Je, Rais Samia atafanikiwa kuleta mabadiliko Tanzania bila Katiba mpya?

Chanzo cha picha, Ikulu, Tanzania
- Author, Markus Mpangala
- Nafasi, Mchambuzi, Tanzania
Rais wa wa Tanzania Samia Suluhu Hassan tangu alipokula kiapo Machi 19 mwaka huu, ilimchukua muda wa saa 41 tangu atoke kuwaongoza wananchi wake kumzika mtangulizi wake rais John Magufuli.
Machi 28 mwaka huu alitoa hotuba ambayo ilibeba ujumbe wa uteuzi,utenguzi,maagizo,kukemea na kuonesha mwelekeo wa serikali yake.
Duru za kisiasa zinabainisha kuwa mabadiliko yanayofanywa na Rais huyo yamechochea baadhi ya wananchi kupigia upatu Katiba mpya kama nyenzo ya kuondoa sheria kandamizi,ufisadi,matumizi mabaya ya madaraka,upotevu na ubadhirifu wa fedha,kukosa uwazi katika ripoti,marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa na Asasi za Kiraia,uhuru wa vyombo vya habari,uhuru wa wanataaluma,Tume Huru ya Uchaguzi pamoja na kuondoa ukimya na utatanishi ulipo kwenye Katiba ya sasa ni miongoni mwa masuala yanayojadiliwa nchini humo.
Mathalani akizungumza wakati wa kupokea ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Mashirika ya umma (CAG) Machi 28 mwaka 2021, Rais Samia alizielekeza Ofisi ya CAG na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) kuchunguza mifumo ya malipo ya fedha.
"Nizungumzie kuhusu mifumo ya malipo. Nimeomba Takukuru na CAG hebu kaeni angalieni maana ndani ya serikali kuna mifumo zaidi ya sita inayotumika kukusanya mapato sehemu mbalimbali. Naomba mkaangalie 'harmonization' ya hii mifumo. Tuangalie ndani ya serikali ni mifumo gani itatumika na ukusanyaji wake ukoje. Kwa sababu mifumo ikiwa mingi inatoa mwanya wa kupoteza mapato. Huyu kutumia mfumo huu na yule kutumia mfumo huu".

Chanzo cha picha, Maelezo
Matamshi yanayofanana na hayo yamewahi kutolewa na marais waliopita wakati wa kupokea ripoti kama hizo, lakini pamekuwa na ugumu kukomesha-ikiwa na maana kuchunguza pekee na kutoa mapendekezo mfumo wa malipo mpya au wa aina moja hakuwezi na mengine yanayofanana nayo hayawezi kulisaidia taifa hilo kama halitakuwa tayari kuanzisha mchakato wa Katiba mpya wenye madhamuni ya kubadili mifumo ya utawala na sheria zitakazoimarisha taasisi na maisha ya wananchi wake.
Je, wabunge kupingana kuhusu hoja ya Katiba mpya ina maana gani?
Machi 30 mwaka 2021 Bunge la Jamhuri ya Muungano lilishuhudia dalili za kurudi mchakatoni kutokana na hoja za wabunge wawili waliokinzana wakati wa vikao.
Mbunge wa Viti Maalumu kutoka chama cha upinzani Chadema, Sophia Mwakagenda alisema Rais Samia Suluhu anapaswa kutibu majeraha yaliyotokana na uchaguzi uliopita kwa kuwaachilia huru wafungwa wote wa kisiasa na kuendelea na mchakato wa Rasimu ya Katiba mpya ya Jaji Warioba.
Hoja ya Mbunge Mwakagenda ilipingwa na Mbunge wa Viti Maalumu wa chama tawala CCM, Munde Tambwe ambaye alieleza bungeni hapo kuwa hayati rais John Magufuli na rais wa sasa Samia Suluhu kwenye mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2020 walinadi maendeleo na kusisitiza kuwa viongozi hao hawakutoa ahadi ya Katiba mpya.
Aidha, kwa nafasi aliyonayo sasa yenye mamlaka makubwa kwa nchi hiyo na alikotoka kisiasa ni dhahiri Rais Samia ni kiongozi 'anayenukia' mchakato wa Katiba mpya.
Yeye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba akiwa chini ya Uenyekiti wa hayati Samwel Sitta, Mbunge wa zamani wa Urambo mkoani Tabora na Spika wa zamani wa Taifa hilo (2005-2010).
Mchakato huo ulikoma mwaka 2014 kwa mgawanyiko wa wapinzani wakiunga mkono Rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba huku chama tawala CCM kiliunga mkono Katiba Pendekezwa ya Kamati ya Andrew Chenge.

Chanzo cha picha, Ikulu, Tanzania
Muundo wa Bunge la Katiba kipindi hicho ulitaka viongozi wa juu watoke katika pande mbili za muungano na kwa vile Mwenyekiti alikuwa ni hayati Samuel Sitta kutoka Tanzania Bara, hivyo nafasi ya Makamu Mwenyekiti iliangukia kwa Mzanzibari Samia Suluhu Hassan.
Usuli unaonesha kuwa Rais Samia akiwa mgombea mwenza wa tiketi ya chama cha CCM alishiriki kikamilifu kunadi na kuahidi kuendelezwa mchakato wa Katiba mpya kupitia mikutano ya kampeni ya uchaguzi mkuu akitumia ilani ya chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita (2015-2020).
Vilevile katika hotuba ya hayati John Magufuli wakati akifungua Bunge la 11 alisisitiza kuendelezwa kwa mchakato wa katiba mpya katika kipindi chake cha kwanza cha miaka mitano (2015-2020).
Hata hivyo hadi kukumilika kwa ngwe ya kwanza ya uongozi wao suala hilo hawakuendeleza mchakato wa Katiba mpya.
Aidha, wakati wa kunadi sera za CCM kwenye uchaguzi mkuu uliopita ilishuhudiwa chama hicho kiupiga teke mchakato huo baada ya kuondolewa kuwa miongoni mwa vipaumbele ndani ya Ilani ya uchaguzi kwa kipindi cha mwaka 2020-2025.
Kwenye mikutano ya kampeni ya urais,ubunge na udiwani si John Magufuli wala Samia Suluhu hawakujihusisha na ahadi za kuendelezwa mchakato wa Katiba mpya.
Si wagombea wa ubunge wala udiwani au timu ya kampeni za uchaguzi mkuu a CCM ambazo zilitamka lolote kuhusu kuendelezwa mchakato wa katiba mpya. Mchakato ni kama ulipigwa teke.

Chanzo cha picha, Ikulu
Je ni utatanishi upi uliojitokeza kwenye Katiba ya sasa?
Katiba ndio muongozo na uhai wa taifa lolote duniani. Inapotokea Katiba haisemi au kuzungumzia jambo kinagauba au kuonesha upungufu wa aina yoyote ni ishara kuwa ni utatanishi hivyo kuhitajika marekebisho ikizingatiwa Tanzania huongozwa na binadamu ambao wanaweza kupatwa na matatizo yoyote.
Duru za kisheria zinabainisha kuwa maeneo yafuatayo yanaleta utatanishi kwa kuzingatia mchakato wa kukabidhiwa madaraka wa Rais Samia:
- Mosi, Rais hakumteua waziri mkuu ndani ya siku 14 kama Katiba inavyoeleza Ibara ya 57(2) mara baada ya kuapishwa kulingana na agizo la muundo wa Baraza la Mawaziri na Serikali.
- Pili,kwa mujibu wa Ibara ya 54 wajumbe wa Baraza la Mawaziri ni Makamu wa rais,Waziri Mkuu,Rais wa Zanzibar na mawaziri wote. Hata hivyo Rais Samia alikaa kikao na baraza la mawaziri pasipo kuwepo Makamu wa Rais kama takwa la katiba lilivyo.
- Tatu, Katiba ya sasa inasema Rais atashauriana na waziri mkuu kuunda Baraza la Mawaziri, lakini waliopo sasa kwa asilimia kubwa 'wamerithiwa' kutoka kwa hayati Magufuli.
- Nne, Katiba ya sasa haisemi lolote kuhusu muda ambao anatakiwa aunde baraza la mawaziri baada ya kuingia madarakani hata baada ya uchaguzi mkuu.
- Tano, Katiba ya sasa inasema rais mteule anapoingia mdarakani na uteuzi wa Mwanasheria mkuu wa serikali unakoma Ibara 59(5b), ikiwa na maana anatakiwa kuapishwa tena kama rais mpya atataka kuendelea naye.
- Sita, baadhi ya mawaziri wa Rais Samia walikula kiapo chini ya utawala wa hayati John Magufuli si Rais Samia.
- Saba, Katiba haielezi Rais mteule atachukua muda gani kuunda Baraza la Mawaziri. Ikumbukwe hayati Magufuli alitumia takribani siku 30 kuunda Baraza la Mawaziri baada ya uchaguzi wa mwaka 2020 ambapo aliawaapisha Mwanasheria mkuu,Waziri wa mambo ya nje na Waziri wa Fedha na Mipango pekee. Pia mwaka 2015 ilimchukua siku nyingi hadi kutangaza baraza la mawaziri, kwa vile hakubanwa na muda ambao kimsingi ilibidi utajwe kwenye katiba.
- Nane, Rais amepewa mamlaka ya kuvunja Baraza la Mawaziri, lakini hajavunja.
- Tisa, Ibara ya 37(5) ya Katiba ya sasa haisemi ni muda gani wa Makamu wa Rais ataapishwa kushika wadhifa wa Rais mara baada ya kutokea kifo mfano cha hayati Magufuli.
Je, itakuwa ajenda ya kuwabeba wapinzani?
Umoja wa Katiba ya Wananchi wa vyama vya upinzani (UKAWA) uliibuka kutokana na minyukano ya kimaslahi ya siasa huku ukinasibu kutetea maoniya wananchi, na ndio waliosikilizwa zaidi kuliko serikali na chama na tawala.
Uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 vyama vya siasa vya ACT Wazalendo, Chadema, NCCR Mageuzi kupitia ilani zao na mikutano ya kampeni vyote vilinadi kurejesha mchakato wa katiba mpya kupitia Bunge la Katiba.
NCCR Mageuzi walieleza kuwa iwapo wangeshinda wangehakikisha wanaitisha muafaka wa kitaifa ili kutengeneza matakwa na kupatikana kwa katiba mpya ya Tanzania.
Wakati serikali ya awamu ya nne chini ya rais Jakaya Kikwete ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa CCM ilipoanzisha mchakato wa Katiba mpya suala hilo halikuwa miongoni mwa sera za chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010-2015.
Hata hivyo shinikizo la wananchi, wanazuoni, wanaharakati,wadau wa maendeleo lilichangia pakubwa kushuhudia uongozi wa Kikwete kuanzisha mchakato huo.
Vyovyote itakavyokuwa upepo wa mchakato wa katiba mpya utabaki kuwa ajenda ya vyama vya upinzani kama sehemu ya kunyukana kisiasa na chama na serikali iliyopo madarakani. Kukinzana kwa wabunge wawili tajwa ni ishara ya awali kuelekea kwenye mnyukano halisi.
Haifahamiki namna CCM na serikali ya Rais Samia itachukua hatua gani au itatafsiri vipi upepo huo ikiwa utavuma kwa kasi na kupokelewa vizuri kwa mara nyingine wananchi wa Tanzania.
Wanasiasa wa vyama vyote, tawala na upinzani wanaonekana kumsoma kwanza rais mpya Samia Suluhu kabla ya kutumbukiza miguu yao kwenye utawala wake huku mchakato wa Katiba ni miongoni mwa mambo yatakayoibuliwa.
Upepo wa sasa unaonekana kumwendea vizuri Rais Samia kwa sababu wanasiasa wa vyama vyote wamefurahishwa na mwenendo wake wa awali kupitia hotuba kadhaa alizozitoa zikidaiwa kujaa mamlaka,diplomasia na kuunganisha Taifa hilo pamoja na mwanzo wa muundo wa serikali yake.
Hata hivyo Wanasiasa kwa asili wakimaliza kusoma mtindo wa mtawala wao kwa kawaida huanza mizungu na kupenyeza ajenda zao. Huko ndiko uliko uwezekano wa kuzaliwa UKAWA ya pili katika madai ya katiba mpya.














