhusu unyanyasaji huo. Wanaume na wanawake waliopitia La Venda Sexy walikuwa wahanga wa ukatili huu."

Filamu fupi ya "Beast"

Sura yake imerejea kwenye mjadala wa umma baada ya kuwa mhusika mkuu wa filamu fupi "Beast", na muelekezi wa filamu wa Chile Hugo Covarrubias, ambayo iliteuliwa kwa tuzo za Oscar wiki hii.

Bestia

Chanzo cha picha, Cortometraje Bestia.

Maelezo ya picha, "Beast" ni filamu iliyoteuliwa cha kitengo cha filamu fupi ya vibonzo iliyoelezea maisha ya Olderöck.

"Ni msisimko wa kisaikolojia kuhusu akili mbovu," Covarrubias anaiambia BBC Mundo.

Mmoja wa watu wachache ambao walipata fursa ya kuzungumza sana na ajenti huyo wa zamani alikuwa mwandishi wa habari wa Chile Nancy Guzmán , ambaye alichapisha kitabu "Ingrid Olderöck, mbwa mwanamke", ambamo - kulingana na mazungumzo hayo- anaandika na kumtaja kama "mwanamke mwenye nguvu zaidi na mkatili katika DINA".

Katika nyumba ya Oldeck

Katika mazungumzo na BBC Mundo, Guzmán anasimulia kwamba siku moja mwaka wa 1996 aligonga mlango wa nyumba ya Olderöck kwenye mtaa wa Bremen, katika wilaya ya Ñuñoa.

"Mwanamke mwenye mwili mnene, mikono mikubwa na sauti ya kishindo alionekana, akiwa na sigara mkononi mwake." Alikuwa ni yeye.

Cortesía Paz Errázuriz

Chanzo cha picha, Cortesía Paz Errázuriz

"Alikuwa amevaa sketi ya maua, sweta ya waridi iliyotengenezwa kwa mikono, na buti fupi."

"Aliishi peke yake kabisa," anasema Guzmán. "Hakuwa na watoto, hakuwa na mume."

"Alikuwa afisa aliyesimamia kikosi cha wanawake ndani ya DINA waliofunzwa kuwatesa, kuwatesa na kuwaua wapinzani"

"Alikuwa kama komando mwenyewe. Alikuwa mtaalamu wa upigaji risasi, kuruka angani, kukumbia na farasi na mafunzo ya mbwa."

"Yeye ndiye aliyemfundisha mbwa aitwaye Volodia ambaye wakati wa vikao vya mateso alikuwa na kazi ya kubaka wanawake na wanaume," anasema Guzmán.

"Kuna wafungwa wa zamani ambao walipata mateso hayo au waliona yaliyowapata wengine, wote wanakumbuka kwamba mmoja wa wale vijana wa kike Marta Neira alikuja huku akilia kwa kukata tamaa kwa sababu alikuwa mwathirika wa kubakwa na mbwa, siku kadhaa baadaye Marta alitoweka. "

"Mimi ni Nazi"

Baba ya Íngrid Olderöck alihama kutoka Ujerumani mwaka wa 1925, akiwa na umri wa miaka 29.

Pamoja na dada zake, Hannelore na Karin, walikua chini ya mfumo mkali sana wa familia.

Hawakuruhusiwa kuzungumza Kihispania au kuwa na marafiki wa Chile.

Hivi ndivyo walivyokua wametengwa kivitendo.

Bestia

Chanzo cha picha, Cortometraje Bestia.

"Nimekuwa Mnazi tangu nilipokuwa mdogo, tangu nilipojifunza kwamba kipindi bora zaidi ambacho Ujerumani iliishi ni wakati Wanazi walipokuwa mamlakani, wakati kulikuwa na kazi na utulivu na hakukuwa na wezi wasio na aibu," anasema Olderöck katika kitabu cha Guzmán.

Pia alifanya mazoezi ya tenisi, kuteleza kwenye theluji, kupanda milima na alidai kuwa mtaalamu wa upigaji risasi.

Akiwa na sifa hizo, haraka akawa sehemu ya huduma ya siri iliyoongozwa na Kanali Manuel Contreras: DINA.

Alipoonyesha uwezo wake, Olderöck alijinyakulia nafasi yake ya mamlaka ndani ya kikosi DINA.

Risasi moja kichwani na moja tumboni.

Lakini mnamo 1981 maisha yake yalibadilika.

Akiondoka nyumbani kwake, alishambuliwa na watu wawili wasiojulikana ambao walimpiga risasi kichwani na tumboni, lakini hawakumuua.

Kwa hakika, alinusurika hadi mwisho wa siku zake akiwa na risasi kichwani, asema Guzmán.

Walishutumu wanachama wa Vuguvugu la Mapinduzi ya Kushoto, MIR, kwa shambulio hilo.

Lakini Olderöck kila mara alisisitiza kwamba shambulio hilo lilikuwa limepangwa dhidi yake na idara za kijasusi ambazo zilikuwa zikijaribu kumwadhibu kwa madai ya jaribio lake la kuasi.

Baada ya shambulio hilo alistaafu na wakati mahakama zilipomwita kutoa ushahidi katika kesi za wafungwa waliotoweka kutoka La Venda Sexy, alijifanya kuwa na amnesia, anasema Guzmán.

"Hakuwa na huruma"

Bestia

Chanzo cha picha, Cortometraje Bestia.

"Alikuwa mwanamke mjeuri, mchokozi ambaye hakuwa na huruma," anaongeza.

Katika moja ya mahojiano, alimwambia kwamba kila wakati alikuwa na bunduki tatu: bunduki kwenye mkoba wake, nyingine kwenye meza, na moja kwenye oveni ya jikoni.

"Kwa hiyo alisimama, akaingia jikoni, akarudi na kuweka bunduki juu ya meza, sikujua la kufanya."

"Mpaka nikamwambia 'chukua hii silaha sipendi silaha' na wakati huo anakasirika na kuniambia kuwa anachukia watu wa aina yangu, akaendelea kurudia..' ninakuchukia'.

Hivyo ndivyo mahojiano yalivyokuwa, anasema Guzmán. Katika tukio jingine alimwambia kuwa makini kwa sababu kulikuwa na shirika la maajenti wa zamani liitwalo DINITA na kwamba "chochote kinaweza kumtokea."

Akiwa na umri wa miaka 58, Íngrid Olderöck alifariki akiwa peke yake, kutokana na kutokwa na damu kwenye utumbo, bila kuhukumiwa kwa uhalifu wowote.