Krimu za kuchubua ngozi: Baba 'ashindwa kumtambua binti yake' aliyejichubua

Grazia

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Grazia, kutoka Bradford, West Yorkshire, alikuwa na miaka 18 alipoanza kutumia krimu hizo

Mwanamke ambaye alikuwa anatumia krimu za kujichubua au kujibadilisha rangi ya mwili kwa zaidi ya miaka 10 amesema kuwa ngozi yake ilibadilika sana kiasi kwamba baba yake hakuweza kumtambua.

Grazia, kutoka Bradford, West Yorkshire, alikuwa na miaka 18 alipoanza kutumia krimu hizo na kuufanya kama mtindo wake wa kila siku kabla ya kuamua kuacha mwaka jana.

"Alilishutuka sana aliponiona kwasababu nilikuwa nimekuwa mweupe kweli," amesema.

Uchunguzi uliofanywa na BBC umebaini kuwa krimu alizokuwa akitumia zinapatikana katika maduka ya kuuza bidhaa za urembo wala hakuitaji barua ya daktari.

Krimu alizokuwa anatumia zilikuwa na kiwango cha juu cha steroidi ambazo hutumika kwa muda mfupi wakati wa mtu ana tatizo fulani la ngozi kama vile ugonjwa wa 'eczema' yaani ukurutu. Wizara ya Afya Uingereza hupendekeza wagonjwa kutumia krimu hiyo kwa wiki moja tu.

Athari za krimu za aina hiyo ni kwamba zinaweza kuchubua ngozi ila baadhi ya watu wanazitumia wakiamini kwamba ni bidhaa za urembo.

Madaktari wa ngozi wameonya kwamba kutumia krimu za aina hiyo kwa kipindi kirefu bila usimamizi wa daktari kunaweza kusababisha madhara ya ngozi.

'Kweli huyu ni wewe?'

Grazia, ambaye sasa hivi ana miaka 29, alihama kutoka Italia hadi Bradford miaka minane iliyopita alipoendelea kutumia bidhaa zenye kemikali ya clobetasol.

Kwasababu alikuwa anaishi ughaibuni, alikuwa akikaa muda mrefu bila kwenda kumuona baba yake.

"Baba yangu aliniambia kwamba hanitambui kwasababu hatujaonana kwa miaka miwili," Grazia amesema.

"Alikatishwa tamaa, alihuzunika na kuniomba niache kuzitumia."

Alikuwa "na ngozi nyingine tofauti kabisa" alipoanza kutumia krimu hizo akiwa na miaka 18, alisema.

"Nilikuwa nikifikira kwamba mimi sipendezi," aliongeza.

"Inanikasirisha kwasababu nimetumia krimu hii kwa kipindi kirefu. Nafikiri kuanza kujipenda ni mchakato wala sio kitu cha siku moja."

Dkt. Walayat Hussain, mtaalam wa magonjwa ya ngozi, alikubali kumuona Grazia ili aweze kutathmini athari za utumiaji wa krimu za steroidi kwa muda mrefu.

Alipoona picha akiwa na miaka 18 na jinsi ngozi yake halisi ilivyokuwa, Dkt. Hussain aliiangalia tena na tena na kumuuliza: "Hi kweli ni picha yako?"

Maelezo ya video, Jahalia Ngonde: Najuta kujichubua ngozi yangu nzuri ya Kitanzania

Wanahabari wa taarifa za kiuchunguzi walifanikiwa kununua krimu hizo katika maduka sita kati ya saba ya kuuza bidhaa za urembo kote eneo la Yorkshire. Katika duka la saba, krimu hiyo ilikuwa imeisha ikawa haipatikani.

Dkt. Hussain alisema kwamba "inatia wasiwasi" kuona kuwa krimu hizo zinauzwa kiholela tu madukani.

"Hizi ni krimu ambazo zinatakiwa kununuliwa kwa karatasi ya daktari pekee kama matibabu," alisema.

"Haustahili kuwa unaweza tu kwenda dukani na kununua dawa hizo unapotaka wewe kwasababu zinaweza kuwa na madhara makubwa kwa mgonjwa."

Krimu za kubadilisha ngozi ndizo zenye "kiwango kikubwa cha kemikali ya steroidi", amesema, hasa za ugonjwa wa eczema.

"Kwahiyo, fikiria iwapo utazitumia bila uelewa wa madhara yake kwa ngozi yako," alisema.

"Mtumiaji wa kawaida hawezi kuelewa madhara ya kemikali ya clobetasol propionate ni nini. Wanaweza kufikiria kwamba zinauzwa kama krimu za kubadilisha ngozi ya rangi, bila kujua kwamba ni dawa zilizochanganywa kwa kemikali kali ya steroidi inayoweza kusababisha matatizo ya muda mrefu."

Hata hivyo, uchunguzi umeonesha kwamba ni vigumu kubaini zinatumiwa kwa wingi kiasi gani kwasababu watu huwa hawakubali moja kwa moja kwamba wanatumia krimu za kubadilisha ngozi.

'Kuwa mzuri

Binti Asumani alihamia Ungereza kutoka Tanzania mwaka 2013 akiwa na mume wake na mtoto wake. Miaka miwili baadaye, alianza kutumia krimu za kubadilisha rangi ya ngozi yake.

Anasema: "Nilitaka kujibadilisha rangi kwasababu niliona rafiki zangu wote wakiwa weupe na nikajiangalia na kujiambia: 'Kwanini na mimi nisiwe mzuri?'"

Binti Asumani akaanza kuulizia ili aweze kuelekezwa bidhaa za urembo zinapatikana wapi na rafiki zake wakamuelekeza katika soko la eneo, alikoweza kupata krimu zenye kemikali kali za kubadilisha rangi ya ngozi.

Lakini baada ya kuzitumia kwa miaka miwili, athari zake hazikuwa nzuri.

"Nilianza kuwa na madoa doa kwenye uso wangu na macho yangu yalianza kutoa machozi kila nilipofungua kopo lenye krimu," amesema.

Baada ya kwenda kwa mtaalamu na kumuonesha krimu hiyo, Bi. Asumani akashauriwa kuacha kuitumia mara moja. Anasema kwamba haikuwa rahisi kwake na ngozi yake ikawa imeanza kuathirika.

"Kuwa mweupe, kuwa mzuri, inachukua muda lakini kuacha haichukui muda. Nikarejelea ngozi yangu ya kawaida katika kipindi cha miezi miwili," anasema.

"Nilihisi vibaya, nilikuwa tu niko ndani kwa kipindi cha miezi miwili sitaki hata kutoka kwasababu nilikuwa mweusi zaidi ya nilivyokuwa awali."

Anasema, ni matumaini yake kwamba mambo yatabadilika kabla ya binti yake kuanza kuhisi kuwa naye anastahili kufanya kama hivyo.

"Kuna haja gani ya kuendelea kudhuru uzuri wako?," anasema. "Ni matumaini yangu kwamba binti yangu ataelewa kuwa nimepitia madhara fulani baada ya kutumia krimu ya kubadilisha rangi ya ngozi."

Presentational grey line

Utumiaji mbaya wa krimu yenye kemikali ya Corticosteroid na athari zinazoweza kutokea

  • Ngozi inakuwa nyembamba sana - ngozi inaweza kuwa kama karatasi nyepesi
  • Matatizo ya kuona - inaongeza hatari ya kupata ugonjwa wa macho wa 'cataract na glaucoma'
  • Ngozi inakuwa katika hatari ya kuchubuka na kuharibika
  • Ngozi itakuwa na mabaka mabaka ya kutisha
  • Ngozi inakuwa na michirizi