Agnes Tirop:Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta awaagiza polisi kuchunguza mauaji ya mwanariadha wa olimpiki

Muda wa kusoma: Dakika 3

Rais Uhuru Kenyatta amejiunga na tasnia ya riadha nchini Kenya katika kumuomboleza Mwanariadha wa Olimpiki Agnes Jebet Tirop ambaye alikutwa amekufa nyumbani kwake katika mji wa Iten, Kaunti ya Elgeyo Marakwet Jumatano.

Agnes Tirop, mwenye umri wa miaka 25, alikuwa katika kikosi cha wanamichzo wa Kenya walioshinda mashindano ya Olimpiki ya Tokyo ya mwaka 2020 ambayo yalicheleweshwa ambapo aliiwakilisha nchi katika mbio za mita 5,000 na kumaliza katika nafasi ya 4 kwenye fainali.

Katika ujumbe kuifariji familia, marafiki, jamaa, na wadau katika mchezo wa riadha, Rais alimumboleza Agnes kama shujaa na bingwa wa Kenya ambaye kifo chake ni pigo kubwa kwa matamanio ya michezo na hadhi ya nchi.

"Inasikitisha, ni bahati mbaya kabisa na na jambo la huzuni kwamba tumepoteza mwanariadha mchanga na aliyeiletea nchi fahari akiwa na umri mdogo wa miaka 25, kupitia ushujaa wake katika riadha ya ulimwengu ikiwa ni pamoja na katika mashindano ya Olimpiki mwaka huu ya Tokyo ambapo alikuwa sehemu ya timu ya Kenya huko Japan, "Rais alisema

"Kinachosikitisha zaidi ni kwamba Agnes, shujaa wa Kenya, alipoteza maisha yake ya ujana kwa njia ya kitendo cha uhalifu kilichotekelezwa na watu wenye ubinafsi na waoga," Rais alisema, na kuamuru polisi kuharakisha msako dhidiya waliotekeleza mauaji yake .

"Ninasihi vyombo vyetu vya kutekeleza sheria vinavyoongozwa na Huduma ya Kitaifa ya Polisi wafuatilie na kuwakamata wahalifu waliohusika na mauaji ya Agnes ili waweze kukabiliwa na nguvu kamili ya sheria," alisema rais Uhuru .

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya nchini humo mwili wa Agnes, mshindi wa medali ya shaba ya Dunia katika mbio za 5000m na bingwa mwandamizi wa mbio za nyika mwaka wa 2015, ulipatikana katika nyumba yake huko Iten na majeraha ya kuchomwa na kisu .

Polisi kupitia ujumbe waliotuma katika twitter walihakikishia umma kwamba wataharakisha katika uchunguzi wa 'kina' kuhusu uhalifu huo .Ujumbe huo wa tume ya huduma kwa polisi pia ulituma risala za rambi rambi kwa familia ,marafiki na tasnia ya spoti nchini .

Mume ni 'mshukiwa'

Uchunguzi wa jinai sasa unaendelea juu ya kifo chake, na polisi wanasema mumewe ametoweka.

Siku ya Jumatano, wachunguzi wa eneo la uhalifu walikuwa nyumbani kwa Tirop, ambaye polisi wanasema aliripotiwa kupotea na baba yake Jumanne usiku.

"[Polisi] walipoingia nyumbani, walimkuta Tirop kwenye kitanda na kulikuwa na damu sakafuni," Tom Makori, mkuu wa polisi wa eneo hilo, alisema.

"Waliona alikuwa amechomwa kisu shingoni, jambo lililotupelekea kuamini ni jeraha la kisu, na tunaamini kwamba ndicho kilichosababisha kifo chake.

"Mumewe bado hajulikani aliko , na uchunguzi wa awali unatuambia kuwa mumewe ni mshukiwa kwa sababu hawezi kupatikana. Polisi wanajaribu kumtafuta mumewe ili aweze kuelezea kilichomsibu Tirop."

Makori ameongeza kuwa polisi wanaamini kuwa CCTV katika nyumba hiyo inaweza kusaidia uchunguzi wao.

Tirop pia alikutwa na jeraha la kuchomwa tumboni mwake, vyanzo vimeiambia BBC.

Mafaniko katika Riadha

"Athletics Kenya imefadhaika leo mchana kujua kuhusu kifo cha mshindi wa medali ya shaba ya Dunia 10,000 Agnes Tirop," shirikisho la riadha nchini limesema katika taarifa.

"Bado tunajitahidi kupata maelezo zaidi juu ya kifo chake. Kenya imepoteza kito ambaye alikuwa mmoja wa vigogo wa riadha wanaokua kwa kasi zaidi katika hatua ya kimataifa, kutokana na maonyesho yake ya kuvutia kwenye tasnia hiyo huo."

Mwezi uliopita, Tirop aliweka rekodi ya ulimwengu kwa mbio za kilomita 10 za wanawake huko Ujerumani.

Kwenye Michezo ya Olimpiki ya 2020 mnamo Agosti, Tirop alimaliza nje kidogo ya nafasi za medali kwa wanawake katika mbio za 5,000m, akifuata mshindi wa medali ya shaba wa Ethiopia Gudaf Tsegay kwa sekunde 0.75.

Pamoja na medali zake za shaba katika 10,000m kwenye Mashindano ya Dunia ya Riadha ya 2017 na 2019, Tirop pia ilivutia nje ya uwanja .

Mnamo Septemba, aliweka muda wa dakika 30 na sekunde moja huko Herzogenaurach, Ujerumani, alipoondoa sekunde 28 kutoka kwa rekodi ya zamani ya mbio za 10km za barabarani iliyowekwa mnamo 2002.

Tirop alianza taaluma yake kama mwanariadha chipukizi mnamo 2011, akishinda medali mbili za shaba katika mita 5,000 katika mashindano ya ulimwengu ya mwaka huo kwa vijana .

Miaka minne baadaye, alishinda mashindano ya nyika Duniani nchini China - kuwa mshindi wa pili mchanga zaidi kwa kiwango hicho.

Katika taarifa yake, Athletics Kenya ilitakia "nguvu familia ya [Tirop] na marafiki wakati huu mgumu".