Mzozo wa Tigray Ethiopia: 'Nimepoteza mkono wangu mwanajeshi akijaribu kunibaka'

A Photoshopped image showing a woman covering her face and holding up her other hand

Chanzo cha picha, Getty Images

Tahadhari: Baadhi ya watu huenda wakaona taarifa hii kama yenye kuumiza moyo.

Mwanafunzi mmoja nchini Ethiopia ameliambia shirika la BBC kuwa alipoteza mkono wake wa kulia akijitetea dhidi ya mwanajeshi aliyekuwa anajaribu kumbaka - ambaye pia alikuwa amemlazimisha babu yake kufanya naye mapenzi.

Mwanafunzi huyo, 18, ambaye kwasababu za kiusalama jina lake limehifadhiwa, amelazwa hospitalini kaskazini mwa Ethiopia eneo la Tigray kwa zaidia ya miezi miwili akiendelea kupata matibabu kutokana na masaibu yaliomkuta.

Mgogoro wa Tigray, ambao ulianza Novemba 2020 wakati Waziri Mkuu Abiy Ahmed alipoanzisha mashambulizi dhidi ya chama tawala eneo hilo cha TPLF baada ya wapiganaji kuteka kambi za jeshi za serikali, umedidimiza ndoto za wengi na idadi kubwa ya walioathirika ikiwa ni wanafunzi wa darasa lake.

Wengi wao pamoja na familia zingine katika mji huo wametoroka makazi yao na kuelekea maeneo ya milimani - baada ya Bwana Abiy, mshindi wa tuzo ya Nobel, kutangaza ushindi kufuatia kuchukuliwa kwa mji wa Mekelle, eneo la Tigray na wanajeshi wa serikali Novemba 29.

Hii ni kwasababu vikosi vya usalama vilianza operesheni ya kutafuta wanachama wa TPLF waliokataa kujisalimisha ambako kumechangia kutokea kwa madai ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya wakazi wa Tigray. Hata hivyo, mamlaka imekanusha madai hayo.

Msichana wa shule na babu yake walisalia nyumbani kwao katika mji wa Abiy Addi, takribani kilomita 96 magharibi mwa mji wa Mekelle, kwasababu ilikuwa vigumu kwao kupata usafiri.

Mountain canyon landscape, with rock formations and valley, in Tigray in northern Ethiopia

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Watu wengi wametoroka eneo la Tigray na kukimbilia maeneo ya milimani wakati wa vita

Desemba 3, kijana mmoja alisema mwanajeshi aliyekuwa amevaa nguo za kijeshi za Ethiopia aliingia kwenye nyumba yao akitaka kujua wapiganaji wa Tigray wako wapi.

Baada ya kusaka nyumba hiyo na kutoona yeyote, aliwaagiza kulala chali kitandani na kuanza kupiga risasi maeneo ya karibu nao.

"Kisha akamuagiza babu yangu afanye mapenzi nami. Babu yangu alikasirika sana na… wakaanza kupigana," mwanafunzi huyo anasema.

Ameongeza kuwa mwanajeshi huyo alimtoa babu yake nje na kumpiga risasi mabegani na mapajani kisha akarejea ndani kwa msichana huyo, huku akisema kuwa amemuua.

"Alisema: 'Hakuna anayeweza kukunusuru. Vua nguo zako.' Nilimuomba mara kadhaa asinifanyie hivyo lakini akanipiga ngumi mara kadhaa."

Mvutano wa wawili hao uliendelea kwa dakika kadhaa - ingawa alihisi anashindwa nguvu na ngumi anazopigwa - na mwisho wake mwanajeshi huyo alishikwa na hasira na kumuonesha bunduki.

"Alinipiga risasi mkono wangu wa kulia mara tatu. Alinipiga risasi mguuni mara tatu. Akaondoka baada ya kusikia mlio wa risasi nje."

Kumbe babu yake bado alikuwa hai ingawa alikuwa amepoteza fahamu na kwa siku mbili zilizofuata walisalia na uoga licha ya kwamba wamejeruhiwa vibaya nyumbani kwao, walikuwa na hofu kiasi cha kuogopa hata kuomba msaada.

'Hakuna haki kabisa'

Akaunti ya msichana huyo kijana inaunga mkono wasiwasi juu ya madai ya ubakaji huko eneo la Tigray yaliyooneshwa na Pramila Patten, mjumbe wa Umoja wa Mataifa anayeangazia unyanyasaji wa king'ono katika migogoro.

Anasema kuwa "kuna taarifa za kuogofya za watu wanaodai walilazimishwa kubaka watu wa familia zao wakati vitisho vya kutokea kwa vurugu zaidi vikiendelea.

"Baadhi ya wanawake inasemekana wamelazimishwa kufanya mapenzi na wanajeshi kwa mabadilishano ya bidhaa za msingi, huku vituo vya afya vimeonesha ongezeko la uhitaji wa dawa za dharura za kuzuia mimba na kupimwa kwa maambukizi ya virusi vya ukimwi, hatua ambayo mara nyingi huwa ni kiashiria cha unyanysaji wa kingono katika mapigano."

Wanawake wengi walibakwa katika eneo la Mekelle. Hili linafanywa kwa maksudi kuvunja maadili ya watu, kuwatishia maisha na kuwachochea kuachana na vita."

Vyama vya upinzani eneo la Tigray vimesema mauaji ya kiholela na visa vya ubakaji vimekuwa "jambo la kawaida", pia vimerejelea kisa cha baba aliyelazimishwa kumbaka binti yake akiwa ameshikiwa bunduki.

Daktari na mwanachama wa makundi ya haki za wanawake - ambao wote hawako tayari kutambulishwa - wameifahamisha BBC mnamo mwezi Januari kwamba wamesajili takriban wasichana 200 walio chini ya umri wa miaka 18 katika hospitali mbalimbali na vituo vya afya huko Mekelle ambao walisema kwamba wamebakwa.

Wengi wao wanasema waliotekeleza unyama huo walikuwa wamevaa sare za jeshi la Ethiopia - na baada ya hapo walionywa dhidi ya kutafuta matibabu hospitalini.

"Wana michubuko. Baadhi yao wamebakwa. Mmoja wao alizuiliwa na kubakwa kwa kipindi cha wiki moja. Imefika wakati hata hajitambui tena.

Na hakuna polisi, bila shaka hakuna haki," daktari alisema.

Mwanaharakati wa haki za binadamu amesema: "Pia tumesikia taarifa kama hizo za kushutusha za watu kubakwa katika maeneo mengine ya Tigray.

Lakini kwasababu ya tatizo la usafiri hatukuweza kuwasaidia.

Inasikitisha sana.

Daktari mwingine anayefanyakazi katika hospitali ya Mekelle alisema kuwa hivi karibuni wanawake watano au sita wamekuwa wakienda hospitalini kutafuta matibabu dhidi ya maambukizi ya virusi vya ukimwi na dawa za dharura za kuzuia mimba kwa madai yanayohusishwa na ubakaji.

Weyni Abraha, ambaye anatoka kundi la kutetea haki za wanawake huko Tigray Yikono na alikuwa Mekelle hadi mwisho wa Desemba ameliambia shirika la BBC kwamba anaamini kuwa ubakaji unatumiwa kama silaha katika vita hivyo.

''Wanawake wengi wamebakwa huko mji wa Mekelle. Na hili linafanywa kwa maksudi kuvunja maadili ambayo yamekuwepo, kuwatishi na kuwashinikiza waachane na vita."

Mkuu wa jeshi la Ethiopia Birhanu Jula Gelalcha amekanusha madai hayo.

"Vikosi vyetu vya ulinzi havibaki. Wao sio waasi. Ni jeshi la serikali. Na jeshi la serikali lina maadili na sheria za kufuata," ameiambia shirika la habari la BBC.

Atakilty Hailesilasse, meya wa muda wa mji wa Mekelle aliyeteuliwa, alisema idadi ya makundi ya kutetea haki za binadamu imetilia chumvi idadi ya waliobakwa.

Serikali hivi karibuni ilituma jopo kazi lake katika eneo la Tigray kuchunguza madai hayo, ikiwemo wajumbe kutoka wizara za wanawake na afya na ofisi ya mwanasheria mkuu ambao wamebaini visa vya ubakaji vilivyotokea ingawa ripoti yao kamili bado haijachapishwa.

Wiki jana, Tume ya Haki za Binadamu nchini Ethiopia imesema visa 108 vya ubakaji vimeripotiwa katika kipindi cha miezi miwili iliyopita eneo la Tigray ingawa ilikubali kuwa "mifumo ya eneo kama polisi na vituo vya afya ambako waathirika wa unyanysaji wa kingono kawaida wangekimbilia na kuripoti visa hivyo havipo tena".

'Nilitaka kuwa mhandishi'

BBC ilijulishwa kesi ya Abiy Addi na daktari baada ya msichana huyo kukatwa mkono.

Yeye pamoja na babu yake walielezea vile walivyopatikana na wana wanajeshi wa Eritrea siku mbili baada ya kushambuliwa ambao walikuwa wakifanya msako katika eneo hilo - ingawa Ethiopia na Eritrea nchi zote mbili zimekanusha kujihusisha na vita vya Tigray.