Martha Koome: Kenya ipo mbioni kuwa na jaji mkuu mpya mwanamke, Je atakabiliwa na changamoto zipi?

Martha Koome

Chanzo cha picha, JUDICIAL SERVICE

Kenya ipo mbioni kumteua jaji mkuu mpya wa kwanza mwanamke baada ya rais Uhuru Kenyatta kuliwasilisha jina la jaji Martha Koome bungeni ili apigwe msasa ana kura kupigwa iwapo ataidhinishwa kuichukua nafas hiyo iliyowachwa wazi na David Maraga ambaye alistaafu .

Jaji huyo wa mahakama ya rufaa atakuwa jaji mkuu wa 15 wa Kenya tangu nchi hiyo ijinyakulie uhuru iwapo bunge litaidhinisha uteuzi wake .

Tume ya huduma kwa idara ya mahakam ilimtangaza Koome mwenye umri wa miaka 61 kama mshindi wa mahojiano kati ya watu wengine 10 waliotuma maombi ya kupewa kazi hiyo .Bunge sasa litajadili uteuzi wake ,katika kinachoonekana tu kama utaratibu lakini anatarajiwa kuidhinishwa na kuteuliwa rasmi na rais .

Koome atahudumu kama jaji mkuu kwa miaka tisa ijayo ambayo itasheheni vipindi viwili vya uchaguzi na uwezekano wa kuandaliwa kwa kura ya maoni kuhusu katiba mpya . Anakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinamngoja afisini ambazo watangulizi wake walijaribu kadri ya uwezo wao kuzishughulikia lakini bila mafanikio waliotarajia .

Martha Koome ni nani?

Jaji Martha Koome alizaliwa katika Kijiji cha Kithiu, katika kaunti ya Meru 1960.

Jaji Koome baadaye alisomea shahada ya sheria katika Chuo kikuu cha Nairobi ambapo alifuzu 1986 na na kujiunga na chuo cha mafunzo ya Sheria nchini Kenya mwaka uliofuata.

Alianzisha Ofisi yake ya huduma za uanasheria 1988, na baadaye akajiunga na Huduma ya mahakama 2003 na kuhudumu katika mahakama tofauti kote nchini, wakati ambapo pia alihudumu kama mwanachama wa chama cha wanasheria nchini Kenya LSK.

Baadaye alijiunga na Chuo kikuu cha London ambapo alisomea shahada ya uzamili kuhusu sheria ambapo alifuzu na kupata cheti cha Sheria ya Umma ya kimataifa 2010 .

Mwaka 2011 , alipandishwa cheo na kuwa jaji wa mahakama ya rufaa na mwezi Septemba mwaka huohuo, alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Muungano wa Mahakimu na Majaji nchini Kenya. Jaji Koome , katika kipindi chake cha miongo mitatu amekuwa mtetezi wa haki za wanawake na ustawi wa Watoto.

Kuna wakati mmoja alihudumu kama mwenyekiti wa baraza la kitaifa la Jopo Maalum kuhusu usimamizi wa haki za watoto ambapo alisaidia katika kufanyia marekebisho sheria ya Watoto.

Jaji mku mpya atakabiliwa na changamoto gani?

Kuna mengi yanayomngoja mezani wakati uteuzi wake utakapokuwa rasmi,kwanza atalazimika kuboresha uhusiano kati ya idara ya mahakama na vitengo vingine vya serikali kama ofisi ya rais ,na bunge .

Rais Uhuru Kenyatta hajakuwa na uhusiano unaoweza kuonekana kama mzuri na watangulizi wa Koome na idara ya mahakama kwa jumla .Wakati mahakama ya juu zaidi ilipofutilia mbali ushindi wake katika uchaguzi wa mwaka wa 2017 ,rais Kenyatta alighadhabika na kuwaita majaji wa mahakama hiyo kama 'wakora'.

Hilo lilizidisha mgawanyiko uliokuwepo kati ya serikali na idara ya mahakama hatua ambayo iliathiri kwa njia fulani ufanisi wa idara hiyo kutekeleza majukumu yake ya kuhakikisha kwamba Wakenya wanapata haki .

Kukaidi maagizo ya mahakama

Kando na tukio hilo , rais ,wizara na idara za serikali pia hawajakuwa wakitii maamuzi yanayotolewa na majaji .

Rais Kenyatta amekataa kuidhinisha uteuzi wa majaji 41 wa mahakama ya rufaa walioteuliwa miaka miwili iliyopita licha ya mahakama kusema kwamba msimamo wake unakiuka katiba .

Kesi nyingi ambazo zimewasilishwa kortini na serikali huendelea kudhihirisha mgawanyiko uliopo kati ya vitengo viwili .Licha ya mahakama kuamuru kwamba nafasi ya makatibu wasaidizi wa mawaziri ,CAS ni ukiukaji wa sheria na zinafaa kuondolewa , rais hajatekeleza agizo hilo na maafisa hao wangali wanahudumu afisini. Kesi nyingine ambayo mahakama ilitoa maagizo yake lakini yamepuuzwa ni kuhusu uhalali wa nafasi ya makamishna wa kaunti .

Korti imesema nafasi hiyo haifai kuwepo katika mfumo wa sasa wa katiba kwani ni muendelezo wa uliokuwa utawala wa mikoa .Serikali kuu hata hivyo imewaacha makamishna hao kusalia ofisini na mwanzoni wakati ugatuzi ulipoanza kutekelezwa nchini Kenya palitokea mgongano kati ya makamishna hao na magavana .

Serikali iliwatumia kama macho na masikio yake katika kaunti ilhali magavana waliochukulia kama maajenti waliotumwa kuhujumu ugatuzi na kuingilia mamlaka yao katika maeneo ya mashinani .

Koome atakuwa na kibarua kigumu za kujaribu kubadilisha mtindo huo ambao ulimfanya mtangulizi wake David Maraga kuonekana kuwa adui wa serikali kwa sababu ya kueleza kufadhaika kwake mara kwa mara kuhusu hatua ya idara za serikali kutotii maagizo yanayotolewa na mahakama . Endapo atafaulu kubadilisha hilo ,Koome huenda akapiga nusu ya hatua ya kusajili ufanisi mkubwa katika kazi yake hiyo .

Rushwa

Donda sugu la rushwa ni tatizo kubwa ambalo jaji mkuu mpya atakutana nalo ana kwa ana atakapoidhinishwa kuanza kazi . Lalama zimezidi kuwepo kuhusu jinsi rushwa ilivyokithiri katika idara ya mahakama . Kuna maamuzi mengi ambayo yamekuwa yakitolewa na majaji ambayo mwishowe yamebainika kushawishiwa na rushwa .

Utafiti mmoja uliofanywa mwaka wa 2019 kwa mfano uliitaja mahakama ya rufaa ya Malindi kama fisadi Zaidi ilhali mahakama kuu ya Kitale ilitajwa kama yenye 'watu wengi wanaoitisha rushwa'.

Jaji mkuu wakati huo David Maraga alisema utafiti ulionyesha kwamba asilimia 22 ya watu waliotumia mahakama walisema walitakiwa kutoa rushwa huko Malindi ilhali 27 hawakupendezwa na huduma katika mahakama kuu ya Kitale.

Mahakama hizo mbili ni mifano tu ya jinsi wovu huo ulivyokithiri katika idara ya mahakama na watangulizi wa Koome walikuwa wamelipa kipau mbele suala la kupambana na rushwa mahakamani .

Bajeti ya idara ya mahakama

Jambo ambalo limekuwa likizua tatizo la mara kwa mara kati ya serikali na idara ya mahakama ni kiasi cha fedha ambacho idara hiyo inatengewa na Wizara ya Fedha .

Mwaka wa 2019 Jaji mkuu mstafuu David Maraga alilalamika hadharani kuhusu kupunguzwa kwa mgao wa fedha ambazo idara hiyo ilipewa .Oparesheni za idara hiyo zimelemazwa na kuathiriwa pakubwa kwa sababu ya uhaba wa fedha . Mahakama zilizoathiriwa sana ni korti za kuhama hama ambazo Maraga alilenga kuzitumia kushughulikia kwa haaka kesi ktika sehemu zilizoko mbali na mahakama .

Jaji Koome atakuwa na jukumu la kuishawishi serikali na bunge kuangalia upya kiasi cha fedha ambacho idara ya mahakama inatengewa ili iweze kuwapa wakenya haki popote walipo. Wakati wa kipindi David Maraga, alilalamika peupe kwamba vitengo vingine vya serikali vilikuwa 'vikiikandamiza' idara ya mahakama .

Maraga wakati huo alisema idara ya mahakama ilihitaji kati ya shilingi bilioni 5 na 6 ili kuendesha oparesheni zake kila mwaka kwa miaka 10 ijayo .

Wakati huo aliwashtumu mawaziri na makatibu wa kudumu ambao hakuwataja waliotaka kumuondoa ofisini . Itakuwa kibarua sasa kwa Jaji Koome kuhakikisha kwamba changamoto hiyo haikumbi hatamu yake atakaposhika hatamu kama jaji mkuu wa kwanza mwanamke nchini .

Mrundiko wa kesi

Tatizo la mrundiko wa kesi sio geni katika idara ya mahakama nchini Kenya .Jaji mkuu ajaye atakuwa na kibarua na kuweka mikakati iliyoanzishwa na watangulizi wake kufanikisha mpango wa mahakama za kidijitali na za kuhama hama ili kuhakikisha kwamba kesi zinashughulikiwa haraka na haki inapatikana kwa wote .

Kuna kesi ambazo zimekuwa zikisikizwa kw ahata miaka 10 huku majaji wanaozishughulikiwa wakihamishwa kiutoka kituo kimoja hadi kingine na hata wengine wakistaafu wakiendelea kuzishughulikia baadhi ya kesi .

Utafiti wa mwaka wa 2019 ulionyesha kwamba Wakenya wengi hawakufurahia muda mrefu ambao majaji walitumia kufanya maamuzi ya kesi . wengi wanaotumia mahakama walitaka idara hiyo kuboresha utumizi wa muda ,kuboresha mawasiliano kati ya mahakama na walalamishi na kutoa maamuzi kwa wakati ili kuepuka visa vya kuchelewesha haki .

Jaji Koome atakuwa na kazi kubwa ya kuweza kuhakikisha kwamba mrundiko wa kesi ambao umekuwepo kwa muda mrefu unashughulikiwa na kesi za awali zinakamilishwa .

Hili litahitaji raslimali za kuwaajiri majaji zaidi au kujenga mahakama katika maeneo mbali mbali ya taifa . Mpango huo ulianzishwa na watangulizi wake lakini sasa atahitaji kuweka himizo na kuboresha asasi za kufanikisha upatikanaji wa yote anayohitaji kushughulikia mrundiko wa kesi mahakamani.

Koome bila shaka anazifahamu vizuri changamoto hizi na atakuwa na mikakati yake au mipango ya kuweza kuzishughulikia ili kuafikia ufanisi wakati wa muhula wake kama jaji mkuu.Wengi watangoja kwa hamu kuona mbinu atakazotumia ili kuweza kufaulu katika masuala ambayo watangulizi wake walijaribu na kukosa kufanikiwa.