Je ni yapi manufaa viliyoyapata vyama vya upinzani Tanzania kwa kujiuzulu kwa Spika Ndungai?

Chanzo cha picha, Bunge
- Author, Markus Mpangala
- Nafasi, Mchambuzi, Tanzania
Kung'atuka madarakani kwa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai mnamo Januari 6, 2022 kumetajwa kuwa ni matokeo ya mwenendo wake na ndiye chanzo cha kuporomoka uhuru wa Bunge,ushindani wa hoja,demokrasia,uvunjwaji wa sheria,matukio ya hofu ya usalama, kuwaadhibu Wabunge wa upinzani kutohudhuria vikao na kuvuliwa ubunge kuwa ni miongoni mwa madoa ambayo yamechafua uongozi wake na uthibitisho wa namna wanasiasa wa upinzani walivyotendewa vibaya hivyo kujiuzulu kwake kunatoa ahueni kwao.
Viongozi na wanasiasa wa upinzani wameelezea uamuzi wa Spika ni nyenzo ya kukoleza madai ya Tume Huru ya uchaguzi na Katiba mpya kwa sababu sasa sakata hilo limewafumbua macho wananchi kuwa Bunge ni mhimili unaodhibitiwa, na pia wamejionea kwa mifano hai juu ya uongozi mbaya na hatari ya Bunge kutawaliwa na uwakilishi wa chama kimoja.
Duru za kisiasa toka vyama vya upinzani vimeeleza kuwa anguko la Spika huyo limetafsiriwa kama ushindi na tafakuri juu ya uhuru wa Bunge pamoja mwenendo wake wa kuwalinda Wabunge wa viti maalumu 19 waliofukuzwa uanachama na Chadema.
Sakata hilo ni kiungo cha msuguano baina ya pande hizo mbili, ambapo wameeleza kuwa matukio waliyokutana nayo kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita yanachora taswira mbaya kwa mwanasiasa huyo ambaye ni Mbunge wa Kongwa mkoani Dodoma.
Spika wa Tanzania anachaguliwa namna gani?
Spika anatakiwa kuwa raia wa Tanzania aliyetimiza miaka 21
- Anayejua kusoma na kuandika Kiswahili na Kiingereza.
- Mwanachama na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa.
- Awe ni miongoni mwa Wabunge waliochaguliwa.
- Awe amedhaminiwa na chama chake
Ni yapi manufaa waliyopata upinzani?
Boniface Jacob, Meya wa zamani wa Manispaa ya Ubungo jijini Dar es salaam wa chama cha upinzani cha Chadema, ameniambia kuwa faida waliyonayo upinzani kwa kujiuzulu Spika, kwanza ni kuona wananchi wanajifunza kwa mifano namna kiti cha Spika chini ya Job Ndugai kilivyobeba ubabe,ukandamizaji na kusisitiza kuwa yote hayo yamefika tamati.
Ameongeza kwa kusema Spika ameondoka katika kiti chake akiwa anaumia moyoni na kujifunza kuwa Bunge la chama kimoja ni hatari kuliko vyama vingi.
"Mimi ni Mkristo naamini katika Mithali 29:2 isemayo wenye haki wakiwa na amri,watu hufurahi, bali mwovu atawalapo, watu huugua. Nikiwa mwanachama na kiongozi wa upinzani yapo manufaa ya kujiuzulu Spika Ndugai, kwanza inakoleza moto wa mikakati yetu na wadau wa haki za binadamu,wananchi kote nchini, wanachama na wafuasi wa Chadema kudai mchakato wa Katiba mpya ili kuiponya nchi yetu.
Uongozi wa Spika Ndugai uliwatendea mambo mabaya wapinzani, amewaumiza, amewadhalilisha na amewaonea.
Kiti cha Spika kilikuwa kinachukua maamuzi yanayoporomosha demokrasia na uhuru wa Bunge badala ya kujenga. Kiti cha Spika hakikutenda haki dhidi yetu, na Bunge lilikosa ile ladha ya ushindani wa hoja, ushauri, utafiti, mashauriano na mijadala ya kujenga nchi yetu. Sasa naona wananchi wamejionea matendo tuyolalamikia kwa miaka mitano ya uongozi wake yamemrudia mwenyewe. Inatupa faida kubwa ya kuaminika na matarajio ni makubwa kwa wananchi na wanachama wetu."

Chanzo cha picha, ACT Wazalendo
Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma wa chama cha ACT Wazalendo, Janeth Joel Rithe kwa upande wake amesema, "Mafunzo yaliyopatikana ni mengi, mfano wa haraka suala la Katiba mpya, ni ajenda ambayo haiwezi kusukumwa bungeni kutokana na Bunge ambalo lilisimamiwa na Spika Ndugai kuwa na wabunge wengi wa chama cha CCM. Tunapokazania Tume huru ya uchaguzi tunaamini itasaidia kupata idadi kubwa ya wabunge na wawakilishi watakaoweza kusukuma ajenda ya Katiba mpya ambayo kwa sasa haiwezi kupatikana, pia kuchochea demokrasia na uhuru wa Bunge letu. Tumeona Rais wa awamu ya sita amekuwa na utashi wa kisiasa wa kukubali tume huru ya uchaguzi kuliko Katiba mpya. Upinzani tutumie upenyo huu sababu dhamira au nia ya Rais iko wazi."
Kuporomoka Demokrasia bungeni
Mathalani hoja ya kuporomoka demokrasia nchini humo ikiwemo Bunge, ripoti ya Freedom House ya mwaka 2021 inabainisha kuwa Tanzania imeanguka katika viwango vya demokrasia kwa kupata asilimia 34 kutoka 60 iliyopata mwaka 2016.
Tathmini ya kipindi cha Spika Ndugai demokrasia iliporomoka kwa kiwango kikubwa ukilinganisha na watangulizi wake.
Anne Makinda na Samuel Sitta waliwahi kushika wadhifa wa Uspika kwa nyakati tofauti. Sitta alianza mwaka 2005-2010, ambapo alikabidhi kiti hicho kwa Anne Makinda 2010-2015. Inaoneka bayana wanasiasa wa upinzani walifurahishwa na vipindi vya viongozi wawili hao na kwamba demokrasia ndani ya Bunge iliwapa nafasi ya kutoa mchango mkubwa.
Watangulizi hao walisimamia demokrasia, wabunge wa upinzani walipata nafasi sawa na chama tawala zaidi. Katika kipindi cha Bunge la 2010-2015, Zitto Kabwe aliibuka kuwa Mbunge machachari wa upinzani aliyekusanya saini za wabunge wenzake ili kukamilisha akidi ya kumng'oa madarakani Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Katika kipindi hicho, aliyewahi kuwa Spika Pius Msekwa alikaririwa na vyombo vya habari kuwa Bunge hilo lilikuwa limechangamka na utamaduni wa umwamba wa kisiasa ulionekana na kudumisha demokrasia.
Msuguano wa upinzani na Spika
Mosi, ikumbukwe uongozi wake Spika Ndugai umewahi kuwafukuza wabunge 8 wa chama cha upinzani cha CUF waliodaiwa kufukuzwa uanachama na Profesa Ibrahim Lipumba katikati ya mgogoro uliokikumba chama hicho, lakini alikataa kuitambua barua ya aliyekuwa Katibu wa CUF Maalim Seif Hamad ya kuwafuta uanachama Wabunge Magdalena Sakaya na Maftah Nachuma.

Pili, uamuzi wa kuwalinda Wabunge 19 waliofutiwa uanachama Chadema. Spika alituhumiwa kuvunja Katiba ya Tanzania ibara ya 67(1)(b) ambayo inafafanua mtu anayestahili kuwa Mbunge ni lazima awe mwanachama na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa. Kwamba Spika aliwaapisha Wabunge wa viti maalumu 19 pasipo matakwa ya Chadema, na sheria ya uchaguzi inavitaka vyama vinavyoshiriki uchaguzi wa rais,wabunge na madiwani kuwasilisha kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi orodha ya majina ya wanachama wake wanaopendekezwa kwenye viti maalumu. Aghalabu Chadema kupitia Katibu mkuu wake John Mnayika kimekuwa kikieleza hakijawahi kupeleka majina hayo NEC.
Tatu, sakata la kuvuliwa ubunge Tundu Lissu. Ikumbukwe Septemba 7 mwaka 2017 aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alishambuliwa kwa risasi nyumbani kwake jijini Dodoma na watu wasiojulikana.
Tukio hilo lilitokea wakati ambao Lissu akitoka kuhuhuduria vikao bungeni, lakini licha ya kupelekwa jijini Nairobi kwa matibabu zaidi kisha Brussels nchini Ubelgiji, Spika huyo wakati akichukua uamuzi huo uliokuwa kwenye mamlaka yake alibainisha kuwa hajui alipokuwa Mbunge huyo, na siku chache baadaye ukaibuka mgogoro wa stahiki alizostahili kupewa Lissu.

Chanzo cha picha, Bunge
Tatu, kuwaadhibu pakubwa wabunge wa upinzani hali ambayo ilisababisha malalamiko dhidi ya Kiti cha Spika kwa kile kinachoitwa uvunjaji wa sheria na matumizi ya nguvu dhidi wawakilishi hao.
Reginald Kwizela Ndindagi, mgombea ubunge Jimbo la Magu mkoani Mwanza kwa tiketi ya Chadema mwaka 2020 amemwambia mwandishi wa makala haya kuwa licha ya Spika kuombwa kufuata sheria na kupunguza dhuluma dhidi ya vyama vya upinzani bado hapakuwa na mabadiliko yoyote.
"Spika aliyeondoka amewahi kutoa adhabu zisizo na msingi kwa wabunge wa upinzani. Aliwafungia kuingia bungeni kwa muda mrefu, mfano Zitto Kabwe,Ester Bulaya na Halima Mdee na hata kumfuta ubunge Tundu Lissu wakati akifahamu fika kuwa Lissu alikuwa mgonjwa. Haya na mambo mengi yanatufundisha kuwa ukitenda dhuluma, mwisho wako hautakuwa mzuri. Kwa nyakati fulani, wakati anayetenda hayo alipokea sifa na utukufu mwingi kutoka kwa wanachama na viongozi wenzake. Lakini sote ni mashahidi kuwa walioshinikiza aachie ngazi ni walewale. waliompongeza wakati akitenda dhuluma,"
Nne, Spika alionekana kufurahishwa na kampeni ya 'Magufuli baki' ambapo mara kadhaa alikaririwa akisema lilikuwa jambo muhimu kwa marehemu John Magufuli kubaki madarakani hata kama hakuwa na mpango huo.
Septemba 2017 aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Chemba mkoani Dodoma (CCM), Juma Nkamia aliwasilisha ajenda ya kuongezwa muda wa muhula wa ubunge na urais kutoka miaka mitano hadi saba.
Pia kampeni ya 'Magufuli baki' ilianzishwa na Lawrence Mabawa. Mwanasiasa huyo amewahi kuomba kuteuliwa kugombea ubunge ndani ya CCM mwaka 2015. Sauti ya Spika katika jambo hili ilisababisha msuguano mwingine na vyama vya upinzani ambavyo vinaamini iliporomosha heshima ya Bunge na wabunge. Hayo ni matukio machache kati ya mengi yalikarahisha wapinzani.
Je kwanini upinzani wanapigania Katiba mpya?

Chanzo cha picha, Ikulu
Ingekuwa mwaka 2020 kisha Spika Ndugai angeliambiwa kuwa hatafika mwaka 2025 akiwa na cheo hicho hakuna ambaye angekubali wala mwenyewe asingeafiki, lakini hivi sasa Spika huyo ameng'atuka katika wadhifa huo na kuibua zaidi mjadala wa Katiba mpya na kutolewa tafsiri tofauti juu ya kiini cha kufikia hatua hiyo kwa maslahi ya taifa.
"Ndugai hakuwa na kosa kuikosoa serikali ya Rais Samia kwa mambo makubwa matatu; kwanza ni jukumu lake si tu kama Mbunge, bali kama kiongozi mkuu wa mhimili huo kuikosoa serikali kwa mambo ambayo yanafanywa, ambayo anadhani kungekuwa na mtizamo mpya.
Lakini pili, yeye kama msimamizi wa serikali, anawajibu wa kuikumbusha serikali juu ya namna bora ya uwajibikaji na utendaji, ikiwa pamoja na kukosoa utekelezaji wa sera. Jambo lingine katika hili ni mwakilishi wa wananchi, hivyo ana fursa ya kuwasemea wananchi." Ameongeza Reginald Kwizela Ndindagi.
Unaweza pia kusoma:
Kwa upande mwingine mgongano wa mihimili ya dola, yaani Rais Samia na aliyekuwa Spika Job Ndugai umeonesha bayana namna gani Watanzania wanatakiwa kuhakikisha kampeni za mahitaji ya katiba mpya inaendelezwa. Kwa mujibu wa Katiba ya sasa Spika anatakiwa kuwa mtii kwa serikali.
"Hili ni tishio kwa uhuru wa Bunge pamoja na kwamba Spika Ndugai hakuwa anafaa kuwa na cheo hicho lakini uhuru wa Bunge unapaswa kulindwa na jambo la ajabu wabunge wote wamekaa kimya, tatizo wote wanatokana na CCM. Wananchi watuelewe jinsi tunavyohangaika na hili dude la katiba mpya ni pamoja na kuondosha mambo kama haya. Bunge linatakiwa kuwa huru.
Mkuu wa mhimili mmoja anajiuzulu kwa kutoa mawazo kinzani na mkuu wa serikali, hii inathibitisha namna gani mihimili yetu iko chini ya usimamizi wa rais. Tukio hili litukumbushe kuongeza kelele za Katiba mpya, vyama vya upinzani na wananchi wamepewa ushahidi wa wazi."
Sakata hili ni kielelezo kizuri cha sera na miongozo mibovu ya namna ya kuandaa na kukuza viongozi. Kwamba ni muhimu Tanzania kuimarisha njia zake za upatikanaji wa viongozi bora. Pamoja na hayo suala la ulevi wa madaraka ni jambo ambalo linapaswa kuwa somo kubwa viongozi,wanasiasa na wananchi ikizingatiwa Ndugai amekuwa mbunge kwa takribani miaka 25 mfululizo. Hivyo kukaa muda mrefu katika nafasi ya ubunge kumemtengenezea dhana ya umiliki wa madaraka ambayo ni dhamana tu.












