Uhuru wa Mahakama unadhoofishwa na serikali ya Kenya?

Uhuru Kenyatta

Chanzo cha picha, IKULU YA RAIS

Maelezo ya picha, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta

Joto la kisiasa nchini Kenya limepanda takriban miaka miwili kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa 2022.

Vitendo vingi vya siasa hiyo vimeekelezwa katika bunge na vingine katika idara ya mahakama.

Katika bunge, viongozi waasi katika chama tawala cha Jubilee wamekuwa wakilengwa siku chache tu baada ya hatua kama hizo kuchukuliwa dhidi ya wenzao waliopo katika bunge la seneti.

Kuondolewa kwao kama wawakilishi wa serikali katika kamati kadhaa ama hata vyeo kadhaa katika bunge na seneti hakuhusiani na utendakazi wao kwani wengi wao awali wamekuwa katika mstari wa mbele katika kuuza sera za serikali kisiasa kwa hali na mali.

Kwa upande mwengine mahakama imekuwa katika malumbano na serikali kufuatia agizo la rais lililotolewa ambalo linaipanga serikali upya kwa lengo la kuafikia matakwa ya Rais Uhuru Kenyatta.

Agizo la rais la hivi majuzi

Rais Kenyatta katika agizo lake ameonekana kuipanga na kuipangua idara ya mahakama kwa kuorodhesha mkono huo ulio huru chini ya mwanasheria mkuu bwana Kihara.

Mbali na hayo kiongozi huyo wa taifa pia alisema katika agizo hilo kwamba shughuli na majukumu ya Tume huru katika katiba kwa mfano IEBC zitasimamiwa na mshauri huyo wa serikali kuhusiana na masuala ya kisheria.

Kama ilivyo katika historia ya taifa hili shughuli za kura zimekuwa zikileta umwagikaji wa damu nchini Kenya kila baada ya uchaguzi huku pande kinzani zikilaumiana kuingilia na hata kuvuruga shughuli hiyo muhimu.

Hivyobasi tume ya uchaguzi ilifanywa kuwa tume huru isiosimamiwa na rais ama wandani wake ili kuleta usawa katika shughuli hiyo ya kidemokrasia ya kuchagua viongozi wapya kila baada ya kipindi cha miaka mitano.

Cha kushangaza ni kwamba agizo hilo la rais sasa linatoa fursa kwa mwanasheria mkuu Paul Kihara kusimamia tume zote ikiwemo tume ya uchaguzi.

Jaji Mkuu wa Kenya David Maraga

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Jaji Mkuu wa Kenya David Maraga

Hii ina maana kwamba tume hiyo inayotakiwa kuwa huru itakuwa ikipata maelekezo kutoka kwa mwanasheria mkuu wa serikali hatua inayokwenda kinyume na sheria simamizi za uhuru wa tume hiyo.

Lakini akimjibu rais baada ya agizo hilo jaji mkuu David Maraga alimwambia rais kwamba idara ya mahakama haichukui maagizo kutoka serikali .

Alisema: Agizo hilo haliwezi kubadilisha ama kutoa majukumu kutoka kwa idara zenye nguvu sawa na tume huru.

Alisema kwamba idara ya mahakama sio wizara ama idara ya serikali inayopatiwa maagizo na serikali.

Kulingana na wakili na mchanganuzi wa kisiasa nchini Kenya Alutalala Mukhwana hatua hiyo ni 'ubakaji' wa katiba kwa sababu tayari usimamizi huo ni kinyume na sheria inayosimamia idara ya mahakama na tume hizo.

Lakini ni kwa nini rais anajaribu kupangua usimamizi wa tume hizi?

Kulingana na wakili Alutalala, rais amekuwa akitaka kulinda na kufahamu kila kinachofanyika katika idara zote serikalini kwa lengo la kuandaa mazingira yatakayomwezesha kuendesha ajenda zake kwa kasi huku akiwa amesalia na chini ya miaka miwili uongozini.

Malumbano kati ya serikali na idara ya mahakama.

Baada ya mahakama kufanya uamuzi uliosababisha kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa 2017 yaliompatia ushindi rais Uhuru Kenyatta rais alinukuliwa akiionya idara ya mahakama kwamba suala hilo ataliangazia akiwa madarakani.

Uamuzi huo wa mahakama ya juu umedaiwa kuwa chanzo cha uhusiano mbaya uliopo kati ya rais Kenyatta na Jaji mkuu Maraga anayeongoza idara hiyo ya haki na sheria.

Kwa mfano kuzorota kwa uhusiano huo kulithibitishwa mwaka jana baada ya idara ya mahakama kupokea bilioni 18 pekee kutoka katika bajeti ya serikali kati ya kitita cha bilioni 35 ilizohitaji.

Hivi majuzi Jaji mkuu David Maraga alimshutumu rais Uhuru Kenyatta kwa kukataa kukutana naye ili kujadiliana ajira za majaji 41 waliopendekezwa na tume ya mahakama. Maraga alisema kwamba hatua ya Kenyatta kukataa kuwaapisha majaji hao kumesababisha mrundikano wa kesi uliopo kwa sasa katika mahakama nyingi.

Jaji huyo alinukuliwa akisema: Wajua nakuheshimu kama rais, pia unajua kwamba nimeshindwa kukutana nawe ili kutatua masuala haya hivyobasi kuniwacha na sababu ya mbadala kutangaza yanayoendelea kwa umma, alisema.

Aliongezea: hatua ya rais kupuuza amri za mahakama sio suala zuri katika demokrasia ya katiba yetu na huenda ikasababisha machafuko, alisema Maraga.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na Naibu Rais, William Ruto
Maelezo ya picha, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na Naibu Rais, William Ruto

Kwa mujibu wa wakili Alutalala uamuzi huo wa serikali ulilenga kuidhibiti idara ya mahakama kutotoa uamuzi usioafikiana na malengo ya serikali.

Vita dhidi ya ufisadi vimeonekana kunoga naye rais Kenyatta akitaka akumbukwe kama kiongozi aliyefanikiwa kukabiliana na jinamizi hilo.

lakini je kuna ari ya kukabiliana na jinamizi hilo bila kupendelea upande fulani?

Kwa mujibu wa wakili Atulala vita dhidi ya ufisadi nchini Kenya haviwezi kufaulu bila ya kuishirikisha idara ya mahakama ilioimarika.

''Wewe unataka kukabiliana na jinamizi la ufisadi lakini upande wa pili umelemaza idara ya mahakama, je ni vipi utafanikiwa kuwakamata na kuwashtaki wafisadi na kutoa uamuzi katika wakati mwafaka iwapo mahakama haina meno ama imelemazwa'', aliuliza wakili huyo?.

Kwa mujibu wa wakili huyo shughuli yote ya kukabiliana na ufisadi imegubikwa na maswali mengi na magumu.

''Siri ni kwamba tupige ufisadi upande huu, upande mwengine kamera zione tunakabiliana na ufisadi lakini ukweli ni kwamba vita hivyo havitafika mbali maana mahakama haina uwezo''.

''Mimi ni wakili na wakati huu mahakama inateseka maana mahakimu ni wachache. Vilevile kulikuwa na mpango wa kuzibadilisha mahakama zote na kuziimarisha katika mfumo wa kidijitali lakini kufikia sasa ahadi hiyo iliowasilishwa na aliyekuwa jaji mkuu Willy Mutunga haijatekelezwa.

Kulingana na wakili huyo serikali ni ndumakuwili ambapo upande mmoja inajaribu kupigana na ufisadi lakini upande mwengine inainyonga idara ya mahakama ili vita dhidi ya ufisadi visifanikiwe.

Mbali na kwamba analipiza kisasi yaliyotokea wakati wa uchaguzi wa 2017, rais Uhuru Kenyatta pia anataka kuhakikisha kwamba ni wandani wake watakaokuwepo katika mahakama ili waweze kutoa uamuzi unaomuunga mkono mahakamani iwapo wabunge watakaidi amri yake bungeni.

Bunge na uchaguzi 2022.

Mwaka 2022 licha ya kwamba rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kung'atuka madarakani baada ya kuongoza kwa awamu zake mbili kama inavyohitajika katika katiba, maslahi yake na yale ya wandani wake pamoja na maslahi ya familia yake ni sharti yaweze kulindwa vizuri kabla hajatoka.

Maslahi hayo hayatatunzwa vizuri iwapo mrithi wake hatokuwa mtu anayemtaka kuchukua uongozi baada ya yeye kuondoka.

Ni kutokana na hatua hiyo ambapo rais amekuwa akitafuta uungwaji mkono bungeni kupitisha miswada rafiki bungeni kwa lengo la kuweka sheria anazohitaji kufanikisha malengo yake ya uchaguzi wa mwaka 2022.

Miswada hiyo ni ile ya kupitia makubaliano yake ya 'Handshake' na mwana wa 'handshake' kwa jina BBI.

Hivyobasi mabunge yoye mawili lile la seneti na lile la kitaifa ni lazima yawe chini ya wale walio na ushawishi wake.

Wakili Alutala Mukhwana anasema kwamba ni kutokana na sababu hiyo ndiposa wale wasioonekana kumuunga mkono rais Uhuru Kenyatta ndani ya chama tawala cha Jubillee wamepigwa ngwala na nafasi zao kuchukuliwa na wale walio tayari kumuunga mkono na kufanikisha ajenda zake serikalini, na pia kuamua nani atakayemrithi 2022.

Rais anataka kuendesha gurudumu la BBI kule atakako yeye.

Kwa hivyo amewang'atua wabunge na maseneta ambao wangekuwa ni pingamizi.

Hili lilihitimishwa baada ya Kiranja wa wengi katika bunge la kitaifa Emmanuel Wangwe kunukuliwa katika runinga akisema kwamba ''Sisi tunafuata amri kutoka kwa kiongozi wa chama, atakavyo yeye ndivyo tutakavyofanya sisi''.