Tyler Perry: Tajiri wa Marekani aliyewapa makao Meghan na Harry nyumbani kwake

Harry na Meghan walihojiwa na Oprah Winfrey

Chanzo cha picha, CBS

Maelezo ya picha, Harry na Meghan walihojiwa na Oprah Winfrey

Katika mahojiano yao na Oprah Winfrey, Duke na Duchess wa Sussex wamesema wazi kwamba baada ya kusitishwa kwa ufadhili wao na Familia ya Kifalme - tajiri wa Marekani Tyler Perry ndiye aliyewapa hifadhi ya makao na ulinzi katika eneo la California mwaka 2020.

Lakini je, Tyler Perry ni nani na alifanikiwa vipi maishani?

Ni mtengenezaji filamu mashuhuri, 51, mchekeshaji, mwigizaji, mzalishaji wa vipindi na mtunzi.

Filamu zake na vipindi vya kwenye televisheni ndio chanzo cha kumfanya kuwa mmiliki wa nyumba Marekani hasa miongoni mwa Wamarekani Waafrika.

Bwana Perry anafahamika sana kwa filamu zake za Madea alizoandika, akazisimamia, mwelekezi na aliyeshiriki kama mhusika mkuu, mwanamke mzee anayetumia viungo bandia.

Mwaka 2015, alijenga studio yake katika kipande cha ardhi cha ekari 330 nje ya eneo la Atlanta, Georga.

Mwaka jana alikuwa bilionea, kulingana na jarida la Forbes.

Pia aligonga vichwa vya habari miezi michache alipoweka wazi kwamba anapitia changamoto za kimaisha, akitangaza kuwa ameachana na mchumba wake wa muda mrefu, na mama ya mtoto wake mmoja, Gelila Bekele.

"Nina miaka 51, sina mchumba na najiuliza ukurasa wangu wa maisha unaofuata utakuwaje. Haijalishi vile hali itakavyokuwa, nitasimama na Mungu, nitakuwa baba mzuri kadiri ya uwezo wangu, na kujitahidi kwa kila namna!!" Bwana Perry aliandika katika ukurasa wake wa Instagram.

"Katika dunia yenye huzuni nyingi, tafadhali jitahidi kuwa mzuri!"

Perry aliwasaidia vipi Harry na Meghan?

Bwana Perry alijitolea kuishi na wanandoa hao - bure - katika moja ya majumba yake ya kifahari na kutuma ulinzi wake walipokuwa wanahama kutoka Canada hadi Los Angeles mwaka 2020, Mwanamfalme Harry na Meghan walisema hivyo katika mahojiano yao maalum na shirika la habari la CBS nchini Marekani Jumapili.

Wanandoa hao walisema waliamua kuondoka baada ya eneo la nyumba waliokuwa wanaishi kisiwa cha Vancouver, magharibi mwa Canada kufahamika na watu wengi.

"Hatukuwa na mpango wowote," Meghan amesema katika mahijiano.

"Tulihitaji nyumba na [Tyler Perry] alijitolea kutusaidia na maafisa wake wa ulinzi pia na hilo likatupatia fursa ya kupumua na kufikiria hatua tutakayochukua."

Tyler Perry hajatoa tamko lake kwanini aliamua kumsaidia Meghan na Harry

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Tyler Perry hajatoa tamko lake kwanini aliamua kumsaidia Meghan na Harry

"Wasiwasi mkubwa ulikuwa ni kwamba wakati tuko Canada, katika nyumba ya mtu mwingine, niliarifiwa kwamba ulinzi utaondolewa ndani ya kipindi kifupi," Harry amesema.

"Ghafla ikanijia akilini kwamba: 'Nikafikiria kwa haraka, mipaka inaweza kufungwa, ulinzi wetu utaondolewa, na hakuna anayejua hatua ya kufungiwa itaendelea kwa muda gani, dunia inajua tuko wapi, sio salama, na bila shaka tutahitajika kuondoka hapa.'"

Harry na Meghan walisema kwamba baadaye, waliamua kwenda kuishi California, na kununua nyumba Montecito.