Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Thomas Sankara na Patrice Lumumba: Mashujaa waliouawa katika hali za kutatanisha
Hatua ya jopo la majaji wa mahakama ya kijeshi kwamba rais wa zamani wa Burkina Faso Blaise Compaoré, anafaa kushtakiwa kwa mauaji ya mtangulizi wake Thomas Sankara, kiongozi ambaye Compaore alimpindua mwaka wa 1987, imefungua matumaini ya uwezekano wa kupatikana kwa haki kuhusu mauaji yake .
Bw Compaoré alilikimbia kwenda mafichoni mwaka wa 2014 baada ya kufeli katiaka jaribio lake la kutaka kubadilisha sharia ili kuendeleza muda wake madarakani .Waranti ya kukamatwa kwake ilitolewa mwaka wa 2015 .
Mahakama hiyo ya kijeshi imesema jumanne kwamba rais huyo wa zamani anafaa kushtakiwa kwa 'kushambulia asasi za usalama wa kitaifa ,kuhusika na njama ya mauaji ya Sankara na kuuficha mwili wake'
Sankara, ambaye huitwa kuwa 'Che Guevara wa Afrika alipendwa sana katika nchi yake na kote barani Afrika . Uamuzi huo wa korti ya kijeshi umtarejesha tena katika mijadala mauaji Sankara na kiongozi mwingine wa bara la Afrika - Patrice Lumumba aliyekuwa na umaarufu kama wake miaka ya 60 huko DR Congo .Je,Ni nani aliyehusika na mauaji ya viongozi hao wawili ambao wanatajwa kuwa mashujaa wa bara hili na katika hali gani?
Thomas Sankara wa Burkina Faso
Marehemu rais wa Burkina Faso, Thomas Sankara - shujaa kwa vijana wengi wa Kiafrika katika miaka ya 1980 - amebaki katika kumbukumbu za wengi tangu alipouawa akiwa na umri wa miaka 37 .
Wengi hadi sasa wanamuenzi Sankara kwa njia mbali mbali wakiwemo mwanasiasa wa Afrika kusini Julius Malema kupitia kofia yake nyekundu ya kijeshi iliyotambulika kama sehemu ya vazi tajika la Sankara.
Akisifiwa na wafuasi kwa uadilifu wake na kiongozi asiye na ubinafsi, nahodha wa jeshi na mwanamapinduzi anayepinga ubeberu aliongoza Burkina Faso kwa miaka minne kutoka 1983
Lakini anaonekana na wengine kama mtu aliyeingia madarakani kupitia mapinduzi na kuthamini nidhamu juu ya haki za binadamu.
Sankara alikuwa mtetezi mkali wa vitu vyote vilivyokuzwa nyumbani - kama pamba - lakini bado tasnia ya nguo za Kiafrika ilishindwa kumfanya kuwa nembo ya T-shati.
Ingawaje Sankara anaweza kuwa sio nembo ya mapinduzi, kama Che Guevara mzaliwa wa Argentina, teksi nyingi kote Afrika Magharibi zina stika ya picha yake kwenye vioo vya bagari yao .
Ushawishi wake hata baada ya kifo unaweza kutambulika hata katika nchi za mbali na Afrika Magharibi kama vile Afrika kusini .
Uwezekano wa kushtakiwa kwa Compaoré, kwa mauaji yake huenda ukamaliza jitihada za muda mrefu za wafuasi wake kupata haki .
Mnamo Disemba tarehe 7 mwaka wa 2015 aliyeongoza mapinduzi ya septemba mwaka huo jenerali Gilbert Diendere alishtakiwa kwa njama ya mauaji ya Sankara .Alikuwa ndiye afisa wa ngazi ya juu kushatakiwa kwa mauaji ya Sankara .
Rais Sankara aliuawa na kikundi cha wanajeshi lakini hali kamili iliyozingira mauaji yake bado haijulikani .
Uchunguzi wa maiti yake uligundua kwamba mwili wake ulikuwa umechanika kwa ajili kupigwa risasi ,wakili wa familia yake alisema.
Nafasi yake kama rais ilichukuliwa na Blaise Compaore ambaye alisalia madarakani kwa miaka 27 kabla ya kuondolewa madarakani na waandamanaji mwaka wa 2014
Jenerali Diendere, ambaye baadaye alihudumu kama mkuu wa ujasusi wa Compaore alionekana kuwa mtu wa karibu sana na Sankara wakati wa mauaji yake .
Inaripotiwa alishirikiana kwa karibu na mashirika ya ujasusi ya Marekani na ufaransa na kusaidia kuachiliwa kwa mateka kutoka mataifa ya nchi za magharibi waliokuwa wakishikilia mara kwa mara na makundi ya kijihadi huko Afrika Magharibi .
Patrice Lumumba wa DR Congo
Waziri mkuu wa kwanza wa Congo aliyechaguliwa alikuwa Patrice Lumumba ambaye muda ,mfupi baadaye alikabiliwa kuvunjika kwa utaratibu na utiifu wa sheria. Kulikuwa na uasi wa jeshi wakati vikundi vya kujitenga kutoka mkoa wenye utajiri wa madini wa Katanga wakifanya harakati zao na wanajeshi wa Ubelgiji walirudi, ikidaiwa walikuwa wamekuja kurejesha usalama.
Lumumba alichukua hatua mbaya - aligeukia Umoja wa Kisovyeti kwa msaada. Hii ilileta hofu huko London na Washington, ambao waliogopa Wasoviet watapata nafasi katika Afrika kama vile walivyofanya nchini Cuba.
Katika Ikulu ya White House, Rais Eisenhower alifanya mkutano wa Baraza la Usalama la Kitaifa katika msimu wa joto wa 1960 ambapo wakati mmoja alimgeukia mkurugenzi wake wa CIA na kutumia neno "kuondolewa" kwa kile alichotaka kifanyiwe Lumumba.
CIA ilianza kufanya kazi. Ilikuja na mipango kadhaa - pamoja na kikosi maalum na dawa ya meno yenye sumu - ili kumwua kiongozi huyo wa Congo. Hayakufanyika kwa sababu ajenti wa CIA aliyekuwa Congo , Larry Devlin, alisema alikuwa anasita kuitekeleza mipango hiyo .
Lakini mnamo Januari 1961, Lumumba alikuwa amefariki.
Je, Uingereza na Marekani zilihusika na mauaji yake ? Sio moja kwa moja. Lumumba Aliendelea kukimbia, alikamatwa na kukabidhiwa kwa serikali mpya ambayo wlaijua fika kwamba ingemuua
Muaji yake yanadaiwa kutekelezwa na wapiganaji kutoka Congo pamoja na Wabelgiji na kwa usaidizi wa serikali yao ambayo ilimchukua sana .Hadi leo mauaji ya Lumumba yameghubikwa na taarifa nyingi na ukweli wa kilichotokea huenda hautajulikana hivi karibuni.