Ligi Kuu England: Man City imegundua udhaifu wa Arsenal katika mbio za ubingwa?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Shamoon Hafez
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Vijana wa Pep Guardilo, Manchester City wamejibu kichapo cha Arsenal cha 2:1 kutoka kwa Bournemouth siku ya Jumamosi, kwa ushindi wa 3-0 dhidi ya Chelsea, ushindi ambao ulifungua mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England.
Huku Arsenal ikiyumba, City inazidi kuwa imara baada ya kusonga mbele kwa pointi sita kuwakaribia vinara hao, huku wakiwa na mchezo mmoja wa kiporo, hali inayoonekana kuwa mbaya kwa Arsenal.
Shangwe za City zimesikika kote magharibi mwa London - na furaha ambayo Guardiola, wachezaji wake na mashabiki waliionyesha, iliashiria jinsi ushindi huu ulivyo muhimu.
City wamefanikiwa katika michezo mitatu iliyopita, wakifunga mabao tisa dhidi ya Arsenal, Liverpool na Chelsea bila kuruhusu bao, wakitwaa Kombe la Carabao na kufika nusu fainali ya Kombe la FA katika kipindi hicho.
"Tumecheza michezo mitatu vizuri, lakini timu bora zaidi nchini Uingereza ni Arsenal na timu bora zaidi barani Ulaya ni Arsenal," alisema Guardiola.
Man City na Arsenal

Chanzo cha picha, Getty Images
Takwimu zinaonyesha Aprili ni mwezi wenye matunda zaidi kwa Guardiola na mbaya zaidi kwa Mikel Arteta wa Arseanl - na matokeo kutoka kwa wapinzani hao wawili wa taji wikendi hii yalithibitisha hilo.
2022-23, Gunners ilikuwa ni timu iliyotumia siku nyingi zaidi (248) kileleni mwa Ligi Kuu bila kushinda taji hilo.
Walikuwa mbele kwa pointi tano baada ya michezo 32 iliyochezwa msimu huo, lakini City, wakiwa na michezo miwili ya kiporo, waliwapiku.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Guardiola - na Arteta - wamewahi kuwa hapa hapo awali.
Jinsi Arsenal walivyopoteza nyumbani dhidi ya AFC Bournemouth ni jambo baya kwao, lakini jambo moja ni hakika - City wametumia fursa ya kupoteza huko kwa kuongeza rekodi yao ya kutoshindwa katika ligi hadi michezo tisa.
Wamepoteza mchezo mmoja tu kati ya michezo 19 iliyopita ya ligi kuu, kuonyesha kwamba wanaanza tena kwenda kileleni.
" Manchester City wameona udhaifu," beki wa zamani wa Manchester United Gary Neville alisema kwenye Sky Sports. "Wanajiandaa na pambano kubwa wikendi ijayo."
Beki wa zamani wa City, Micah Richards, anasema: "Arsenal wangeweza kuwa mbele kwa pointi tisa jana, sasa ni pointi sita."
"Mashabiki wana imani na hawajaacha kuamini... Sisemi kwamba watashinda lakini wamejipa matumaini na hilo ndilo wanaloweza kulifanya."
Jambo moja ambalo linawapa nafuu Arsenal ni michezo iliyobaki.
Ingawa mechi ya Jumapili ijayo inasalia kuwa mechi kubwa, michezo mitano iliyobaki ya Gunners ni dhidi ya timu zilizo katika nusu ya mwisho ya jedwali.
Wakati huo huo, City italazimika kukabiliana na timu ngumu Everton na Brentford, pamoja na kukamilisha msimu huu nyumbani dhidi ya Aston Villa, wanaowania ubingwa wa Ligi ya Mabingwa.
Mechi ijayo

Chanzo cha picha, BCC
"Wakitushinda, basi tutakuwa tumekwisha, tukitoka sare pia tumekwisha," alisema Guardiola.
Ikiwa City wataweza kushinda na kupunguza pengo kati ya timu hizo, wanaweza kuwa kileleni mwa jedwali wakati Arsenal watakapocheza tena kwenye Uwanja wa Emirates.
City watasafiri hadi Burnley kwa ajili ya mchezo wao Jumatano, Aprili 22. Ushindi katika mechi hiyo utawapeleka kileleni wakiwa na mechi tano za kucheza.
Guardiola aliboresha kikosi chake msimu uliopita wa joto kwa kuwatoa wachezaji nyota wenye uzoefu wakiwemo Kevin de Bruyne, Ilkay Gundogan, Kyle Walker na Ederson.
Waliingia wachezaji kama Gianluigi Donnarumma na Rayan Cherki, huku Marc Guehi na Antoine Semenyo wakiongezwa Januari - wachezaji hao wote wana umri wa miaka 26 au chini na walianza katika ushindi wa Jumapili.
Hii inaifanya kikosi cha City ambacho ni kichanga lakini kinachoonyesha kuwa kina uwezo wa kukabiliana na changamoto na kiko njiani kwa ajili ya kushinda mataji matatu ya ndani, baada ya kutwaa Kombe la Carabao.
Nahodha Bernardo Silva amekuwa pamoja na Guardiola katika kila hatua na anaongoza timu hiyo bila ubinafsi, huku kiungo Rodri akianza kuonyesha aina ya uchezaji uliompatia tuzo ya Ballon d'Or ya 2024, baada ya kuwa nje ya uwanja kutokana na majeraha kwa muda mrefu.
Erling Haaland anasalia kuwa mfungaji bora wa ligi hiyo akiwa na mabao 22. Mnorway huyo alifunga mara 19 katika michezo yake 17 ya mwanzo, lakini amefunga mara tatu pekee katika michezo 13 tangu wakati huo, na kuthibitisha kwamba City hawategemei sana mchezaji huyo mwenye miaka 25 kuchukua mzigo wa mabao.
Kuondolewa kwa City katika Ligi ya Mabingwa kunamaanisha kuwa wana wiki moja ya mapumziko kabla ya kukabiliana na Arsenal, ambao watalazimika kucheza mchezo wao wa pili wa robo fainali dhidi ya Sporting.
Ikiwa Man City itapata ushindi mwingine wikendi ijayo - wataimarisha zaidi nafasi yao ya kutwaa ubingwa.















