Kiongozi mwigine wa chama cha NLD kinachoongozwa na Aung San Suu Kyi akamatwa Myanmar

Win Htein (kushoto) ni kiongozi wa juu wa chama cha NLD kinachoongozwa na Aung San Suu Kyi (kulia)

Chanzo cha picha, AFP

Wanajeshi nchini Myanmar wanamshikilia kiongozi mwingine mwandamizi kutoka chama cha Aung San Suu Kyi cha National League for Democracy party NLD, katika juhudi za kuendelea kuishikilia nchi hiyo.

Win Htein alichukuliwa kutoka nyumbani kwake Yangon mapema siku ya Ijumaa. Katika mazungumzo kwa njia ya simu na BBC, amesema amekamatwa chini ya sheria za uchochezi na kupelekwa kwa mji mkuu, Nay Pyi Taw. Kiongozi huyo mwenye miaka 79 amesema viongozi wa mapinduzi wanaohia kauli zake zinazoyapinga mapinduzi hayo.

Siku ya Alhamisi, Baraza la Usalama la umoja wa mataifa lilitoa wito kwa maafisa wa jeshi nchini Myanmar kumwachilia Aung San Suu Kyi na viongozi wengine waliowekwa kizuizini licha ya kwamba hawakukemea mapinduzi hayo. Saad Hammadi, kutoka Amnesty International, ameiambia BBC hali hiyo iliacha maswali ikiwa wakimbizi wengi wa Rohingya wanaoishi katika kambi za Bangladesh wanaweza kurudi Myanmar salama.

"Mapinduzi haya ya kijeshi, haswa na taasisi hii ambayo ina damu mikononi mwake kwa uhalifu wa kutisha ambao umefanya dhidi ya Warohingya na makabila mengine madogo, kwao kurudi madarakani nchini Myanmar hakika inapunguza ujasiri wa kuboresha hali katika nchi na kurudishwa salama, achilia mbali kuhakikisha haki na uwajibikaji. " Alieleza.

Ijumaa alasiri, mamia ya waalimu na wanafunzi pia walikusanyika nje ya chuo kikuu, ambapo walikua wakionyesha ishara mbalimbali kuashirika kuyakataa mapinduzi hayo.

Jeshi lilipindua serikali ya Bi Suu Kyi baada ya kudai uchaguzi wa Novemba ambao chama cha NLD kilishinda, ulikuwa wa ulaghai, ingawa Tume ya uchaguzi ya nchi hiyo ilisema hakuna ushahidi wa kuthibitisha madai hayo.

Hatua hiyo ilisababisha jumuia mbalimbali za kimataifa kulaani kitendo hicho na kutishia kuiwekea Myanmar vikwazo.

Katika taarifa yake ya hivi karibuni, Rais wa Marekani Joe Biden alitoa wito kuwaachilia wanasiasa, maafisa na wanaharakati waliowekwa kizuizini.

Marekani tayari ilikuwa imetishia vikwazo vikali kwa Myanmar, ambayo pia inajulikana kama Burma.

Tayari makampuni mbalimbali ya vinywaji, mawasiliano na hata usafiri yametishia kufuta uhusiano wake na nchi ya Myanmar kutokana na mapinduzi hayo, huku baadhi ya nchi za Kusini Mashariki mwa bara Asia nazo zikionesha dalili ya kufuata mkondo huo.

Huku hayo yakiendelea, maandamano bado yamepamba moto katika viunga mbalimbali vya miji ya nchi hiyo. Lakini ni kwa namna gani maandamano haya yatabadilisha msimamo wa jeshi na hatimaye kuwaachilia wanasiasa na wanaharakati wanaoshikiliwa? Huenda ni jambo la kusubiri.