Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Familia za Marais: Kutoka Tanzania ,Kenya, Cuba, hadi DRC ,hizi ndizo baadhi ya familia zilizotoa rais zaidi ya mmoja
- Author, Yusuf Jumah
- Nafasi, BBC Swahili
Uongozi wa taifa ni jukumu kubwa na nafasi za urais huwa ni wadhifa mkubwa wenye majukumu mengi na uzito wa kipekee .Ni watu wachache kote duniani ambao hupata nafasi ya kuongoza nchi zao .
Kuna wengi ambao hupigania uongozi na kote duniani kuna visa vya nchi kupigana au hata kujipata katika migogoro ya uongozi kwa sababu ya watu kutaka kuwa marais au kuziongoza nchi zao. Hata hivyo ,nafasi ya urais kwa baadhi ya watu kutoka familia chache duniani imeshikiliwa na zaidi ya mtu mmoja kutoka familia moja.
Kuna nchi ambazo zimeongozwa na Babu ,baba na mwanae kupitia utawala wa kidemokrasia au hata wa kiimla.Hizi hapa familia ambazo zimebahatika kumtoa rais zaidi ya mmoja kuziongoza nchi zao.
Tanzania/Zanzibar: Dkt Hussein Mwinyi na Ali Hassan Mwinyi / Abeid Amani Karume na Amani Abeid Karume
Ali Hassan Mwinyi alihudumu kama rais wa Zanzibar kwa mwaka mmoja kuanzia 1984 hadi 1985 kabla ya kumrithi Mwalimu Julius Nyerere na kuiongoza Tanzania kwa miaka kumi .Mwanae Hussein Mwinyi ndiye rais wa sasa wa Zanzibar . Huko Zanzibar pia familia moja imewahi kuwatoa marais wawili- Abeid Amani Karume aliyeongoza mapinduzi mwaka wa 1964 na akatawala visiwa hivyo hadi 1972 alipouawa .Mwanawe wa kiume Amani Abeid Karume aliongoza Zanzibar mwaka wa 2000 hadi 2010 .
DRC: Joseph Kabila na babake Laurent Desire Kabila
Joseph Kabila Kabange ni mwanasiasa wa DRC ambaye alihudumu kama rais wan chi hiyo kuanzia mwaka wa 2001 hadi mwaka wa 2019 . Alichukua usukani wa taifa hilo baada ya kuuawa kwa Laurent-Désiré Kabila.
Laurent-Désiré Kabila, au Laurent Kabila, alikuwa kiongozi mwanageuzi ambaye alihudumu kama rais wa tatu wa taifa hilo kuanzia mei mwaka wa 1997 alipomtimua madarakani Mobutu Sese Seko, hadi alipouawa Januari tarehe 16 mwaka wa 2001.
Gabon :Omar Bongo na mwanae Ali Bongo Ondimba
El Hadj Omar Bongo Ondimba ni mwanasiasa wa Gabon aliyekuwa rais wa pili wan chi hiyo kwa miaka 42 kutoka mwaka wa 1967 hadi kifo chake mwaka wa 2009.
Baada ya kifo chake mwanae Ali Bongo Ondimba ambaye wakati mwingine huitwa Ali Bongo alichukua usukani wa nchi hiyo Oktoba mwaka wa 2009. Baba na mwanae wameiongoza Gabon kwa jumla ya miaka 54 sasa .
Marekani: George H.W. Bush na mwanawe George W. Bush
George Walker Bush alihudumu kama rais wa 43 wa Marekani kuanzia 2001 hadi 2009 .Ni mwanachama wa Republican na kabla ya kua rais alikuwa gavana wa 46 wa Jimbo la Texas kutoka mwaka wa 1995 hadi 2000.
Baba yake rais Bush wa pili, George Herbert Walker Bush naye alihudumu kama rais wa 41 wa Marekani kati ya mwaka wa 1989 hadi 1993. Mwanae mwingine Jeb Bush amewahi pia kuwania tiketi cha chama cha Republican ili kugombea urais lakini akashindwa . Aliwahi pia kuhudumu kama gavana wa 43 wa Jimbo la Florida kutoka 1999 hadi 2007.
Cuba: Fidel Castro na kaka yake Raul Castro
Kiongozi wa Cuba Raul Castro ametangaza kwamba anajiuzulu kama rais wa taifa hilo .Lakini je,ulijua kwamba hatua hiyo itafikisha tamati uongozi wa Zaidi ya miaka 60 wa familia ya Castro? Raul ni kakake Fidel Castro ambaye aliongozataifa hilo kw amuda mrefu tangu mapinduzi ya 1959 .
Raul alichukua uongozi wa nchi hiyo kutoka kwa kakake Fidel Castro mwaka wa 2011. Fidel ndiye alieongoza Cuba katika mapinduzi hayo yam waka wa 1958 na Raul alikuwa mmoja wa viongozi wa mapinduzi hayo .
Raul mwenye umri wa miaka 89 amesema anajiondoa kama kiongozi wa chama cha kikomunisti hatua ambayo itaifanya nchi hiyo kujipata na kiongozi mpya asiyetoka katika familia ya Castro kwa miaka zaidi ya 60 sasa . Fidel alianza kuugua mwaka wa 2006 na mwaka wa 2008 alimkabidhi hatamu za uongozi kakake .Baadaye aliaga dunia mwaka wa 2016 .
Kenya:Uhuru Kenyatta na baba yake Jomo Kenyatta
Rais wa sasa wa Kenya Uhuru Kenyatta alichukua madaraka mwaka wa 2013 na kushinda muhula wa pili mwaka wa 2017/2018.Kabla ya kua rais aliwahi kuhudumu kama kiongozi wa upinzani na baadaye naibu waziri mkuu .
Babake ,Mzee Jomo Kenyatta ndiye aliyekuwa rais wa kwanza wa Kenya alipoingoza Kenya hadi mwaka wa 1978 alipofariki dunia na makamu wake Daniel Moi kuchukua madaraka . Uhuru akimaliza muhula wake mwishoni mwa mwaka wa 2022 ,baba na mwanae watakuwa wameongoza Kenya kwa jumla ya muda wa miaka 24.
Guinea ya Ikweta: Teodoro Obiang Nguema na Mjomba wake Francisco Macías Nguema
Teodoro Obiang Nguema Mbasogo ni mwanasiasa wa Guinea ya Ikweta ambaye ni rais wa pili wa nchi hiyo yangu Agosti mwaka wa 1979 . Alichukua usukani wa nchi hiyo baada ya kuipindua serikali ya mjomba wake Francisco Macías Nguema ambaye alikuwa rais wa kwanza wa taifa hilo kuanzia mwaka wa 1968 hadi 1979 alipopinduliwa na kuuawa .
Kando na mtu na mjomba wake kuwahi kuhudumu katika nafasi ya juu nchini humo , rais wa sasa Teodoro Obiang Nguema alimteua mtoto wake kiume Teodoro Nguema Obiang Mangue kama makamu wa rais mwaka wa 2012 . Hatua hiyo inamaanisha kwamba huenda Obiang Mangue akamrithi baba yake ili kuendelea kuiongoza nchi hiyo .
India: Indira Gandhi na baba yake Jawaharlal Nehru
Indira Priyadarshini Gandhi alikuwa mwanasiasa wa India ambaye alihudumu kama Waziri Mkuu wa kwanza wa India na wa pekee mwanamke hadi sasa . Alikuwa binti yake Waziri Mkuu wa kwanza wa taifa Jawaharlal Nehru.
Indira Gandhi aliuawa mnamo tarehe 31 Oktoba mwaka wa 1984 mjini , New Delhi. Aliuawa na walinzi wake wa dhehebu la Sikh Satwant Singh na Beant Singh baada ya operesheni iliyopewa jina Operation Blue Star.
Operation Blue Star ilikuwa ya kijeshi iliyoamrishwa na Indira kati ya Juni Mosi na tarehe 8 mwaka wa 1984 kumuondoa Sikh Jarnail Singh Bhindranwale na wafuasi wake kutoka hekalu takatifu la Harmandir Sahib huko Punjab.
Babake Indira ,Jawaharlal Nehru alikuwa mwanaharakati wa uhuru wa India na abaadaye akahudumu kama waziri mkuu wa kwanza wa taifa hilo kabla ya Binti yake kuiongoza nchi hiyo baadaye .
Korea Kaskazini:Familia ya Kim-Babu ,baba na Mjukuu
Iwapo kuna familia ambayo imeiongoza nchi yao kwa lazima ,basi ni familia ya Kim huko Korea kaskazini .
Kim Il-sung ndiye mwanzilishi wa taifa la Korea Kaskazini na aliongoza nchi hiyo chini ya chama cha kikomunisti kuanzia 1948 hadi kifo chake mwaka wa 1994. Baada ya kifo chake mwanae wa kiume Kim Jong-il alichukua usukani mwaka wa 1994 hadi 2011 alipoaga dunia na uongozi wa taifa hilo ukachukuliwa na Kim Jong-un ambaye bado yupo madarakani .
Chini ya utawala wake ameagiza kuuawa kwa maafisa kadhaa wanaodhaniwa kupinga uongozi wake yakiwemo mauaji ya kakake wa kambo Kim Jong-nam mwaka wa wa 2017 katika uwanja wa ndege wa Kuala Lumpar huko Malaysia
Togo: Gnassingbé Eyadéma na mwanae Faure Gnassingbé
Faure Essozimna Gnassingbé Eyadéma ni mwanasiasa wa Togo ambaye amekuwa rais wa taifa hilo la Afrika maghaibi tangu mwaka wa 2005 . kabla ya kuchukua usukani aliteuliwa na babake rais Gnassingbé Eyadéma kuwa waziri wa Madini na kuhudumu kuanzia 2003 hadi 2005 .
Kabla ya hapo rais alikuwa baba yake Gnassingbé Eyadéma kuanzia 1967 hadi alipoaga dunia mwaka wa 2005 . Alishiriki majaribio mawili ya kuipundia serikali mwaka wa 1963 na 1967 na kuwa rais Aprili mwaka wa 1967.
Canada: Justin Trudeau na baba yake Joseph Elliott Trudeau
Justin Pierre James Trudeau ni mbunge nchini Canada na amekuwa akihudumu kama waziri mkuu tangu mwaka wa 2015 . Amekuwa kiongozi wa chama cha Liberal Party tangu mwaka wa 2013.
Babake,Joseph Philippe Pierre Yves Elliott Trudeau aliyejulikana kama PET, alikuwa waziri mkuu wa 15 wa Canada kutoka mwaka wa 1968 hadi 1984 na baadaye kwa muda mfupi kama kiongozi wa upinzani kati ya mwaka wa 1979 hadi 1980
Lebanon: Rafic Al Hariri na mwanae Saad Al-Hariri
Rafic Bahaa El Deen Al Hariri alikuwa bwenyenye nchini Lebanon aliyehudumu kama waziri mkuu wa taifa hilo kutoka 1992 hadi 1998 na kwa awamu nyingine kutoka 2000 hadi 2004 alipojizulu .
Mnamo Februari 2005, Rafic Hariri aliuawa pamoja na watu wengine 21 katika mlipuko huko Beirut .
Kilo 1000 za vipulizi aina ya TNT zililipuliwa wakati msafara wa magari yake ulipokuwa ukipita karibu na hoteli St. George . Miongoni mwa waliofariki ni walinzi wake na waziri wa zamani wa Uchumi Bassel Fleihan.
Baadaye mwanae Saad El-Din Rafik Al-Hariri alihudumu kama waziri mkuu wa Lebanon mwaka wa 2009 hadi 2011 na 2016 hadi 2020. Mtoto huyo wa Hariri amekuwa akiongoza chama cha Future Movement party tangu mwaka wa 2007.