Martha Koome: Jaji Mkuu mpya Kenya aingia kazini pakiwa na mengi kushughulikiwa

Jaji mkuu mpya

Chanzo cha picha, JUDICIAL SERVICE COMMISSION

Maelezo ya picha, Muda mfupi baada ya bunge kuidhinisha uteuzi wake ,rais Uhuru Kenyatta alimteua rasmi Martha Koome kuwa Jaji Mkuu wa Kenya

Jaji mkuu mpya wa Kenya Martha Koome na mwanamke wa kwanza kushikilia wadhifa huo nchini Kenya ana mengi yanayomgonja afisini .

Katika siku ambayo bunge liliidhinisha uteuzi wake ,rais Uhuru Kenyatta alitumia muda wa chini ya saa tano kuufanya rasmi uteuzi huo ili kumfanya aanze kazi . Hata hivyo ana mengi ambayo yanamkodolea macho na wengi wanangoja kwa hamu kuona jinsi atakavyoyashughulikaia .

Kesi ya BBI

Baadhi ya mambo hayo ni kulinda uhuru wa mahakama ambao sasa umeonekana kutishiwa kufuatia uamuzi wa majaji kwamba mchakato wa kuirekebisha katiba kupitia Jopo la Maridhiano(BBI) ulikiuka sheria na ni kinyume na katiba . Pia kuna hofu kwamba uhuru wa idara ya mahakama utakuwa hatarini endapo afisi nyingine ya kudhibiti shughuli za mahakama itaundwa kama ilivyopendekezwa .

Kikubwa hata hivyo anapoanza kazi yake ni uteuzi wa jopo la majaji ambao watasikiza kesi ya rufaa iliyowasilishwana serikali kupinga uamuzi wa majaji wa mahakama kuu waliotupilia mbali mchakato mzima wa BBI .

Hilo ni suala kikubwa kisiasa nchini Kenya na Koome atahitaji ustaarabu wa kuweza kulikwea kwani kesi hiyo ina uwezo mkubwa w hata kufikishwa mbele ya mahakama ya juu zaidi ambayo yeye ndiye rais wa korti hiyo.

Alhamisi iliyopita,jopo la majaji watano lililoongozwa na Jaji Joel Ngugi lilitangaza Mswada wa BBI kuwa kinyume cha katiba ukitaja ukiukwaji wa sheria uliofanywa wakati wa kuandaa na kuunda mchakato mzima.

Walitangaza Mswada wa BBI kuwa batili. Hatua hiyo imefanya idara ya mahakama kuwa kiungo muhimu sana katika kuamua hatima ya mchakato mzima wa BBI na siasa za mwaka wa 2022.Kila atakachofanya jaji mkuu mpya Koome,kitaangazia kwa zaidi ya macho mawili . Kazi kubwa kwake itakuwa kuhakikisha kwamba anatoa haki na pia anadumisha uhuru wa idara ya mahakama .

Alikuwa ameonyesha kuwa suala hilo linaweza kushughulikiwa kupitia mazungumzo kati ya Mahakama na Serikali akisema wanategemeana.

Koome ambaye atakuwa jaji mkuu wa 15 wa Kenya analeta uzoefu wamiaka mingi aliopata kutoka zaidi ya miongo mitatu katika idara ya Mahakama.

Kando na kizingiti cha jinsi atakavyoshughuikia kesi kuhusiana na mchakato wa BBI ,Koome pia atakabiliana na changamoto zifuatazo;

Kukaidi maagizo ya mahakama

Jaji mku kwanza ,atalazimika kuboresha uhusiano kati ya idara ya mahakama na vitengo vingine vya serikali kama ofisi ya rais ,na bunge .

Rais Uhuru Kenyatta hajakuwa na uhusiano unaoweza kuonekana kama mzuri na watangulizi wa Koome na idara ya mahakama kwa jumla .Wakati mahakama ya juu zaidi ilipofutilia mbali ushindi wake katika uchaguzi wa mwaka wa 2017 ,rais Kenyatta alighadhabika na kuwaita majaji wa mahakama hiyo kama 'wakora'.

Hilo lilizidisha mgawanyiko uliokuwepo kati ya serikali na idara ya mahakama hatua ambayo iliathiri kwa njia fulani ufanisi wa idara hiyo kutekeleza majukumu yake ya kuhakikisha kwamba Wakenya wanapata haki . Uhusiano huo tena umejaribiwa wiki jana baada ya majaji kufanya uamuzi wa kuharamisha mchakato wa BBI .

Kando na tukio hilo , rais ,wizara na idara za serikali pia hawajakuwa wakitii maamuzi yanayotolewa na majaji .

Rais Kenyatta amekataa kuidhinisha uteuzi wa majaji 41 wa mahakama ya rufaa walioteuliwa miaka miwili iliyopita licha ya mahakama kusema kwamba msimamo wake unakiuka katiba .

jAJI MKUU

Chanzo cha picha, JUDICIAL SERVICE COMMISSION

Kesi nyingi ambazo zimewasilishwa kortini na serikali huendelea kudhihirisha mgawanyiko uliopo kati ya vitengo viwili .Licha ya mahakama kuamuru kwamba nafasi ya makatibu wasaidizi wa mawaziri ,CAS ni ukiukaji wa sheria na zinafaa kuondolewa , rais hajatekeleza agizo hilo na maafisa hao wangali wanahudumu afisini. Kesi nyingine ambayo mahakama ilitoa maagizo yake lakini yamepuuzwa ni kuhusu uhalali wa nafasi ya makamishna wa kaunti .

Korti imesema nafasi hiyo haifai kuwepo katika mfumo wa sasa wa katiba kwani ni muendelezo wa uliokuwa utawala wa mikoa .Serikali kuu hata hivyo imewaacha makamishna hao kusalia ofisini na mwanzoni wakati ugatuzi ulipoanza kutekelezwa nchini Kenya palitokea mgongano kati ya makamishna hao na magavana .

Serikali iliwatumia kama macho na masikio yake katika kaunti ilhali magavana waliochukulia kama maajenti waliotumwa kuhujumu ugatuzi na kuingilia mamlaka yao katika maeneo ya mashinani .

Koome atakuwa na kibarua kigumu za kujaribu kubadilisha mtindo huo ambao ulimfanya mtangulizi wake David Maraga kuonekana kuwa adui wa serikali kwa sababu ya kueleza kufadhaika kwake mara kwa mara kuhusu hatua ya idara za serikali kutotii maagizo yanayotolewa na mahakama . Endapo atafaulu kubadilisha hilo ,Koome huenda akapiga nusu ya hatua ya kusajili ufanisi mkubwa katika kazi yake hiyo .

Ufisadi

Donda sugu la rushwa ni tatizo kubwa ambalo jaji mkuu mpya atakutana nalo ana kwa ana atakapoidhinishwa kuanza kazi . Lalama zimezidi kuwepo kuhusu jinsi rushwa ilivyokithiri katika idara ya mahakama . Kuna maamuzi mengi ambayo yamekuwa yakitolewa na majaji ambayo mwishowe yamebainika kushawishiwa na rushwa .

Utafiti mmoja uliofanywa mwaka wa 2019 kwa mfano uliitaja mahakama ya rufaa ya Malindi kama fisadi Zaidi ilhali mahakama kuu ya Kitale ilitajwa kama yenye 'watu wengi wanaoitisha rushwa'.

Jaji mkuu wakati huo David Maraga alisema utafiti ulionyesha kwamba asilimia 22 ya watu waliotumia mahakama walisema walitakiwa kutoa rushwa huko Malindi ilhali 27 hawakupendezwa na huduma katika mahakama kuu ya Kitale.

Mahakama hizo mbili ni mifano tu ya jinsi wovu huo ulivyokithiri katika idara ya mahakama na watangulizi wa Koome walikuwa wamelipa kipau mbele suala la kupambana na rushwa mahakamani .

Mrundiko wa kesi

Tatizo la mrundiko wa kesi sio geni katika idara ya mahakama nchini Kenya .Jaji mkuu ajaye atakuwa na kibarua na kuweka mikakati iliyoanzishwa na watangulizi wake kufanikisha mpango wa mahakama za kidijitali na za kuhama hama ili kuhakikisha kwamba kesi zinashughulikiwa haraka na haki inapatikana kwa wote .

Kuna kesi ambazo zimekuwa zikisikizwa kw ahata miaka 10 huku majaji wanaozishughulikiwa wakihamishwa kiutoka kituo kimoja hadi kingine na hata wengine wakistaafu wakiendelea kuzishughulikia baadhi ya kesi .

Utafiti wa mwaka wa 2019 ulionyesha kwamba Wakenya wengi hawakufurahia muda mrefu ambao majaji walitumia kufanya maamuzi ya kesi . wengi wanaotumia mahakama walitaka idara hiyo kuboresha utumizi wa muda ,kuboresha mawasiliano kati ya mahakama na walalamishi na kutoa maamuzi kwa wakati ili kuepuka visa vya kuchelewesha haki .

Jaji Koome atakuwa na kazi kubwa ya kuweza kuhakikisha kwamba mrundiko wa kesi ambao umekuwepo kwa muda mrefu unashughulikiwa na kesi za awali zinakamilishwa .

Hili litahitaji raslimali za kuwaajiri majaji zaidi au kujenga mahakama katika maeneo mbali mbali ya taifa . Mpango huo ulianzishwa na watangulizi wake lakini sasa atahitaji kuweka himizo na kuboresha asasi za kufanikisha upatikanaji wa yote anayohitaji kushughulikia mrundiko wa kesi mahakamani.

Koome bila shaka anazifahamu vizuri changamoto hizi na atakuwa na mikakati yake au mipango ya kuweza kuzishughulikia ili kuafikia ufanisi wakati wa muhula wake kama jaji mkuu.Wengi watangoja kwa hamu kuona mbinu atakazotumia ili kuweza kufaulu katika masuala ambayo watangulizi wake walijaribu na kukosa kufanikiwa.

Bajeti na ufadhili wa idara ya mahakama

Jambo ambalo limekuwa likizua tatizo la mara kwa mara kati ya serikali na idara ya mahakama ni kiasi cha fedha ambacho idara hiyo inatengewa na Wizara ya Fedha .

Mwaka wa 2019 Jaji mkuu mstafuu David Maraga alilalamika hadharani kuhusu kupunguzwa kwa mgao wa fedha ambazo idara hiyo ilipewa .Oparesheni za idara hiyo zimelemazwa na kuathiriwa pakubwa kwa sababu ya uhaba wa fedha . Mahakama zilizoathiriwa sana ni korti za kuhama hama ambazo Maraga alilenga kuzitumia kushughulikia kwa haaka kesi ktika sehemu zilizoko mbali na mahakama .

Jaji Koome atakuwa na jukumu la kuishawishi serikali na bunge kuangalia upya kiasi cha fedha ambacho idara ya mahakama inatengewa ili iweze kuwapa wakenya haki popote walipo. Wakati wa kipindi David Maraga, alilalamika peupe kwamba vitengo vingine vya serikali vilikuwa 'vikiikandamiza' idara ya mahakama .

Maraga wakati huo alisema idara ya mahakama ilihitaji kati ya shilingi bilioni 5 na 6 ili kuendesha oparesheni zake kila mwaka kwa miaka 10 ijayo .

Wakati huo aliwashtumu mawaziri na makatibu wa kudumu ambao hakuwataja waliotaka kumuondoa ofisini . Itakuwa kibarua sasa kwa Jaji Koome kuhakikisha kwamba changamoto hiyo haikumbi hatamu yake atakaposhika hatamu kama jaji mkuu wa kwanza mwanamke nchini .