Apple yafuta app ya Quran China

Chanzo cha picha, Getty Images
Apple imefuta moja ya program tumishi maarufu ya Quran duniani kutoka kwa mtandao wake nchini China. Kampuni hiyo imechukua hatua hiyo kufuatia ombi kutoka kwa maafisa wa China.
App ya Quran Majeed inapatikana kote duniani kupitia Apple Store. Karibu watu 150,000 walishirikisha maoni yao kupitia njia ya maoni. App hiyo pia inatumiwa na mamilioni ya waumini wa Kiislam duniani.
BBC inafahamu kuwa app hiyo iliondolewa baada ya kushirikisha maudhui ya ambayo yanaenda kinyume na sheria.
Serikali ya China haijatoa tamko lolote kuhusiana na hatua hiyo licha ya ombi la BBC la kupata kauli yao.
Kufutwa kwa app hiyo kuligunduliwa mara ya kwanza na Apple Censorship - tovuti ambayo inafuatilia progamu zote zilizopo kwenye Apple App duniani.
Katika taarifa kutoka kwa waundaji wa app ya, PDMS, kampuni hiyo ilisema "Kulingana na Apple, app yetu ya Quran Majeed imefutwa kutoka kwa App store ya China App kwa sababu inajumuisha maudhui ya ziada ambayo yanahitaji kuidhinishwa na mamlaka za China".
"Tunajaribu kuwasiliana na wasimamizi wa mitandao wa China na mamlaka zingine husika kusuluhisha suala hili".
Kampuni hiyo imesema ina wafuatiliaji karibu milioni moja ambao wanatumia huduma yao nchini China.
Chama tawala nchini China kinatambua rasmi dini ya Kiislamu.
Hata hivyo, China imetuhumiwa kwa kukiuka haki ya jamii ya Waislamu wa Uyghur wanaoishi Xinjiang.
Mapema mwaka huu BBC iliripoti kuwa maimamu wa Uighur walikuwa wakilengwa katika msako wa mamlaka za China katika eneo la Xinjiang.
Apple imekataa kutoa tamko,lakini imeelekeza BBC kwa sera zake juu ya Haki za Binadamu ambazo zinasema: "Tunatakiwa kutii sheria za nchi husika, na wakati mwingine kuna maswala magumu ambayo tunaweza kutokubaliana na serikali."

Hata hivyo, haijulikani ni sheria gani ambazo programu hiyo imevunja nchini China. Quran Majeed inasema "inaaminiwa na zaidi ya Waislamu milioni 35 duniani".
Mwezi uliopita, Apple na Google zilifuta app ya kupiga kura ilibuniwa na koingozi wa upinzani wa Urusi aliyefungwa Alexei Navalny.
Mamlaka nchini Urusi zilikua zimetishia kupiga faini kampuni hizo mbili ikiwa hazitafuta app hiyo ambayo iliwapa wapiga kura maelezo ya ni kina nani watawaondoa kitini wagombea wa chama tawala.
China ni moja ya soko kuu ya Apple, na ugavi wa kampuni hiyo unategemea sana utengenezaji wa Wachina.
Afisa mkuu mtendaji wa Apple, Tim Cook ameshtumiwa kwa unafiki na wanasiasa wa Marekani kwa kuangazia juu ya siasa za Marekani, na kufumbia macho juu ya siasa za China.
Bwana Cook alimshtumu Donald Trump kwa kupiga marufuku wasafiri kutoka nchi saba za Kiislamu mwaka 2017.













