Wafahamu watu mashuhuri waliofariki Afrika 2021

Chanzo cha picha, Various
Wakati mwaka 2021 unaelekea ukingoni tunakumbuka vifo vya waanzilishi, wenye ushawishi mkubwa na utata waliofariki mwaka huu.
Hawa ni miongoni viongozi 10 ambao tuliwaaga

1.BABA WA TAIFA Kenneth Kaunda, 97
Kiongozi wa uhuru wa Zambia, ambaye alifariki mwezi Juni, alikuwa mmoja wa viongozi wa mwisho wa kizazi cha Afrika ambao walipigana na ukoloni.

Chanzo cha picha, Getty Images
Alisema ndoto yake ni kuona Wazambia wana maisha mazuri ikiwemo kila Mzambia kumiliki jozi ya viatu.
Maarufu kwa jina la KK, alipenda sana kupiga gitaa na alikuwa mwalimu wa shule kabla ya kujiunga na mapambano ya uhuru na kuwa mfuasi mkubwa wa juhudi za kukomesha ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, pia aliunga mkono harakati za ukombozi nchini Msumbiji na nchi ambayo sasa ni Zimbabwe.
Pia tuliwapoteza: Sultan El-Hadj Ibrahim wa Cameroon, Mbombo Njoya, mfalme wa Wapedi wa Afrika Kusini, Victor Thulare III na Kefa Sagbadjou Glele, mfalme wa ufalme wa Abomey wa Benin.
2.MUHUBIRI MAARUFU TB Joshua, 57
Chapisho kwenye ukurasa wa Facebook wa mchungaji wa Nigeria mwezi Juni lilisema tu: "Mungu amemchukua mtumishi wake". Ilianzisha wimbi la maombolezo kati ya mamilioni ya wafuasi wa Kanisa lake ulimwenguni kote.

Chanzo cha picha, AFP
Mhubiri huyo mashuhuri, ambaye baadhi ya wanasiasa wakubwa ni miongoni mwa waumini wake, alifahamika kwa "miujiza" yake na alidai kuponya magonjwa ya kila aina ikiwa ni pamoja na HIV.Fahamu utabiri na utata uliomzunguka TB Joshua
Pia tulimpoteza: Kadinali Christian Tumi wa Cameroon, ambaye kifo chake kiliunganisha taifa hilo lenye migogoro kupitia maombelezo. Alexandre José Maria dos Santos, kasisi na kadinali wa kwanza mweusi wa Msumbiji, msomi mashuhuri wa Kiislamu wa Tunisia Hichem Djait na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Sudan Kusini Paulino Lukudu Loro.
Pia tumewapoteza Profesa wa Nigeria na mtafiti wa masuala ya virusi
David Olufemi Olaleye na John Baptist Mukasa, moja Kati ya madaktari wachache wa upasuaji wa Neva ambaye alijitolea kuelimisha Kizazi kijacho cha madaktari.
3. Rais John Magufuli, 61
Kifo cha rais huyo wa Tanzania kilitangazwa mwezi Machi baada ya kutoonekana hadharani kwa zaidi ya wiki mbili.

Chanzo cha picha, AFP
Serikali ilisema alifariki kutokana na shida za moyo, lakini wanasiasa wengine wa upinzani walidai alikuwa ameambukizwa Covid-19.
Mtoto wa mkulima mdogo, aliibuka na kuwa rais mwaka 2015 na akasifiwa kwa mtazamo wake huo.
Anayejulikana kama The Bulldozer, wakosoaji walimshtumu kwa kuwa mtu wa mabavu ambaye alijaribu kubana uhuru wa waandishi wa habari, kutishia upinzani na kusababisha maelfu ya vifo kwa kudhoofisha mapambano dhidi ya virusi vya corona.
Pia tuliwapoteza: Rais wa Chad Idriss Déby, ambaye aliuawa kwenye uwanja wa vita, na Waziri Mkuu wa Ivory Coast Hamed Bakayoko, ambaye alikuwa na saratani.
Marais wa zamani kutoka Algeria - Abdelaziz Bouteflika, Madagascar - Didier Ratsiraka, Somalia - Ali Mahdi Mohamed na Chad - Hissène Habré, pia walifariki.
Makamu wa Rais wa Zanzibar Seif Sharif Hamad, Waziri wa Mambo ya Nje wa Zimbabwe Sibusiso Moyo na Waziri wa Uchukuzi Joel Biggie Matiza wote walifariki dunia baada ya kuambukizwa Covid-19.
4. Mshindi wa Tuzo ya Nobel Desmond Tutu
Alizaliwa kipindi cha ubaguzi wa rangi Afrika Kusini. Alijiunga na Kanisa la Anglican na kuwa Askofu Mkuu wa Kwanza Mweusi katika mji wa Cape Town mwaka 1986, miaka miwili baadae alitunukiwa tuzo ya Amani ya Nobel kwa kazi yake ya kupambana kumaliza utawala wa wazungu.

Chanzo cha picha, Getty Images
Alijulikana kwa upendo, alikuwa mwenyekiti wa Tume ya Maridhiano ya nchi hiyo baada ya Nelson Mandela kushinda uchaguzi wa kwanza ulio huru na wa haki mwaka 1994 akichukuliwa Kama kiongozi wa maadili Afrika Kusini, Tutu wakati fulani pia alikuwa mkosoaji mkubwa wa serikali iliyofuata juu ya ubaguzi wa rangi
Pia tulimpoteza: FW de Klerk, rais wa mwisho wa ubaguzi wa rangi wa Afrika Kusini, ambaye alishiriki Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 1993.
5. MWANARIADHA Agnes Tirop, 25
Wanariadha wa Kenya walipatwa na mshtuko baada ya kujua kwamba rafiki yao na anayeshikilia rekodi ya dunia aliuawa kwa kuchomwa kisu mwezi Oktoba.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mumewe, Ibrahim Rotich, amekana mashtaka ya mauaji yake. Tirop alikuwa mkimbiaji wa mbio ndefu ambaye alivunja rekodi ya dunia ya kilomita 10 mwezi Septemba na pia alionekana kwenye Michezo ya Olimpiki ya Tokyo.
Pia tuliwapoteza : Mwendesha baiskeli wa Eritrea Desiet Kidane, aliyefariki baada ya kugongwa na gari alipokuwa kwenye mazoezi, kutoka Senegal aliyekuwa mkuu wa shirikisho la riadha duniani Lamine Diack, Mwanasoka wa Afrika Kusini Ryder Mofokeng ambaye alikuwa nahodha wa Kaizer Chiefs kwa miaka 11 na mchezaji kandanda wa Nigeria Yisa Sofoluwe.
6.Sarah Obama, 99
Mama Sarah, kama alivyojulikana, alipata umaarufu duniani wakati mjukuu wake wa kambo Barack Obama alipokuwa rais wa Marekani mwaka wa 2009, lakini tayari alikuwa anajulikana sana nyumbani kwao magharibi mwa Kenya ambako alikuwa ameolewa na mwanamume mzee zaidi alipokuwa kijana.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa miongo kadhaa, aliendesha taasisi ya kusaidia kusomesha watoto yatima na wasichana, jambo ambalo alilifanya kwa nguvu kwani yeye hakuweza kujisomea. Mwaka 2014 alipata tuzo ya muanzilishi wa elimu ya UN kwa kazi yake.
Barack Obama alisema kujitolea kwake katika elimu kulianza na watoto wake,"Ingawa sio mama yake mzazi, Bibi aliweza kumlea baba yangu kama mtoto wake, na ilikuwa ni shukrani kwa upendo wake na kutiwa moyo kwamba aliweza kupinga tabia mbaya na kufanya vizuri kwa kupata ufadhili wa kuhudhuria chuo kikuu cha Marekani."
7.MFALME Goodwill Zwelithini, 72
Kiongozi wa jamii ya Wazulu nchini Afrika Kusini, alikuwa mtetezi mkubwa wa kulinda utambulisho wa kitamaduni katika kipindi chote cha utawala wake wa miaka 50.

Chanzo cha picha, AFP
Alitokana na kizazi cha Mfalme Cetshwayo, ambaye aliwaongoza Wazulu katika vita na jeshi la Uingereza mwaka wa 1879.
Ingawa baba huyu wa watoto 28 kutoka na wake sita hakuwa na mamlaka rasmi ya kisiasa, aliwasilisha wazo kwamba licha ya Afrika Kusini kuwa ya kisasa haija acha asili yake.
Mmoja wa wake zake, Malkia Mantfombi Dlamini-Zulu, alichukua nafasi hiyo mwezi Machi, lakini alifariki mwezi mmoja baadaye.
8. MCHEKESHAJI Soheir El-Bably, 86
Taaluma ya mwigizaji huyo wa Kimisri iliyodumu kwa miaka 50 ilimwezesha kushiki kwenye filamu, uchekeshaji jukwaani na katika televisheni. Alicheza majukumu makubwa lakini labda alijulikana zaidi na kupendwa kwa ustadi wake wa kuchekesha.

Chanzo cha picha, AFP
Alipata mafanikio makubwa kwenye televisheni akicheza nafasi za uongozi katika baadhi ya mfululizo maarufu ambao ni msingi wa maisha ya familia kila Ramadhani.
Pia tuliwapoteza: Mchekeshaji wa Kisomali Ibrahim Ismail, anayejulikana zaidi kwa jina lake la utani la Soran na mwigizaji na mchekeshaji mwingine wa Kisomali Abdi Muridi Dhere, Mmoja wa wachekeshaji maarufu zaidi wa Nigeria Baba Suwe pia aliaga dunia.
9.Daktari wa upasuaji Matolase Mtonga, 34
Mmoja wa madaktari wachache wa upasuaji wa kurekebisha sehemu za mwili wa Zambia, Mtonga alipata wito wa kazi hiyo wakati akiwahudumia wagonjwa walioungua kama mwanafunzi wa udaktari.

Chanzo cha picha, ReSurge
Mtonga alifariki mwezi Desemba muda mfupi baada ya kurudi kutoka Katika mkutano wa upasuaji wa kurekebisha sehemu za mwili nchini Marekani.
Moja ya ujumbe wa pole iliandikwa kupitia Facebook kutoka kwa mtu ambaye mke wake alitibiwa na Mtonga miaka michache iliyopita: "Dr Mtonga alikwenda mbali zaidi na kutumia fedha zake kununua kile kilichohitajika kutumia kwenye matibabu ya mke wangu ili kuhakikisha kuwa mkono wa mke wangu wa kulia na vidole vinapona.
10.Mwanamuziki Alemayehu Eshete, 80
Anajulikana Kama Elvis wa Ethiopia,
Alemayehu alikua mwanamuziki mashuhuri katika tasnia ya muziki wa aina ya jazz ya Ethiopia kuanzia miaka ya 1960 na amekuwa akiimba hadi miaka yake ya mwisho. Tangu siku zake za ujana, alijulikana kwa kuimba nyimbo za Elvis Presley na aliwahi kuliambia gazeti la the Guardian mwaka 2008 kwamba James Brown ndie alikuwa mshawishi wale mkubwa

Chanzo cha picha, Getty Images
''Nilivaa kama Mmarekani, nikakuza nywele zangu, nikaimba Jailhouse Rock na Teddy Bear, wakati mwingine tulifanya "Strangers in the Night". Lakini wakati nilipoanza kuimba nyimbo za Kiamhari umaarufu wangu uliongezeka," alisema.
Pia tuliwapoteza: Mwimbaji wa Afrika Kusini Sibongile Khumalo, ambaye mtindo wake ulianzia na uimbaji wa opera hadi jazz hadi nyimbo za kitamaduni; mwimbaji wa jazz wa Afrika Kusini Jonas Gwangwa, msanii wa nyimbo za injili na jazz kutoka Malawi Wambali Mkandawire, mmoja wa waimbaji maarufu wa Senegal Thione Seck, mwimbaji wa Cameroon Wes Madiko na Rapa wa Rwanda Jay Polly, ambaye alikuwa amezuiliwa kwa tuhuma za dawa za kulevya pia mwanzilishi kwenye tasnia ya hip-hop ya Namibia Kanibal na mmoja wa waimbaji wanaopendwa zaidi wa Algeria Rabah Deriassa












