Korea Kaskazin: Kim Jong-un aapa kujenga 'jeshi lisiloonekana'

TH

Chanzo cha picha, Reuters

Kiongozi wa Korea Kaskazini ameapa kujenga "jeshi lisiloonekana" kukabiliana na sera za uadui kutoka Marekani, kulingana na vyombo vya habari vya taifa hilo.

Kim Jong-un aliongeza kuwa utengenezaji wa silaha ni kwa ajili ya kujilinda , na sio kuanza vita.

Bw Kim ametoa kauli hizo katika onyesho la nadra la ulinzi huku aliwa amezingirwa na aina mbali mbali za makombora ya masafa.

Korea Kaskazini hivi karibuni ilifanya majaribio ya kile inachodai ni kombora jipya la kisasa la kuzuwia mashambulio ya makombora ya masafa yanayorushwa kutoka kwa ndege.

Wakati huo huo Korea Kusini ilifanya majaribio ya silaha za ufyatuaji wa makombora kutoka majini.

TH

Chanzo cha picha, KCNA

Katika hotuba yake aliyoitoa katika onyesho la kujilinda la 2021 lililofanyika Pyongyang, ambapo zana za kijeshi vikiwemo vifaru na nyingine za kufyatua makombora vilionyeshwa, Bw Kim alielezea kujengwa kwa uwezo wa kijeshi katika Korea Kusini na akasema Korea Kaskazini haitaki vita na jirani yake.

"Hatujadili vita na yeyote, bali tunazuwia vita na kuongeza zana zinazozuwia vita kwa kulinda taifa letu," alisema.

Bw Kim pia alishutumu Marekani kwa kuchochea wasi wasi kati ya Korea Kaskazini na Korea Kusini.

Aliongeza kuwa hakuna "msingi wa kitabia" wa kuifanya Korea Kaskazini iamini kwamba Marekani sio adui wake.

Rais wa Marekani Joe Biden amerudia kusema kuwa Marekani iko tayari kufanya mazungumzo na Korea Kaskazini, lakini ameitaka Pyongyang kuachana silaha za nyuklia kabla ya kulegezwa kwa vikwazo dhidi yake. Korea Kaskazini imekataa hilo kwa sasa.

Korea Kaskazini imepigwa marufuku ya kufanya majaribio ya makombora ya Ballistic na silaha za nyuklia na Umoja wa Mataifa. Imekuwa mara kwa mara ikikiuka marufuku hizi na matokepo yake imewekewa vikwazo vikali.

Mwezi uliopita, shirika la Umoja wa Mataifa la udhibiti wa nishati ya Atomiki lilisema kuwa Korea Kaskazini inaonekana kuwa ilianza mchakato wa kutengeneza madini ya plutonium kwa ajili ya kutengeneza silaha za nyuklia na kukiita kitendo hicho "cha kusumbua sana "

Korea Kaskazini kila mara imekuwa ikisema kuwa inahitaji kuendelea kutengeneza silaha za nyuklia kwa ajili ya ulinzi.

Lakini waangalizi wanasema pia inatumika kama njia ya kuliunganisha taifa hilo masikini. Korea Kaskazini inadhaniwa kuwa kuwa na matatizo ya kiuchumi baada ya maafisa kufunga mipaka yake ili kuzuwia usambaaji wa Covid-19.

Usambazaji wa bidhaa muhimu kama chakula na mafuta kutoka Uchina ambayo ni mshirika wake mkuu wa kisiasa na kiuchumi umezuiwa.