Namna Rais Samia anavyotumia mitandao ya kijamii

Chanzo cha picha, IKULU YA RAIS TANZANIA
- Author, Ezekiel Kamwaga
- Nafasi, Mchambuzi
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Miaka 20 au 30 iliyopita, haikuwa kazi rahisi kuwafahamu viongozi wakubwa kama wafalme na marais kuliko kile ambacho kingezungumzwa na vyombo vya habari.
Shukrani kwa mitandao ya kijamii kama Facebook, Twitter na Instagram - wananchi sasa wanaweza kufahamu walau kidogo kuhusu viongozi.
Wanaweza kuwafahamu ni akina nani ni marafiki wa viongozi wao, familia zao? Mambo wanayoyapendelea, vitabu wanavyosoma na mwelekeo wao wa kiitikadi au mtazamo kuhusu sera na masuala muhimu ya kitaifa na kimataifa.
Wakati Watanzania wakiwa wameingia katika awamu mpya ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ni wakati mwafaka sasa kufahamu maisha ya mitandaoni ya mwanamke huyu wa kwanza kuwa Rais wa Tanzania yanatuonyesha nini.
Kusema ukweli, huwezi kupata mengi kumhusu Samia kupitia akaunti zake za mitandaoni. Kama walivyo viongozi wengi wa Tanzania - hususani watangulizi wake katika ofisi yake mpya; mitandao ya kijamii hutumika tu kama shajara (diary) ya matukio ya kila siku ya viongozi.
Mara moja moja, Samia huweza kutoa pole kwa wafiwa au manusura katika ajali au kutoa salamu za heri ya siku ya kuzaliwa kwa viongozi. Na hivi ndivyo Jakaya Kikwete na hayati John Magufuli - marais wengine wa Tanzania waliokuwa na akaunti kwenye mitandao ya kijamii, walivyokuwa wakitumia mitandao hiyo.
Huo ni upande mmoja tu wa habari. Pamoja na hayo, bado akaunti za Rais kwenye mitandao ya kijamii vinatueleza vitu kuhusu yeye kama ambavyo tutaona baadaye kwenye mitandao ya kijamii.

Viongozi na mitandao ya kijamii
Yanapozungumzwa masuala ya viongozi na mitandao ya kijamii, hakuna kiongozi anayetajwa kumzidi Rais wa 44 wa Marekani, Barack Obama. Yeye ndiye kiongozi anayefuatiliwa na watu wengi zaidi duniani akiwa na wafuasi zaidi ya milioni 130 duniani.

Obama aliingia rasmi Twitter mnamo Aprili, 2007 na tangu wakati huo hajawahi kupumzika. Mwaka 2015, aliweka rekodi ya Ikulu ya Marekani kuwa na akaunti binafsi kwa ajili ya Rais wa Marekani (@POTUS) ambayo sasa inatumiwa na Rais Joe Biden baada ya kutumiwa pia na Donald Trump.
Kama ambavyo Rais John F. Kennedy wa Marekani hujulikana kwa kuitwa Rais wa kwanza wa televisheni, Obama hujulikana pia kama Rais wa kwanza wa mitandao ya kijamii.
Baada ya Obama kutumia kwa faida na nguvu mitandao hiyo, sasa jambo la ajabu ni kwa Rais kutokuwa na akaunti hasa kwenye mtandao wa twitter ambao hutumiwa zaidi na viongozi kuwasiliana na watu wao.

Samia anamfuata nani mitandaoni?
Kwenye yake binafsi ya twitter, Samia anafuata watu 27 tu na unapata picha hasa kuhusu ni watu wa aina gani ambao yeye hupenda kupata habari zao.
Miongoni mwa wanasiasa wa Tanzania, kuondoa hayati Rais John Magufuli, ni wanasiasa watatu tu ambao Rais huyu wa sita wa Tanzania anafuatilia habari zao. Wanasiasa hao ni Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Mbunge wa Bumbuli, January Makamba na Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye.
Akaunti hiyo ya Rais Samia pia inaonyesha hamfuati kiongozi yeyote miongoni mwa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Miongoni mwa watumiaji mashuhuri wa mtandao huo ni marais Uhuru Kenyatta wa Kenya na Paul Kagame wa Rwanda lakini wao hawajamfuata Samia naye hajawafuata bado.
Hata hivyo, uchambuzi wa haraka wa watu anaowafuatilia Samia unaonyesha ni mtu anayefuatilia habari za wanawake mashuhuri na taasisi zinazojihusisha na masuala ya watu wa jinsia hiyo.
Viongozi kadhaa wa kike waliompongeza Rais Samia baada ya kuchukua hatamu.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe, 1
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe, 2
Katika twitter, Samia anamfuata mke wa Obama, Michelle, mtangazaji mashuhuri wa vipindi vya televisheni wa Marekani, Oprah Winfrey, mwanasiasa Hillary Clinton, Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris (ambaye tayari amemtumia Samia salamu za pongezi kufuatia kuwa kwake Rais wa Tanzania) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Wanawake.
Miongoni mwa viongozi wa bara la Afrika, Samia anamfuata kiongozi mmoja tu; Ali Bongo Ondimba ambaye ni Rais wa Gabon.
Mtu mwingine ambaye anafuatwa na Samia ni mtawala wa Dubai, Sheikh Mohamed bin Rashid al Makhtoum. Ndiye mtu pekee kutoka Mashariki ya Kati ambaye Rais huyu mpya wa Tanzania anamfuata kupitia mtandao huo.
Pamoja na ukaribu wake na kufahamiana na wasanii, Samia hamfuati mwanamuziki, mwigizaji au mtu yeyote anayejihusisha na masuala ya Sanaa na burudani ndani ya Tanzania au nje ya nchi.
Wakati Samia anatangaza kuwa Rais Machi 17 mwaka huu kufuatia kifo cha Magufuli, alikuwa na wafuasi 416,000 kwenye mitandao ya kijamii lakini kufikia Machi 26 mwaka huu, alikuwa na wafuasi 474,000, hili ni ongezeko la watu 58,000 katika kipindi cha takribani siku 10 tu.

Chanzo cha picha, MKURUGENZI WA MAWASILIANO AFISI YA RAIS TANZANIA
Nchini Tanzania, Mama Samia yuko nyuma ya wanasiasa kama Kikwete mwenye wafuasi milioni 1.5, Zitto Kabwe mwenye wafuasi milioni 1.2 na January Makamba mwenye wafuasi milioni moja.
Hata hivyo, kwa cheo chake kipya, mwamko wa Watanzania kwenye matumizi ya mitandao ya kijamii na shauku ya watu duniani kote kutaka kujua Rais mwanamke wa Afrika anafanya nini, Samia ana fursa ya kuwapiku wanasiasa hao katika kipindi cha miaka michache ijayo.
Kwa kutazama aina ya watu anaowafuata Samia, ni rahisi kuona kwamba ni mwanasiasa anayefuata mwelekeo wa kiliberali na anavutwa zaidi na siasa za kimagharibi kuliko Mashariki.
Kwa kufuata watu kama Michelle, Hillary na Oprah, akaunti hii binafsi ya Samia inamuonyesha kama mwanasiasa anayeamini katika nguvu ya wanawake na kwenye kuvunja vikwazo dhidi yao.
Kwa mwanasiasa ambaye anawaita viongozi wa EAC na nchi za Jumuiya ya Uchumi ya Kusini mwa Afrika (SADC) kaka zake - kama alivyowaita wakati wa tukio la msiba wa kitaifa wa Magufuli uliofanyika Dodoma, inashangaza kwamba hamfuati yeyote miongoni mwa viongozi wa nchi hizo na badala yake anamfuata Ondimba wa Gabon.

Tahadhari ya mitandao
Pamoja na uzuri wa mitandao ya kijamii katika kutoa taarifa na kubadilishana maarifa, kumekuwa pia na hatari za kutumia mitandao hiyo. Kwa mfano iko hatari ya kuingiliwa na wakorofi na kuweka picha au habari zisizofaa.
Lakini, tatizo kubwa zaidi la mitandao ya kijamii liko katika aina ya watu wanaoitumia. Wapo watu ambao hutumia mitandao hiyo kukashifu, kubagaza na kutukana viongozi na mwanasiasa anayeingia katika dunia hii ni muhimu akawa na ngozi ngumu.
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ni miongoni mwa waliowahi kuonja joto hii ya jiwe kutoka kwa watu wa mitandaoni kiasi kwamba kuna wakati - Novemba mwaka jana, aliamua kujitoa akieleza kwamba amechoshwa na matusi anayotukanwa.
"Hata twitter niliondoka huko nikaona hiyo kitu ni bure, ni matusi tu. Unakaa hapo unasoma hulali. Afadhali nilale nipige story na mama (mkewe, Margareth) niende kufanya kazi," alisema Uhuru.

Chanzo cha picha, TWITTER/@SULUHUSAMIA
Je, Samia atakuwa Obama au Magufuli kwenye mitandao?
Baada ya kuwa Rais, sasa utakuwa uamuzi wake mwenyewe kuamua kama akaunti zake za mitandao ziwe hai na zenye kufuatiliwa kwa kuwekwa taarifa mpya kila wakati au kuendelea kutumika kama shajara tu ya ziara zake.
Mtangulizi wake, Magufuli, alikuwa pia akitumia mitandao kama shajara na mara moja moja kutuma salamu za pole au pongezi kwa watu binafsi, makundi au taasisi zilizofanya vizuri au kupatwa na majanga.
Kama atafuata utaratibu wa Marekani, Samia anaweza kuzifanya akaunti zake kuwa sehemu yake si ya kuonyesha nini anachofanya kazini kila siku - lakini pia kutoa mtazamo wake binafsi kuhusu matukio yanayoendelea duniani na kujichanganya na watu wa kawaida katika mijadala mbalimbali.
Kama kuja jambo halijaeleweka vizuri au ni gumu kueleweka, Rais anaweza kutumia mitandao kulifafanua kwa maneno machache na lugha nyepesi na kama kuna jambo ambalo serikali yake inalifanya na hakuna maelezo ya kueleza kwa nini mwelekeo huo umechukuliwa, anaweza pia kutumia nafasi hiyo kueleza.
Kwa vyovyote vile, kuna kila dalili kwamba akaunti za mitandao ya kijamii za Rais Samia Suluhu Hassan hazitakuwa kama zilivyokuwa zamani mara baada ya kukaa na kuzoea wadhifa wake mpya.
Obama alizindua akaunti yake ya Rais wa Marekani (@POTUS), kwa kurusha kijembe kwa swahiba wake, Hillary Clinton.
Tutarajie kitu kama hicho kwa Rais Samia kuelekea kwa kaka zake wa EAC, SADC au kwa msanii maarufu kama Diamond Platnumz kama namna yake ya kujitambulisha rasmi kuingia katika kundi hili maalumu?
Tusubiri.












