Reza Karimi: Mshukiwa wa shambulio la kinu cha nyuklia cha Natanz atajwa Iran

The photo of the man on Iranian state television

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Runinga ya Iran imepeperusha picha hii ya mtu wanayemshuku kukihujumu kinu cha nyuklia.

Runinga ya serikali ya Iran imemtaja mwanamume ambaye vitengo vya ujasusi vinadai alihusika katika shambulio la kinu cha nyuklia cha Natanz siku chache zilizopita.

Reza Karimi alitoroka muda mchache kabla ya mlipuko huo, runinga ya Network ilisema ikionesha picha ya mtu katika kile kinachosemekana kuwa ni ya mtu anayetafutwa.

Interpol inasema kwamba haiwezi kuthibitisha kwamba bwana Karimi alikuwa miongoni mwa watu waliopo katika orodha ya watu wanaosakwa sana.

Iran imeilaumu Israel kwa kutekeleza shambulio hilo na kuimarisha mipango yake ya kinyuklia.

Isreal haijathibitisha ama kukana kuhusika kwake , lakini radio ya Umma imenukuu vyanzo vya kijasusi ikisema kwamba ni operesheni ya mtandaoni iliotekelezwa na Mossad.

Shambulio hilo lilitekelezwa muda mfupi kabla ya Iran kushiriki katika mazungumzo yanayolenga kufufua makubaliano ya kinyuklia ya 2015 na Marekani, Uingereza, China, Urusi na Ujerumani.

Makubaliano hayo yanalenga kuizuia Iran kutengeneza silaha za kinyuklia , kitu ambacho inakana kutaka kufanya.

Israel inapinga makubaliano hayo ikisema kwamba hayataizuia Iran kuwa taifa lenye nguvu za kinyuklia.

Makubaliano hayo , ambayo yaliifanya Iran kupunguza mipango yake ya Kinyuklia ,nayo ikifaidika na kuondolewa kwa vikwazo , yalikuwa hatarini kuanguka baada ya aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump kujiondoa 2018.

Hatua ya Iran kutangaza kwamba itazalisha asilimia 60 ya madini ya Uranium kufuatia shambulio hilo la Jumapili ilikuwa ukiukaji zaidi wa makubaliano hayo ya kinyuklia, ambapo inaruhusiwa kuzalisha uranium kwa asilimia 3.67 ili kutengeza Mafuta ya nyuklia yanayotumika katika vituo vya nguvu za nyuklia kutoa joto kwa mitambo ya umeme.

Je ni nini kilichofanyika Natanz?

Haijulikani jinsi shambulio hilo lilivyofanyika.

Hatahivyo , Alireza Zakani , mkuu wa kituo cha utafiti katika bunge la Iran alisema kwamba maelfu ya mashine zilizotumika kusafisha vifaa vinavyotengeneza nyuklia ziliharibiwa katika Eneo la Natanz.

Shambulio hilo lilifanyika katika kituo kimoja na kuathiri urefu wa mita 50 chini ya ardhi , alisema afisa mwengine.

Kinu cha Natanz katika picha iliyopigwa mwaka 2005

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Kinu cha Natanz katika picha iliyopigwa mwaka 2005

Siku ya Jumamosi , Runinga ya Iran ilitangaza kwamba wizara ya ujasusi ilimtambua Reza Karimi , kuwa mshukiwa wa usaliti ".

Hatua muhimu zinachukuliwa ili kukamatwa na kurudishwa nchini kupitia njia za kisheria, aliongezea. Kituo hicho cha habari pia kilionesha picha za eneo lililoharibiwa.

Lakini alipoulizwa iwapo bwana Karimi alikuwa miongoni mwa watu wanaotafutwa sana , Interpol ilikana kutoa tamko kuhusu ''watu binafsi au visa fulani''. Tovuti ya Interpol haioneshi ilani nyekundu kwa mtu yeyote kwa jina Reza Karimi.

Je mpango huo wa Kinyuklia unaweza kuokolewa?

Mazungumzo hayo yanayolenga kufufua makubaliano hayo ya kinyuklia yalioanza siku ya Alhamisi katika mji mkuu wa Austria , Vienna yameripotiwa kupiga hatua.

Hatahivyo mpatanishi mkuu wa Iran Abbas Araqchi aliambia chombo cha habari cha serikali , ''njia iliopo mbele sio rahisi na kwamba kuna mvutano mkali''.

Mataifa ya China, Urusi, Ufaransa , Uingereza , Ujerumani na Iran yote yanahusika .

Marekani haipo ijapokuwa ujumbe wake upo katika hoteli moja unapovuka barabara, kulingana na chombo cha habari cha Reuters.