Virusi vya Corona: Mgombea wa urais kutoka upinzani Congo afariki kutokana na Covid 19

Guy Brice Parfait Kolelas, mmoja wa wagombeaji wakuu wa urais katika taifa la Congo-Brazzaville

Chanzo cha picha, Getty Images

Mgombea wa urais wa Upinzani nchini Congo - Brazaville amefariki dunia kwa ajili ya Covid 19Guy Brice Parfait Kolelas, mmoja wa wagombea wakuu wa urais katika taifa la Congo-Brazzaville amefariki dunia siku ya Jumapili saa chache baada ya kukamilika kwa shughuli ya upigaji kura nchini humo .

Mkurugenzi wa kampeini yake ameliambia shirika la AFP kwamba Kolelas " aliaga dunia akiwa katika ndege ya matibabu iliyokuja Brazaville kumchukua siku ya jumapili'

Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 61 alikuwa amepatikana na virusi vya Corona siku ya Ijumaa ya mwisho ya kufanya kampeini .

Uchaguzi wa Jumapili uliendeshwa kwa njia shwari lakini ni wapiga kura wachache waliojitokeza kushiriki uchaguzi huo kulingana na waangalizi .

Alikuwa mmoja wa wagombeaji sita wa upinzani waliokuwa wanawania kiti hicho dhidio ya rais Sassou Nguesso.

Siku moja kabla ya uchaguzi picha ya video ilichapishwa ikimuonyesha bwana Kolelas akiwa mnyonge lakini akiwamiza wapiga kura kujitokeza kushiriki zoezi la upigaji kura .

Bwana Kolelas alikosa hafla yake ya mwisho ya kampeni Ijumaa baada ya kusema siku moja mapema kwamba anahofia alikuwa na malaria, shirika la habari la Associated Press linaripoti.

Alilazwa katika hospitali ya kibinafsi katika mji mkuu, Brazzaville, na baadaye ilithibitishwa kuwa alikuwa na Covid-19.

Akiongea kwa Kifaransa kutoka kitandani mwake hospitalini, Bwana Kolelas alisema: "Ndugu zangu wapendwa, nina shida.

Ninapambana na kifo. Walakini, ninawauliza jitokezeni na kupiga kura kwa mabadiliko. Nisingepigania bure."Mkuu wa timu ya serikali ya kupambana na Covid-19, Elira Dokekias, alisema kuwa hali ya Bwana Kolelas ilikuwa mbaya Jumamosi, Associated Press inaripoti.

Hali yake ilikuwa thabiti siku ya Jumapili kwa yeye kuhamishiwa kwenye kitengo cha coronavirus katika hospitali ya chuo kikuu huko Brazzaville, na angepelekwa nje ya nchi kwa matibabu, Dkt Dokekias alinukuliwa akisema.

Baada ya kupiga kura katika mji mkuu, Bwana Sassou Nguesso alimtakia afueni ya haraka Bw Kolelas.

Umati mkubwa wa watu ulikusanyika kumuona rais, na watu wengi hawakuvalia barakoa na wengi walipuuza kanuni za kupambana na Corona.

Bwana Sasou Nguessou alimshinda Bw Kolelas katika uchaguzi uliopita wa mwaka wa 2016, akipata asilimia 60 ya kura ikilinganishwa na 15% za mpinzani wake.

Kampuni inayofuatilia matumizi ya mitandao NetBlocks iliripoti kwamba huduma za intaneti zilizimwasiku ya jumapili kabla ya upigaji kura .

Chama kikubwa cha upinzani the Pan-African Union for Social Democracy (UPADS), kilisusia uchaguzi huo kikisema kinahofia kura hiyo italigawanya taifa Bwana Sassou Nguesso amekuwa madarakani tangu 1979, isipokuwa kipindi cha miaka mitano baada ya kushindwa uchaguzi mnamo 1992.

Congo-Brazzavile imerekodi rasmi zaidi ya visa 9,000 vya Covid 19 na vifo 130.

Bwana Kolela ambaye ni waziri wa zamani wa uvuvi ni mwanawe waziri mkuu wa zamani .