Urembo wao uliwahadaa wengi Marekani,kumbe walidaiwa kuwa majasusi wa Moscow

Chanzo cha picha, FACEBOOK/ MARIA BUTINA
- Author, Yusuf Jumah
- Nafasi, BBC Swahili
Tabasamu zao zilikuwa za kuvutia ,urembo wao ulikuwa kama chambo na misheni zao zilikuwa za siri kubwa .
Mahusiano ya karibu waliojenga na wanaume mbali mbali nchini Marekani yalikuwa na lengo moja kuu:Kukusanya habari muhimu kuhusu mipango ya siri na mikubwa ya serikali ya Marekani na kuhakikisha kwamba Urusi ilifahamu yote yaliokuwa yakiendelea nchini humo .
Wengi waliishi nchini Marekani kwa miaka na hata kuolewa na kuanzisha familia nchini humo .Katika usiri wa maisha yao uliojaa mengi ya giza na yasiojulikana walidaiwa kuwa majasusi wa Moscow.Karibu katika maisha ya baadhi ya wanawake wa kipekee waliopewa mafunzo ya kijasusi kuisaidia Urusi kufahamu yote yaliyokuwa yakifanyika ndani na nje ya serikali ya Marekani na washirika wake .
Kipindi cha Vita baridi
Kwa miaka mingi ilishukiwa kwamba Urusi haikuwa imekomesha oparesheni zake za kijasusi nchini Marekani na katika sehemu nyingi za dunia .Hata hivyo tangu nyakati za vita baridi na mapambano ya nchi za magharibi dhidi ya ukomunisti ,Urusi iliendelea na oparesheni za kisiri za ujasusi ambazo mashirika mengine ya ujasusi hasa ya Marekani hayakudhani zingeweza kufanikishwa kwa muda mrefu .
Baadhi ya oparesheni hizo zilihusisha majasusi maalum wa kike ambao walipewa mafunzo na Moscow na kisha kutumwa katika miji ya Marekani ili kukita kabisa ndani ya maisha ya kijamii ya wamarekani na kufichua siri nyingi za sekta mbali mbali nchini humo .Wadadisi wanasema hadi sasa kunazo oparesheni kama hizo za majasusi wa Urusi nchini Marekani na hata Uingereza .
Katika miaka ya hivi karibuni hata hiyo mashirika ya kijasusi ya Marekani yamefaulu kuvunja mitandao ya siri ya oparesheni za kijasusi za Urusi nchini mwao.Ufichuzi umeonyesha matumizi ya wanawake warembo kupindukia ambao walikuwa na mafunzo maalum waliotumiwa kwa miaka mingi katika oparesheni hizo za Moscow.Unaweza kusema walitoka 'Moscow na mapenzi' kumbe walikuwa na hila .Hawa hapa baadhi ya wanawake kama hao waliokamatwa kwa kushukiwa kuwa majasusi wa Moscow:
Maria Butina
Julai mwaka wa 2018 Serikali ya Marekani ilitangaza kumkamata mwanamke mwenye umri wa miaka 29 raia wa Urusi kwa jina Maria Butina . Alishtumiwa kwa kuifanyia kazi serikali ya Urusi na lengo lake kuu lilikuwa kuyaingilia makundi ya kisiasa nchini Marekani kwa lengo la kupata Habari zinazoeza kutumiwa kuihujumu Marekani .

Chanzo cha picha, MARIA BUTINA/FACEBOOK
Maria Butina alikuwa ameanzisha uhusiano wa karibu na chama cha Republican na alikuwa mtetezi wa haki za kumiliki bunduki, kulingana na ripoti za vyombo vya habari nchini Marekani
Mashtaka dhidi yake hayakuhusiana na uchunguzi wa Jopo la Mueller ambao ulihusu madai ya Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani wa mwak wa 2016.
Inasemekana alifanya kazi kwa maelekezo ya maafisa wa ngazi za juu wa Kremlin.
Wakili wa Bi Butina Robert Driscoll alisema kwamba mteja wake alikuwa "sio jasusi" na badala yake tu alikuwa mwanafunzi wa uhusiano wa kimataifa "ambaye alilenga kutumia digrii yake kufanya taaluma ya biashara".
Aliingia Marekani kama mwanafunzi
Butina, alikuwa mzaliwa wa Siberia na alenda Marekani a kwa visa ya mwanafunzi kusoma katika Chuo Kikuu cha Amerika. Malalamiko hayo yanadai kwamba alikuwa akiifanyia kazikwa siri serikali ya Urusi
Alianzisha kikundi kinachoitwa Right to Bear Arms kabla ya kufika Marekani , na vyombo vya habari vya Marekani hapo awali viliripoti uhusiano wake na Chama cha Kitaifa cha Bunduki (NRA), kundi lenye uhawishi mkubwa sana kuhusu haki ya kutumia nguvu ya bunduki nchini Marekai
Hapo awali alikanusha kufanya kazi na serikali ya Urusi.
Washington Post iliripoti kwamba alikua msaidizi wa benki ya Urusi na seneta wa zamani Alexander Torshin.
Bwana Torshin, ambaye ni mwanachama wa maisha wa NRA, na Bi Butina walihudhuria hafla za NRA huko Marekani kuanzia 2014.
Alihudhuria pia hafla ya kampeni ya Trump na inasemekana alimwuliza Bw Trump maoni yake juu ya uhusiano wa nje na Urusi.
"Tunaelewana na Putin," Bwana Trump alikuwa amejibu, kulingana na Washington Post.

Anna Chapman
Mnamo mwaka wa 2010 julai ulimwengu ulipewa onyesho lililofanana na maigizo ya filamu baada ya watu kumi waliodaiwa kuwa majasusi wa Urusi kukamatwa na shirika la FBI nchini Marekani .Kumi hao walikuwa wameishi Marekani kwa muda mrefu sana na hata kuendelea na maisha ya kifamilia kama Wamarekani wengine .
Majasusi wa Marekani walikuwa wamewafuatilia kwa takriban miaka kumi kabla ya kukamatwa kwao na baadaye kurejeshwa Urusi .
Miongoni mwa waliokamatwa ni mwanam ke mmoja ambaye urembo wake uliviutia vyombo vya habari kote ulimwenguni huku picha zake zikitundikwa katika majarida mbali mbali na watu wengi wakitaka kujua mengi kumhusu .Jina lake ni Anna Chapman na wakati huo alikuwa na umri wa miaka 28 .
Jina lake halisi hata hivyo ni Anna Kushchenko na alikuwa binti wa Mwanadiplomasia mmoja mkuu wa Urusi aliyesomea Volgograd na Moscow.
Anadaiwa kuishi Uingereza kwa miaka mitano akihudumu katika sekta ya fedha na hata aliolewa na raia wa Uingereza Alex Chapman kati ya mwaka wa 2002 na 2005.Alisalia na jina la pili la Chapman hata walipotengana .
Bwana chapman baadaye aliliambia jaria la the Daily telegraph kwamba hakushangazwa na yaliyomsibu mke wake wa zamani . Alisema mke wake alikuwa amebadilika sana katika ndoa yao na alikuwa akifanya mikutano ya sir ina 'rafiki zake wa Urusi'
Uhusiano na KGB
Bwana Chapman pia alifichua kwamba mke wake wakati ho alikuwa amemueleza kwamba babake alikuwa afisa wa ngazi ya juu wa shirika la ujasusi la zamani la Urusi KGB na kwamba 'angemfanyia babake lolote'.
Bi Chapman hakuficha uhusiano wake na Urusi alipowasili mjini New York kutoka Moscow Februari mwaka wa 2010 akisema alitaka kuanzisha kampuni ya ajira iliyowalenga wanataaluma katika miji yote miwili .
Baadaye Chapman alikuwa miongoni mwa maajenti wa Urusi waliokabidhiwa Moscow wakati nchi hizo mbili zilipobadilishana majasusi waliokamatwa katika ngome ya kila mmoja wao .
Mengi kumhusu chapman yangali yameghubikwa na usiri mkubwa lakini wajibu wake na oparesheni za ujasusi za Urusi pia bado hazijatoa ufunuzi kuhusu jukumu lake katika sakata hiyo nzima .












